Wakati Ligi Kuu ikiwa imesimama kwa muda kupisha kalenda ya Fifa, jumla ya timu 10 zipo mtegoni huku presha ikiwa kubwa kwa makocha katika vita ya kukwepa kushuka daraja kufuatia matokeo yasiyoridhisha.
Ligi Kuu imesimama kwa sasa ambapo inatarajia kurejea Aprili 12 kwa mechi kadhaa kupigwa kabla ya kuendelea kwa ratiba hiyo kwa michezo ya raundi ya 21 kwa timu hizo kuwania ubingwa, kubaki kwenye ligi na kushuka daraja.
Hadi sasa timu sita ndizo zipo katika hesabu nzuri ikiwa ni Yanga wanaoongoza Ligi hiyo kwa pointi 52, Azam akifuata kwa alama 47, Simba 45, Coastal Union 30, Tanzania Prisons akiwa na 28 sawa na KMC.
Timu 10 zimejikuta katika likizo ya ‘mtego’ na presha kwa makocha wao kutoweza kula bata hadi baadhi kuamua kuzuia mapumziko kuhakikisha wanaendelea kujifua kujiweka sawa na mashindano hayo.
Mbali na Ligi Kuu, timu hizo zinakabiliwa pia na kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na ni Prisons pekee iliyotolewa katika michuano hiyo ilipokubali kulala kwa penalti 5-4 dhidi ya TRA ya First League katika hatua ya 32.
Timu zinazopigania kubaki au kushuka daraja ni Singida Fountain Gate walio nafasi ya saba kwa pointi 24 sawa na Kagera Sugar na Namungo (23) sawa na Dodoma Jiji na Ihefu huku Mashujaa wakiwa nafasi ya 12 kwa pointi 21 sawa Tabora United na Geita Gold.
JKT Tanzania na Mtibwa Sugar ndio wapo katika msitali mwekundu wa kushuka daraja kwa pointi 20 na 16 na kuweka hofu kwa mashabiki wa timu hizo kwenye hatihati ya kushuka daraja.
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema kutokana na matokeo waliyonayo imewafanya kuwahi mapema kambini kuendelea na program kujiandaa na mechi zilizobaki akieleza kuwa matokeo ya mechi tatu za mwisho zimeongeza matumaini kwao.
“Tayari tumerejea kambini kuendelea na maandalizi ya mechi zetu za Ligi Kuu na Kombe la ASFC, hatuwezi kukata tamaa bali kupambania ushindi kwa michezo yote kisha kuona hatma yetu,” alisema Katwila.