Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lishe kwa mastaa Ligi Kuu Bara ni ishu kubwa

Lishe Bora.jpeg Lishe bora kwa wachezaji wa Mpira

Sun, 28 Aug 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Lishe ni kipengele muhimu kwa wachezaji kutokana na namna ambavyo wanavyotumia nguvu nyingi katika majukumu yao.

Kutokana na majukumu makubwa ndani ya uwanja mchezaji anatakiwa kutumia mlo kamili ambao unahitajika kuwa na wanga, vitamini, protini sambamba na maji kwa wingi.

Makala hii inakujuza namna lishe inavyofuatwa katika baadhi ya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

MTAALAMU WA LISHE

Daktari wa masuala ya lishe (Nutritionist) Hadija Lyellu anasema, mchezaji anatakiwa kula mlo kamili ambao unajumuisha makundi yote ya vyakula. Anasema akikamilisha chakula cha makundi yote matatu kwa maana ya (wanga, vitamini, protini) anatakiwa kutumia maji ya kunywa kwa wingi kutokana na nguvu na jasho linalomtoka wakati akiwa katika majukumu yake.

“Mchezaji anatakiwa kupata chakula saa mbili kabla ya kwenda kufanya mazoezi maana mmeng’enyo wa chakula chake unachukua muda, hivyo anatakiwa kujipa muda sahihi kutokana na nguvu anayoitumia uwanjani.”

Anasema baada ya kucheza mpira anatakiwa kupata chakula kizito na maji ya kutosha, akiwa anacheza anatakiwa kunywa maji kiasi ili yasimfanye akashindwa kukimbia.

‘’Asubuhi mchezaji kula chapati sio shida ila anatakiwa kuongezewa walau supu, yai la kuchemsha na tunda lolote lenye sukari asilia.

‘’Baada ya mazoezi anatakiwa kula karanga, korosho, dafu, mchana akila ugali sio mbaya lakini atumie unga ambao nafaka yake haijakobolewa, unakuta mchezaji anakula ugali na samaki mdogo, sio sawa kwani anatakiwa awe hata nusu na mboga za majani za kutosha hapo sawa.

“Mchezaji anatakiwa kula ndani ya muda, hata akitumia mlo kamili asipofuata muda ni ngumu sana, pia matumizi ya pombe kwa wachezaji yanatakiwa kuwa na kipimo asinywe sana.”

MADAKTARI NAO

Dk. Nassor Matuzya aliyewahi kuwa daktari wa Yanga anasema, mchezaji anatakiwa kupata mlo kamili, na aina ya vyakula anavyotumia havitakiwi kupita kiwango. Chakula chake kisimfanye kuwa mwepesi na mzito zaidi, lakini kinatakiwa kuwa katika makundi matatu.

“Makundi hayo ni la kuujenga mwili, kuulinda pamoja na kuutia nguvu.Mchezaji akikosa vyakula vya aina hiyo hata nguvu uwanjani inakuwa shida kwake,” anafafanua.

Daktari. Juma Sufiani anasema, kwa mchezaji lishe ndio kila kitu, hivyo asipoifuata kutakuwa na kitu kinapungua ndani yake.

“Mchezaji akiwa hafuati lishe kamili hata mikikimikiki ndani ya uwanja ataonekana anaonewa tu na wenzake kumbe tabu anayo mwenyewe,” anasema Dk. Sufiani.

YANGA MLO KAMILI

Ukubwa wa Yanga katika suala la mlo kamili linazingatiwa ndio maana wachezaji wake wanakuwa na nguvu za kutosha kuweza kustahimili dakika 90 uwanjani.

Daktari wa Yanga, Shecky Mngazija anasema wachezaji wote wanatumia mlo kamili, vyakula ambavyo vinajenga akili na utimamu wa mwili na kuzingatia vinywaji salama.

Mngazija anasema wachezaji wanahitaji nguvu kwa asilimia kubwa hivyo wanawapa kipaumbele kwenye vyakula vya wanga kwa 70%, protini 15%, mafuta 10%, madini na vitamini 5%.

