Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi ya wanawake inavyopambana kupoteza mafanikio yaliyopatikana

Timu Za Wanawake.png Ligi ya wanawake inavyopambana kupoteza mafanikio yaliyopatikana

Tue, 21 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL) imeanza kukua kwa kasi, kwani baadhi ya wachezaji waliowahi kucheza hivi sasa wanafanya vyema kwenye mataifa makubwa kisoka duniani.

Licha ya ukuaji huo, lakini kuna changamoto mbalimbali zinazolikumba soka hilo, hususan ratiba kwani klabu zinaanza maandalizi mapema bila kujua lini michezo hiyo inaanza.

Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisapoti michezo kwa asilimia kubwa, lakini WPL ndio inamuangusha.

Mwanaspoti kwa kuzingatia hilo linakuletea baadhi ya mambo ambayo ligi hiyo inamuangusha Rais Samia.

RATIBA

Kwa timu za wanaume ratiba inaonekana kuwa rafiki kwani ligi inapomalizka huchukua takriban miezi mitatu ndipo msimu mwingine huanza tofauti na wanawake ambao wanaweza kukaa zaidi ya miezi sita.

Mpaka sasa haijajulikana ligi hiyo itaanza lini kwa sababu tayari baadhi ya timu zimeingia kambini miezi zazidi ya miwili kuanza maandalizi.

Kwa kawaida ligi hiyo haina muda maalumu wa kuanza kama ilivyo kwa wanaume kwani inaweza kuanza Oktoba mwishoni au katikati ya Novemba kulingana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linavyoamua.

Tangu msimu wa 2022/2023 ulipomalizika ni miezi saba sasa imepita bila kujua dira ya ligi hiyo itaanza lini, kwani baadhi ya wachezaji wanazitumikia timu zao za taifa na wengine wamesalia kambini.

NGAO YA JAMII

Inasemekana msimu huu umekuwa na mabadiliko kwa ligi hiyo kwani kabla kuanza itaanza na Ngao ya Jamii. Timu nne zilizomaliza juu katika msimamo msimu uliopita zitakutana kukipiga zikiwa ni JKT Queens, Yanga Princess, Simba Queens na Fountain Gate Princess ndizo zitashiriki michuano hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Desemba.

Timu hizo zenye ushindani mkubwa zitacheza kuwania Ngao ya Jamii itakayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi, Dar es Salaam, huku Yanga Princess, Fountain Gate na Simba Queens zikiingia bila kushiriki mashindano yoyote kwa miezi sita tangu ligi ilipomalizika Mei, mwaka huu.

USAJILI

Hadi dirisha dogo linafunguliwa mwezi ujao, bado ligi haijaanza na baadhi ya timu zikiwa tayari zimesajili wachezaji wapya ambao hazijawatumia ili kutathmini ubora walio nao.

Yanga Princess na Fountain Gate ndizo ambazo dirisha kubwa zimesajili wachezaji huku JKT Queens ikiongeza baadhi ya wachezaji kikosini ingawa imetesti mitambo katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) pamoja na Klabu Bingwa Afrika iliyomalizika hivi karibuni nchini Ivory Coast.

Lakini, WPL inaanza timu nyingi zikiwa zimesajili wachezaji ambao hawajacheza mashindano yoyote, hivyo tangu ligi imalizike Mei na iwapo litafika dirisha dogo ina maana zitakuwa zimesajili mara mbili bila kucheza, iwapo zitasajili.

GEITA, BUNDA MAMBO MAGUMU

Geita Gold na Bunda Queens ndizo timu ambazo zimepanda Ligi Kuu msimu huu, baada ya Mkwawa Queens ya Iringa na Tiger Queens ya Arusha kushuka msimu uliopita zikiambulia pointi tatu na kuweka rekodi ya kutoshinda mchezo wowote.

Timu hizo mbili mpya katika mashindano hayo hazifahamu nini kinaendelea kwani hazijapewa ratiba na zipo kambini zikiendelea na maandalizi ya msimu mpya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Bunda Queens, Alley Ibrahim alisema ratiba imekuwa changamoto kwao, lakini hawana namna.

Anasema tangu wapande daraja wanaendelea na mazoezi huku wakisubiri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupanga ratiba ya kuanza msimu upya.

“Tuliambiwa ligi itaanza katikati ya mwezi wa 12, lakini mpaka sasa kimya hatujajua. Sisi tupo na maandalizi tu. Ni changamoto kubwa hatuna namna tunakabiliana nazo tu,” anasema Alley

Kiongozi wa Geita Gold ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema timu ipo kambini kwa baadhi ya wachezaji wakisikiliza ratiba ya TFF.

Anasema karibu wachezaji wanane wameitwa timu ya taifa, hivyo wengine wamesalia wakijifua, lakini hawajui lini ligi hiyo itaanza lini.

“Labda (TFF) wanaisubiri timu ya taifa kwanza ndio watoe mwongozo wa ligi, lakini kiukweli ratiba haijulikani, baadhi ya wachezaji wanaendelea na mazoezi,” anasema kiongozi huyo.

KILIO CHA KOCHA

Akizungumzia suala hilo, Kocha Mkuu wa Fountain Gate Princess, Masoud Juma anasema ratiba inawapa ugumu makocha na wachezaji kwani wana muda mrefu kambini bila kucheza mechi za mashindano.

Masoud anasema kwa kawaida mchezaji anapaswa kucheza mechi mara kwa mara hivyo kucheleweshwa kwa ratiba kunasababisha kuwapotezea nyota wao ubora.

“Tunaomba waandishi mtusaidie kupaza sauti hili suala la ratiba. Ukiangalia muda mrefu tunakaa bila ya kucheza, inakuwa ngumu hata kwa mchezaji. Utakuta mwingine kiwango chake kinashuka,” anasema Masoud

Chanzo: www.tanzaniaweb.live