Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi ya wanawake kuanza leo

Dd40cc6f5da369bb2e0b1566a79a0f2c.png Ligi ya wanawake kuanza leo

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

PAZIA la Ligi Kuu ya soka ya Wanawake Tanzania Bara,msimu wa tano linatarajiwa kufunguliwa leo kwa michezo sita kuchezwa katika viwanja vya miji tofauti.

Katika Uwanja wa Majimaji Songea, Ruvuma Queens itaialika Mlandizi Queens ya Pwani, mchezo utakaochezeshwa na Lugano Mbuba kutoka Songwe akisaidiwa na Sikudhani Mkurungwa wa Njombe na Yuster Weston kutoka Mbeya na mezani atakuwepo Aziza Ndimbaye.

Wageni katika ligi, Mapinduzi Queens ya Njombe itacheza na bingwa mtetezi Simba Queens katika Uwanja wa Sabasaba, ambapo waamuzi ni Amina Kyando wa Morogoro akisaidiwa na Anna Venance na Jane Mayala wote wa Morogoro na mezani atakuwepo Oresta Mbwilo.

Kigoma Sisters itakuwa kibaruani na Alliance Girls ya Mwanza katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, waamuzi ni Getrude Galves kutoka Kagera akisaidiwa na Leah Bake na Agnetha Mutabora kutoka Kagera na mezani ni Said Salum.

Wageni wengine ES Unyanyembe wataialika TSC ya Mwanza katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora ambao utachezeshwa na Ester Adalbert kutoka Singida akisaidiwa na Mwankasala Lugiluka na Aina Ismail kutoka Dodoma na mezani atakuwepo Justina Charles.

Kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam Yanga Princess itaialika Tanzanite Queens, mchezo utakaochezeshwa na Monica Wazael kutoka Singida akisaidiwa na Marry Seleman na Fatuma Salum kutoka Pwani na mezani atakuwepo Khadija Mastoka. JKT Queens ikiwa nyumbani katika Uwanja wa Meja Jenerali, Isamuhyo, Dar es Salaam itacheza na Baobab Queens ya Dodoma, mchezo utakaochezeshwa na Tatu Malogo kutoka Tanga, akisaidiwa na Martha John wa Tanga na Gladness Okeyo wa Pwani na mezani atakuwepo Halima Ally.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea na mzunguko wa pili Desemba 2 ambapo itachezwa michezo sita pia. Wakati huohuo Chama cha soka la wanawake nchini (TWFA) kinatarajiwa kufanya Mkutano wake Mkuu wa Mwaka Dar es Salaam leo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TWFA, Amina Karuma, alisema mkutano huo ni wa kawaida kwa kuzingatia katiba yao na utatoa fursa kwa wajumbe kujadili mambo mbalimbali ikiwemo maendeleo ya soka la wanawake nchini.

“Chama cha mpira wa miguu nchini (TWFA) kesho (leo) tutakuwa na Mkutano Mkuu wa kawaida wa mwaka kama katiba yetu inavyoelekeza na utafanyika katika Hoteli ya Itumbi hapa Dar es Salaam,” alisema Karuma

Chanzo: habarileo.co.tz