“Tunapendelea kuwapa vyakula vya wanga kama mihogo, mahindi kwa kuwa vina wanga mwingi, pia matunda, maji na mboga za majani kwa wingi kwa kuwa tunaamini afya bora ndio mtaji wa wachezaji kwa kufikisha malengo ya timu,”anasema Mngazija.

Mngazija hakuishia hapo alisema aina ya vinywaji wanavyowapatia: “Wachezaji wetu mbali na maji, kinywaji pekee tunachowashauri kutumia kwa wingi ni juisi ya matunda asilia na hatuweki sukari yoyote kwa kuwa sukari haturuhusu kutumia pasipo kuichemshwa jikoni.

“Katika vyakula ambavyo tunazuia kwa wingi ni matumizi makubwa ya protini kwa wachezaji wetu kwasababu ikitumika kwa wingi inasababisha kuongezeka kwa mafuta na uzito, hivyo inamnenepesha mchezaji, pia matumizi makubwa ya chumvi ni kitu tunazingatia sana,”anabainisha.

Aidha Mngazija anasema: “Pombe ni moja ya kileo ambacho haturuhusu wachezaji wetu kutumia kwani hukausha maji mwilini kwa kiwango kikubwa, unapokunywa lita moja na unapoenda haja ndogo unapoteza lita moja na robo ya maji jambo ambalo ni muhimu kwa mchezaji,”

“Vinywaji vya kuongeza nguvu ‘energy’ na soda haturuhusu kabisa kwa sababu soda zinabeba sukari nyingi sana ambazo ni hatari kwa afya zao hasa mapigo ya moyo na uzito,” anafafanua Mngazija.

AZAM FC

Licha ya uchanga wake timu hii iliyopanda Ligi Kuu mwaka 2007 ni moja kati ya klabu zinazozingatia mlo kamili kwa wachezaji wake.

Daktari wake, Mwanandi Mwankemwa anasema pindi wakiwa kambini wachezaji wao wanatumia vyakula anavyovipendekeza kwa wakati husika.

“Wachezaji wetu wanapotoka kambini kwenda makwao kufahamu kama wanafuata ratiba kamili ya mlo ni ngumu, lakini kwa mchezaji anayejitambua anafuata tunawasisitiza sana katika hilo,”anasema.

Anasema vyakula vimegawanyika katika makundi mbalimbali ambayo ni wanga, mafuta, protini, maji, vitamini na madini.

“Vyakula vya wanga kama mihogo, wali, ugali, mikate na vyenye asili ya maziwa vinatengeneza sukari na kuupatia mwili nguvu.

“Aina ya pili ya vyakula vya mafuta yako katika aina mbalimbali yanayoleta joto na nguvu mwilini yanapatikana kwenye nyama, mbogamboga na vyakula vyenye asili ya karanga pia inaongeza joto mwilini.

“Kundi la tatu ni protini inajenga mwili mchezaji akifanya mazoezi zinapungua mwilini na inapatikana katika samaki, maharage na karanga nk, maji ni karibu asilimia 60 ya mwili wa mwanadamu lengo kubwa ni kukontroo joto pamoja na kutoa hewa chafu mwilini.

“Kundi jingine ni vitamini hizi zinasaidia kemikali mbalimbali mwili kuzuia damu kutoganda, inasaidia kutoa sumu mwilini na kuweka sawa seli za mwili zinapoharibika, hii inapatikana hasa katika matunda, samaki na nk,”anasema Mwankemwa.

Anaongeza kundi jingine ni madini ambayo yana maana kubwa kwa wachezaji hasa madini ya sodium yanayopatikana kwenye chumvi yanafanya kazi kusaidia mishipa ya fahamu na misuli.

“Kuna madini ya chokaa yanajenga mifupa na madini ya chuma kuweka damu sawa, mchezaji kupata mlo kamili vyakula vyake vinatakiwa kuwa na mchanganyiko wa vyakula hivyo,” anasema.

