Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi imeisha, timu zijapange msimu ujao

Paredi Yanga Neema.jpeg Ligi imeisha, timu zijapange msimu ujao

Mon, 27 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imetangazwa kuwa bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2023/24, mechi za mwisho zikitarajiwa kuchezwa kesho.

Ubingwa huo wa Yanga ni wa tatu mfululizo ikiipokea Simba iliyotoka kutwaa mara nne mfululizo kuanzia msimu wa 2017/18 mpaka msimu wa 2020/21.

Kutangazwa kwa Yanga kuwa mabingwa kunaashiria msimu wa ligi hiyo kufika mwishoni na sasa inachezwa michezo ya kukamilisha ratiba.

Kumalizika kwa msimu wa ligi kunaashiria kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Agosti mwaka huu kwa timu zilizobaki na zile zilizopanda daraja msimu huu.

Klabu ambazo zimepata bahati ya kupanda daraja na zile zilizobakia Ligi Kuu zianze sasa kujipanga kwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi hiyo.

Ubingwa wa Yanga au kufanya vizuri kwa klabu ya Azam FC havikuja kwa bahati, ni mipango na mikakati iliyowekwa na viongozi wa klabu hizo.

Kwa sasa mashabiki na wanachama wa Yanga wanatembea kifua mbele wakitamba kutokana na mafanikio ya timu yao.

Kwenye kila mafanikio kuna juhudi zilizofanywa. Ubingwa wa Yanga wa tatu mfululizo umetokana na juhudi za viongozi wake kuwekeza na kutengeneza kikosi bora.

Kumalizika kwa msimu huu sasa kunatoa fursa kwa klabu zingine kujiandaa kwa msimu ujao wa ligi uliopangwa kuanza miezi mitatu ijayo.

Kujiandaa ni pamoja na kuwa na benchi zuri la ufundi, kusajili wachezaji wazuri na wenye ubora pamoja na kufanya maandalizi mazuri kwa kikosi kizima.

Kengold FC na Pamba FC ni timu mpya Ligi Kuu msimu ujao, zinapaswa kujipanga vizuri ili kutoa ushindani wa kweli na kuendelea kusalia kwenye ligi hiyo.

Pamba FC imetumia zaidi ya miaka 20 kurejea tena Ligi Kuu, inapaswa kujipanga na kujiandaa vyema ili kuendelea kusalia kwenye ligi hiyo, vinginevyo irejee ilikokuwa.

Kwa timu ambazo zimebakia msimu huu wa Ligi Kuu na zilikuwa kwenye hali mbaya, ni wakati mwafaka kwao  kujipanga upya kwa kuandaa timu nzuri kwa ajili ya ushindani msimu ujao.

Mtibwa Sugar, moja ya timu ‘king’ang’anizi’ kwenye Ligi Kuu, iliyotwaa ubingwa mwaka 1999 na 2000 na haikuwahi kuporomoka daraja tangu ilipopanda Ligi Kuu, msimu huu imeshuhudiwa inashuka daraja na kwenda kucheza ‘Championship’. Hili halijatokea isivyo bahati.

Matokeo mabaya waliyokuwa wanapata kwenye mechi zao yamesababisha kushuka daraja. Ni funzo kwa timu nyingine kuhakikisha zinakuwa na timu nzuri ili kutoa ushindani.

Mtibwa ni kama chuo cha soka kwa wachezaji wazawa, wachezaji wengi wanaowika sasa wamepitia kwenye timu hiyo inayosifika kwa kutoa nafasi kwa vijana kuonesha vipaji vyao.

Tunataka kuona msimu ujao unakuwa na ushindani zaidi ya msimu huu, kila timu ijiandae na kujipanga, ifanye usajili mzuri na wenye tija kwa maendeleo ya timu.

Tunakumbusha klabu, ligi imemalizika na sasa zijipange kwa ajili ya msimu ujao, zisajili vizuri ili kuendelea kuiongeza thamani ligi yetu inayotajwa kuwa namba tano kwa ubora barani Afrika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live