Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Liverpool yaingilia dili la Branthwaite kwenda United

Jarrad Branthwaite Jarrad Branthwaite

Sat, 24 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mabosi wa Liverpool wanataka kuingilia kati dili la beki wa kimataifa wa England anayekipiga Everton, Jarrad Branthwaite, 22, kwenda Manchester United dirisha hili.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun, Liverpool inataka kutoa Pauni 63 milioni pamoja na nyongeza ya Pauni 7 milioni kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kumsajili staa huyo.

Branthwaite ni miongoni mwa wachezaji waliotajwa kutaka kusajiliwa na Man United tangu kuanza kwa dirisha hili lakini changamoto kubwa ni kiasi cha pesa kinachohitajika na Everton.

Everton inadaiwa kuhitaji kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni ili kumuuza beki huyu, lakini vigogo wa Man United wanataka kutoa Pauni 60 milioni pekee.

Hakuna uhakika wa asilimia 100 ikiwa Everton itakubali ofa ya Liverpool ambayo ipo tayari kutupa pesa yote, lakini Pauni 7 milioni itatoa kulingana na kiwango ambacho staa huyo atakionyesha.

Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 43 za michuano yote na kufunga mabao 10.

Raheem Sterling

WAWAKILISHI wa winga wa Chelsea, Raheem Sterling, 29, wamewasiliana na Aston Villa ili staa huyo atue kwenye timu hiyo katika dirisha hili lakini Kocha Unai Emery inadaiwa ndiye kikwazo kwani haoni kama staa huyo ataweza kuingia kwenye mfumo wake kutokana na staili yake ya uchezaji. Mkataba wa sasa wa Sterling unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na baadhi ya timu za Saudia zilimhitaji lakini amekataa.

Aaron Ramsdale

SOUTHAMPTON inataka kutuma ofa kwenda Arsenal kwa ajili ya kumsajili kipa wa kimataifa wa England, Aaron Ramsdale, 26, katika dirisha hili. Rasmdale inadaiwa anataka kuondoka Arsenal dirisha hili kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha washika mitutu hao. Mkataba wa Ramsdale mwenye umri wa miaka 26 unamalizika mwaka 2026.

Eddie Nketiah

MABOSI wa Arsenal wanatarajiwa kumruhusu straika wa timu hiyo, Eddie Nketiah, 25, kwenda kufanya vipimo vya afya kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wa kujiunga na Nottingham Forest ndani ya siku chache zijazo. Hivi karibuni Nottingham ilidaiwa imefikia makubaliano ya kutoa Pauni 30 milioni kwa ajili ya kumnunua Eddie.

Samu Omorodion

ASTON Villa inadaiwa ipo katika mazungumzo na wawakilishi wa straika wa Atletico Madrid, Samu Omorodion ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Alaves. Straika huyu raia wa Hispania wawakilishi wake wameingia katika mazungumzo na Villa baada ya dili lake la kwenda Chelsea kukwama. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.

Andreas Christensen

TOTTENHAM na Manchester United zinataka kutuma wawakilishi wao kwenda Hispania kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mabosi wa juu wa Barcelona ili kuipata huduma ya beki wa timu hiyo na Denmark, Andreas Christensen, 28, katika dirisha hili. Msimu ulipita alicheza mechi 42 za michuano yote, Barca inaonekana kuwa tayari kumwachia kutokana na hali yao ya kiuchumi.

Mats Hummels

BRIGHTON, Real Sociedad na Real Mallorca zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya beki wa zamani wa Borussia Dortmund, Mats Hummels, 35, ambaye kwa sasa yupo huru baada ya kumaliza mkataba wake na Dortmund. Awali Hummels alitajwa kuwa katika rada za baadhi ya timu za Marekani lakini ameonyesha kuwa bado anahitaji kucheza soka la kiushindani.

Kieran Trippier

EVERTON, AC Milan, Bayern Munich na timu mbalimbali kutoka Uturuki zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili beki kisiki wa kimataifa anayekipiga Newcastle United, Kieran Trippier, 33, katika dirisha hili. Kieran mwenye umri wa miaka 33, ni kati ya wachezaji walioonyesha kiwango bora katika kikosi cha kwanza cha Newcastle kwa msimu uliopita. Mkataba wake unamalizika mwaka 2026.

Chanzo: Mwanaspoti