KUTOFUATA LISHE

Mwankemwa anasema ndani ya uwanja kipa anakimbia kilomita sita (6) katika mchezo ila wachezaji wa mbele na katikati wanakimbia kilomita kuanzia 8-10 huku mabeki wakitumia kilomita 12 kama hajafuata lishe hawezi kufikia lengo lake ndani ya uwanja.

“Anaweza akapungukiwa madini ya chuma akawa na damu kidogo matatizo ya madini ya chokaa akavunjika kirahisi, hivyo basi ni muhimu sana mchezaji kufuata lishe, ina maana kubwa sana kwao na sio kujilia tu.”

CHAKULA KINGI / KIDOGO

Mwankemwa anasema, sababu za mtu kula chakula kingi ama kidogo inategemea mwili ukoje.

“Tofauti pia ya umri mfano mchezaji wa U-17 hawezi kula chakula sawa na mchezaji mkubwa. Mkubwa ana mahitaji makubwa zaidi na mtu mwingine anakuwa na mwili mkubwa hawezi kula chakula kidogo.”

Huku Dk. Hadija anasema “Kuna mchezaji anakuwa na mwili mdogo mwingine mwili mkubwa hivyo hawawezi kula chakula kinacholingana, cha msingi wote wafuate mlo kamili basi.”

WASIKIE WACHEZAJI

Mchezaji wa Geita Gold, Juma Mahadhi anasema, timu ndogo kuzingatia suala la lishe ni changamoto kubwa sana, lakini kwa mchezaji anayetambua umuhimu anajiongeza mwenyewe.

“Nakumbuka nilipokuwa Yanga daktari anaenda jikoni achana na ufundi wa mpishi lakini mkono wake unakuwepo ndio maana wachezaji wa timu kubwa wanaonekana tofauti na hizi timu nyingine.

“Timu nyingi ndogo wachezaji wanakula ili washibe tu sasa kama sisi tunaojua umuhimu wa lishe unaamua kujiongeza hata kuweka tunda au kitu chochote lakini wanakuona una mashauzi.”

Aidha Mahadhi anasema, wachezaji wa timu ndogo wanaonekana kukomaa lakini wakienda Simba, Yanga na Azam mwezi mmoja tu wanabadilika kutokana na timu hizo kuwalea kwa kufuata utaratibu.

Raizin Hafidh aliyekuwa mchezaji wa Mbeya Kwanza anasema timu nyingine wachezaji wanajilia tu ilimradi wasife njaa.

“Timu nyingi asubuhi wachezaji tunakula chapati mbili na chai ya rangi, mchana ugali samaki au nyama, ila usiku wali maharage ‘never miss’, hapo mchezaji usipojiongeza ni kazi sana,”anasema.

Hafidhi anasema mwili unakosa nguvu kwa sababu wachezaji wakiwa uwanjani mazoezi yanakuwa magumu, hivyo wasipopata chakula sahihi mwili hauwezi kustahamili.

“Ikitokea maandalizi ya mchezo wa Simba au Yanga yanakuwa mazuri sana hata chakula chake kinakuwa kizuri sana, baada ya hapo mambo yanaenda kama yalivyokuwa awali,” anasema.

Mchezaji mmoja (jina tunalo) aliyewahi kuitumikia Yanga miaka ya hivi karibuni na kuhamia timu nyingine anasema, timu ndogo chakula wanakula tu ili washibe na ndio maana wachezaji wanakosa nguvu kama wa timu za Simba, Yanga na Azam FC.

“Huku ni ngumu sana. Mshahara ukiingia najiongeza chumbani kwangu utakuta korosho, karanga na vitu vingine ambavyo. Hata kupata samaki kwenye timu ndogo ilikuwa kazi sana,”

“Nilivyokuwa Yanga unapewa bakuli kubwa la supu na nyama kibao lakini huku kupata supu hiyo mpaka ujiongeze mwenyewe na hata huo wali samaki ni kasamaki kadogo kama unaonja vile,” alisema staa huyo.

