Dar es Salaam. Ligi ya soka ya mchangani maarufu 'chandimu' imezinduliwa jijini Dar es Salaam ikishirikisha timu nane katika hatua ya awali.
Msimu wa Ligi hiyo ambayo imepewa jina la Sodo Bingwa Awards unashirikisha timu za mikoa sita nchini na inachezwa kwa kutumia mipira ya kufumwa na karatasi 'Chandimu' na wachezaji wakicheza bila njumu.
Ligi hiyo itachezwz hadi Desemba kabla ya mabingwa wa kila mkoa kuchuana kusaka bingwa wa taifa baadae mwaka huu.
Flora Chacha kutoka kampuni ya Betika iliyodhamini Ligi hiyo amesema uzinduzi wa mechi za awali kwa Dar es Salaam umetanguliwa na mchezo wa ngao ya jamii kati ya timu ya Gharama Ndogo dhidi ya Ajax.
Kabla ya mechi hiyo timu ya wafanyakazi wa Times FM ilicheza na wasanii wa Bongo Fleva walioongozwa na Inspekta Haroun, Juma Nature, KR Muller na Banana Zoro waliofungwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Sifa Temeke.
"Tunatambua mtaani kuna wachezaji vijana wengi wanapenda kucheza soka hali hiyo imetusukuma tudhamini michuano hii kuhakikisha tunaendeleza vijana hao katika wa soka," alisema Flora.
Alisema tayari mashindano hayo yamefanyika mikoa minne, ikiwemo Mbeya , Dodoma, Bukoba na sasa inafanyika jijini Dar es Salaam na mipango yao kwenda katika mikoa mingine miwili kabla ya timu zitakazofanya vizuri kutinga fainali baadae mwaka huu.
"Baada ya mikoa yote kumaliza Ligi yao, mabingwa wa kila mkoa watachuana kwenye fainali ya taifa kupata bingwa wa taifa wa Sodo baadae mwaka huu," amesema Flora.