Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lomalisa akifichua siri ya kambi Yanga "Mazoezi ni magumu"

Joyce Lomalisa Mutambala Lomalisa akifichua siri ya kambi Yanga

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga imerejea nchini alfajiri ya jana kutoka Algeria baada ya kutoka kugongwa mabao 3-0 na CR Belouzdad, huku beki wa kushoto wa timu hiyo, Joyce Lomalisa akifichua siri ya kambi akisema licha ya klabu yao kubanwa na ratiba ngumu, lakini wamepania kufanya makubwa kwenye michuano yote.

Yanga ilikuwa Algeria na kukumbana na kipigo cha mabao 3-0 kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika inayoshiriki baada ya kupita miaka 25 ilipocheza kwa mara ya kwanza 1998, lakini ikikabiliwa na kazi ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Kwa kutambua ugumu wa mechi zote, hasa baada ya kupoteza Ngao ya Jamii kwa watani wao, Simba, beki Lomalisa alisema wachezaji wa timu hiyo wamekuwa wakijipanga sambamba na benchi la ufundi la timu hiyo ili kuhakikisha kila shindano wanaloshiriki wanafanya vyema kuendelea kuwapa raha mashabiki.

Akizungumza nasi mapema kabla ya kusepa Algeria, Lomalisa alisema kile kinachoonekana kwa timu hiyo kinavyocheza kwa kupiga mpira mwingi na wakati mwingine kushinda mechi ngumu kirahisi, inatokana na jinsi wanavyojifua kambini kwa mazoezi magumu yakiwa na lengo la kutimiza malengo matatu waliyonayo kwa sasa kutetea tena Ligi Kuu, ASFC na kufika mbali kwenye mechi za CAF.

Msimu uliopita Simna ilitetea mataji matatu ikiwamo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na ASFC kwa msimu wa pili mfululizo, mbali na kufika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kupoteza mbele ya USM Alger ya Algeria iliyoshinda jijini Dar es Salaam 2-1 na kupasuka 1-0 ikiwa kwao, lakini kanuni ya bao la ugenini ikwabeba Waalgeria licha ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2.

Lomalisa alisema kazi ngumu katika kikosi chao ipo mazoezini ambapo hakuna mchezaji anakuwa na amani kutokana na ugumu wa mazoezi na kimbembe kinaanzia kwa kocha wa mazoezi Taibi Lagrouni ambaye ana mazoezi makali, hata hivyo yanawasaidia kuwa wepesi kwenye mechi zao ili kutimiza malengo ya msimu.

Beki huyo aliongeza ukiacha mazoezi ya Lagrouni pia wanapohamia upande wa ufundi huko wanakutana na Miguel Gamondi, ambaye ni kocha mkuu anayependa timu icheze kwa ubora na malengo uwanjani kwa kila mechi, hata inapotokea wamepoteza iwe ni kutokana na matokeo ya kawaida ya soka.

“Sio rahisi kabisa tunapokuwa mazoezini kuna wakati tunaomba mechi zifike mapema ni bora kucheza mechi kuliko kuwa mazoezini, mazoezi yetu ni makali sana. Tunapoanza yale ya viungo, hicho ndio kipindi kigumu zaidi kwani kocha Lagrouni ana mazoezi makalim, japo yanatusaidia kuwa kwenye ubora,” alisema Lomalisa na kuongeza;

“Tukihamia mazoezi ya ufundi tunakutana na Gamondi nako kuna ugumu kama hutaweza kucheza kwa ubora anaoutaka utapoteza nafasi, ni kocha makini sana akisaidiana na kocha Mussa (N’dew), naona kabisa tukizidi kuwa kwenye ubora ule ule.”

Beki huyo Mkongo aliongeza pia ushindani wa nafasi baina ya wachezaji nalo ni kitu kingine kinachoifanya timu kuwa imara zaidi kwani, kila mchezaji anapenda kuwa fiti na kiwango kizuri ili kujihakikisha namba.

“Msimu huu tuna timu bora zaidi kila mchezaji ana ubora mkubwa wale wanapata nafasi hawataki kufanya makosa na wanaosubiri nao wana ubora na wanashindana mambo haya ndio yanatuongezea nafasi ya kuendelea kuwa imara zaidi ndio maana naona tikifika mbali ndani na kule kimataifa, labda itokee tu.”

Chanzo: Mwanaspoti