VIONGOZI WA TIMU

Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania Robert Munis anasema, suala la wachezaji kufuata taratibu za lishe ni gumu na wengi wao linawashinda.

“Chakula cha mchezaji hakitakiwi kuwa na mafuta mengi hata sisi viongozi tunafuata taratibu kile ambacho daktari wetu anatuambia tukifuate, akisema wachezaji wetu wanatakiwa kula kitu fulani sisi tunanunua.

“Shida inakuja kwao hawataki kabisa kula chakula hicho mara nyingi kinapikwa bila ya mafuta na wao wanapenda vilivyoungwa, kuna wakati hadi chakula kinamwagwa,” anasema Munis.

Aidha anasisitiza ikitokea zikapikwa chipsi na kuku siku hiyo ni ngumu kukuta chakula kimebaki.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ anasema uongozi ni jukumu lao kuhakikisha kila kitu kinachohitajika kwa mchezaji kinapatikana kwa wakati.

Simba mchezaji hawezi kula chakula ovyo ovyo, kile chakula kinachoandaliwa na mpishi wao ni kutokana na matakwa ya daktari husika.

“Daktari wetu anatuambia leo asubuhi wachezaji wanatakiwa hiki, mchana hivi na usiku ni hivi tunachokifanya ni utekelezaji tu kwa mpishi.

“Anajua wachezaji wanatakiwa nini kwa kushirikiana na mpishi na sisi kama viongozi jukumu letu ni kuhakikisha kinachohitajika kinapatikana,” anasema Try Again.

SIMBA WAKO MAKINI

Mpishi wa Simba, Samwel Mtundu ‘Sam’ anasema anapika chakula freshi kila siku kutokana na mahitaji husika ya siku.

“Kama ni mchicha unatoka kuchumwa kabisa shambani, nyama inatoka Buchani siku husika, hata kuku wanatoka kuchinjwa siku hiyo na hata upishi wake mafuta sio sana katika chakula chao,”anasema.

Anasema mwanzo alipata wakati mgumu kukiandaa chakula chao kutokana na mambo kuwa mengi tofauti na chakula cha kawaida.

Anaeleza ugumu anaokutana nao katika kuandaa chakula cha wachezaji tofauti na huko nyuma wakati akipika katika mahoteli mbalimbali.

Anabainisha kuwa, kazi ya kupika chakula chao ni ngumu lakini kwa kuwa anajua nini anakifanya ndio maana anaweza kutimiza majukumu hayo bila shaka kabisa.

Anasema wachezaji wana vvyakula vyao fulani hivi ambavyo daktari ndiye anayesema wale hiki au wasile hiki yeye kama mpishi anafuata mwongozo.

“Inategemeana na aina ya wakati na mabadiliko ya chakula yanaangalia ni ya aina gani ya mechi ambazo wanakutana nazo na eneo husika kisha mimi nafuata maelekezo zaidi.

“Mfano tunaenda kucheza mechi ngumu wachezaji wanatakiwa kula vyakula vyenye wanga mwingi, na vile ambavyo havina mafuta mengi zaidi ya mchemsho,” anasema.

Mpishi wa moja kati ya timu za chini ambaye hakutaka kuandikwa jina lake anasema, timu hiyo (jina tunalihifadhi) ilimradi wachezaji wanakula ila hawazingatii lishe kabisa kama ilivyo kwa timu za hapo juu.

“Kufuata taratibu za kumhudumia wachezaji kwa kadiri inavyotakiwa ni kazi sana.

“Timu hizi ndogo nyingi haziwezi kufuata ratiba na kuzingtia ulaji mzuri kwa wachezaji wao,” anasema na kuongeza:

“Timu zinazoweza kufanya hivyo ni chache sana ila huku kwetu ni ngumu.

“Hata kwenye chai tukisema mayai ya kuchemsha hiyo ni gharama ya mboga mchana jambo ambalo ni changamoto kubwa,” anasema mtoa habari huyo ambaye hakutaka kutajwa.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz