Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi kubwa Ulaya zatishia mgomo Klabu Bingwa Dunia

FIFA Club World Cup 2023 Ligi kubwa Ulaya zatishia mgomo Klabu Bingwa Dunia

Sat, 1 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi kubwa Ulaya pamoja na vyama vya wanasoka wa kulipwa wanaripotiwa kuungana na kuwaambia Fifa: “Hatutacheza Klabu Bingwa Dunia mnaua mchezo wa soka.”

Tishio hilo la mgomo linadaiwa kuongozwa na bosi wa Ligi Kuu England, Richard Masters, bosi wa chama cha wanasoka wa kulipwa, PFA, Maheta Molango na kigogo wa LaLiga, Javier Tebas.

Vigogo hao wamepanga kufungua mashtaka labda kama tu mashindano hayo yatakayohusisha timu 32 yatafanyiwa maboresho na kupangiwa upya ratiba yake baada ya hii ya sasa ya kufanyika majira ya kiangazi mwakani huko Marekani, huku kwa Ligi Kuu England timu zinazotarajia kushiriki ni Manchester City na Chelsea.

Vigogo wengine wa Ulaya watakaoshiriki ni Bayern Munich na Real Madrid na michuano hiyo ya wiki nne inakuwa na zawadi ya pesa, Pauni 600 milioni.

Mabosi wa Fifa mwanzoni hawakuwa na wasiwasi kabisa kuhusu ustawi wa wachezaji, lakini bosi wa wachezaji hao, Molango aliambia SunSport: “Soka imeamua kuua bidhaa yake mwenyewe. Wale watu wanaohusika na mchezo huu, wanapaswa kuwa wasikivu.

“Kama hawawezi, basi sisi kama chama tutawajibika kuchukua hatua kwa ajili ya wachezaji na kinachofuata basi ni hatua za kisheria zitachukua mkondo. Mamlaka za mchezo huu zilikuwa na nafasi nzuri ya kutushirikisha, lakini hawakufanya hivyo. Mzigo walionao wachezaji kwa sasa ni mkubwa mno. Ni jambo linaonekana wazi jinsi ratiba zinavyolazimishwa kuingizwa kwenye kalenda na hazifiti.”

Vyama vya kimataifa vya wachezaji FifPro na PFA vinaamini ratiba iliyopangwa itazifanya klabu kutokuwa na namna zaidi ya kuwalazimika wachezaji kurejea kwenye vikosi vyao bila hata ya kuwapa wiki tatu za mapumziko kama kanuni za soka la kulipwa zinavyoelekeza.

Wanasheria sasa wameambiwa kuandaa nyaraka muhimu kujiandaa na vita ya kisheria dhidi ya Fifa labda tu kama wataamua kurudi mezani na kubadili mambo.

Masters ndiye mkuu wa Chama cha Ligi za Dunia, ambayo inawakilisha ligi zote kubwa za soka duniani. Na kwamba bosi huyo alipanga kukutana na Tebas na Molango katika mkutano maalumu wa FifPro na PFA wa kujadili mzigo mkubwa unaowakabili wachezaji uliopangwa kufanyika jana Alhamisi huko London, England.

Na Molango aliongeza: “Hili ni tatizo kwenye mchezo wote wa soka.”

Chanzo: Mwanaspoti