Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Argentina, Lionel Scaloni amegoma kuweka ukomo wa Lionel Messi kucheza kuitumikia timu hiyo.
Messi, alikuwa nahodha wa Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar na kuiongoza nchi yake kushinda taji hilo mwaka 2022 ambapo pia alitajwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo.
Alipoulizwa kwenye mkutano na waandishi wa habari, Scaloni alisema: “Tuliweke akilini mwetu kwamba Messi bado ni mchezaji wa timu hii. Tunatakiwa kuwaza tofauti atakapoondoka.
“Ukweli ni kwamba bado anacheza soka la ushindani, achaneni naye, tuko tayari kumstaafisha? Tutakuwa wendawazimu.”
Messi aliingia akitokea benchi na kucheza dakika 40 kwenye ushindi wa bao 1-0 wa Argentina dhidi ya Paraguay Alhamisi iliyopita mchezo wa kufuzu kwa fainali hizo.
Mshambuliaji huyo wa Inter Miami alifunga kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ecuador lakini baadae alikosa mchezo wa pili wa kufuzu wa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Bolivia ambao Argentina waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Argentina imeshinda mechi zake zote tatu za kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 na wanaongoza kundi kwa pointi mbili mbele ya Brazil.