Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi kuu yarejea na vita ya nafasi

Prisons Pcers Ligi kuu yarejea na vita ya nafasi

Fri, 12 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vita ya nafasi katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea leo wakati Tanzania Prisons inayonolewa na Ahmad Ally itaavaana na ya KMC Abdihamid Moalin kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mechi hii inasubiriwa kwa hamu kubwa kwa kuwa timu zote zimelingana pointi kila moja ikiwa nazo 28, Prisons nafasi ya tano na KMC ya sita.

Oktoba 27, 2023 KMC ilishindwa kutamba ikiwa nyumbani katika mchezo wa mwisho timu hizo kukutana baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na maafande hao ambao hawajapoteza katika michezo mitatu iliyopita wakiwa nyumbani, wamevuna pointi saba kwa kuzifunga Tabora United (2-1), Singida FG (3-1) huku wakitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC.

Takwimu zinaonyesha KMC haijashinda katika michezo mitatu iliyopita ikiwa ugenini, imeambulia pointi mbili tu mbele ya JKT Tanzania (1-1) na Singida FG (0-0) huku ikipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Ihefu.

Akizungumza na Mwananchi, Moalin alisema anaamini kwa maandalizi waliyofanya wanaweza kupata ushindi licha ya kukiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu.

"Haitakuwa mechi nyepesi kwa sababu Prisons ni miongoni mwa timu nzuri kwenye ligi na wamekuwa washindani wetu kwa miaka mingi, tumejiandaa kufanya vizuri ili kuendelea kusogea katika nafasi za juu, kila kitu kuhusu mchezo kipo tayari na wachezaji wangu wapo tayari," alisema kocha huyo.

Kwa upande wa kocha wa Prisons, Ahmad Ally alisema,"Tunaijua KMC na tumejiandaa nao, tunajua ubora wao ulipo hivyo tutahakikisha hatufanyi makosa ambayo yanaweza kutugharimu, tutatumia madhaifu yao kuwaadhibu."

Wazir Junior kwa KMC mwenye mabao 11 na Samson Mbangula (8) wa Prisons ndio wachezaji hatari zaidi kwenye vikosi hivyo ambao watakuwa wakitazamwa zaidi katika mchezo huo ambao utachezwa saa 8:00 mchana.

Mchezo mwingine ambao unatarajiwa kupigwa leo jioni ni kati ya Mashujaa dhidi ya Coastal Union ya Tanga utakaopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma ikumbukwe kuwa mwenyeji wa mchezo huo ametoka kuitoa Simba katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa mikwaju ya penalti (6-5).

Mara ya mwisho zilipokutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Mashujaa walikiona cha moto baada ya kuchapwa mabao 2-0.

Huu ni mchezo mwingine wa nafasi kwa kuwa Coastal Union ipo nafasi ya nne na pointi 30 baada ya kucheza michezo 21, kama itapoteza mchezo huu na Prisons kushinda itashuka hadi nafasi ya tano na kuwaacha Maafande hao wakwee nafasi ya nne kwenye msimamo.

Kwa Upande wa Mashujaa inatakiwa kufanya jambo lolote kupata ushindi kwa kuwa ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 21 katika michezo 21, ipo kwenye hatari ya kushuka daraja mwishoni mwa msimu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live