Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu ya wanawake mambo ni moto

Yanga Princes 6 Ligi Kuu ya wanawake mambo ni moto

Sun, 31 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na Ligi Kuu Bara, kuna utamu mwingine wa Ligi ya Wanawake (WPL) unaoendelea viwanja mbalimbali nchini na baadhi ya timu zikianza vyema na nyingine zikiangukia pua.

Vigogo vya Simba, Yanga na JKT vimeanza kwa kishindo na kuumaliza mwaka vizuri huku timu zilizopanda daraja msimu huu zikimaliza mwaka kwa kilio baada ya kutofanya vizuri kwenye mechi mbili.

Mwanaspoti linakuchambulia raundi mbili za moto WPL ambazo zimetamatisha mwaka 2023.

YANGA, SIMBA BALAA JINGINE

Simba Queens na Yanga Princess zimeanza na moto Ligi Kuu kwani tayari imekusanya pointi sita kwa michezo miwili ikiwa sawa na JKT Queens na Alliance.

Mnyama huyo wa kike katika michezo miwili imefunga mabao 10 na kuruhusu mabao mawili, ikishinda mabao 5-0 dhidi ya Ceasiaa Queens na mchezo wa juzi ilishinda 5-2 dhidi ya Baobab Queens.

Kwa Wananchi, Yanga mechi mbili imefunga mabao manane na kati ya hayo mawili yakifungwa na straika mpya, Janeth Bundi na sita yakiwekwa kambani na mawinga na viungo.

Msimu huu hususan Yanga imeanza kwa kishindo na kama itaendelea hivyo basi inaweza kujiweka katika nafasi ya kutafuta ubingwa wa kwanza kwa Wananchi tangu ligi ilipoanzishwa mwaka 2016.

Staa kama Precious ambaye anamudu kucheza namba 10 na straika kwenye Michuano ya Ngao ya Jamii aliwika na namna ya uchezaji wake bado anaendelea kuonyesha kiwango bora na kuisaidia timu hiyo kwani kwenye mabao manane iliyofunga timu hiyo amehusika kufunga matatu na kutoa asisti moja.

JKT CHUPUCHUPU, ALLIANCE FRESHI

JKT nayo juzi ilikuwa na mechi ya pili dhidi ya Geita Gold Queens ilipoondoka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nyankumbu jijini Geita.

Haikuwa mechi ya kitoto kwani mpaka dakika 90 mechi ilikuwa sare ya 0-0 katika dakika za nyongeza Johari Shaban aliiandikia bao dakika za jioni.

Geita ilionesha upinzani mkali ikicheza kwa kuiheshimu JKT ambayo ni mabingwa watetezi wa WPL msimu uliopita na kuifanya mechi kuwa ngumu kwa dakika zote 90.

Mechi nyingine kali ilipigwa juzi kwenye Uwanja wa Karume Mara, kati ya Alliance Girls na Bunda na Alliance ikiondoka na ushindi wa mabao 3-2.

Hadi kipindi cha kwanza Bunda ilikuwa mbele kwa mabao mawili ndipo kipindi cha pili Alliance ilipobadilika na kurudisha mabao matatu yaliyoipa point tatu.

BUNDA, GEITA QUEENS NI VIPIGO

Ikumbukwe timu zote mbili zilipanda daraja msimu huu na tayari zimeanza na vichapo vya kukaribishwa kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Mechi ya kwanza Bunda ilipokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa JKT Queens na juzi ilichapwa mabao 3-2 dhidi ya Alliance Girls.

Geita ilipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Alliance kwa mabao 2-1 na juzi ikiikalia kooni JKT kwa kuruhusu tena bao 1-0.

WPL MAMBO NI MOTO

Hapa ndipo kuna balaa kwani Asha Mnuka, Asha Djafar wa Simba Queens na Precius Christopher (Yanga) ndio wanaongoza kwenye msimamo wa wafungaji wakitupia kambani mabao matatu kila mmoja.

Wengine ni Janet Bundi (Yanga Princess), Donisia Minja, Winifrida Gerald (JKT Queens), Amina Ramadhani (Fountain Gate Princess)na Nelly Kache wakifunga mawili kila mmoja.

Vita inakuja kwa watani wa jadi, Simba na Yanga ambao ndio wanaongoza kwa ufungaji kwa Asha ambaye mechi moja amefunga mabao matatu na Precious ambaye alifunga mabao mawili kwenye mechi moja.

MSIMAMO ULIVYO

Ushindi wa mabao 5-2 unaifanya Simba kukaa kileleni mwa msimamo ikiongoza kwa idadi ya kufunga mabao mengi, Yanga Princess ikishika nafasi ya pili huku JKT ikishika nafasi ya tatu ikifunga mabao matano.

Alliance iko nafasi ya nne ikikusanya point sita ikifunga mabao matano na kuruhusu mabao matatu huku Fountain ikiwa nafasi ya tano na pointi tatu na mchezo mmoja mkononi.

Kwa matokeo hayo yanaifanya Bunda na Geita kusalia mkiani baada ya mechi kupoteza point sita.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Amani Queens, Morice Katembo alisema sababu kubwa ya timu yake kuruhusu mabao 6-1 dhidi ya Yanga ni wachezaji kukosa kujiamini na kuchelewa kuingia kambini.

“Tulifanya makosa wenzetu wakapata mabao ya mapema, ukiangalia namna wachezaji wangu walivyocheza utaona hawana ufiti kwa sababu tuliingia kambini wiki mbili kabla ya michezo naamini mechi yetu ijayo dhidi ya JKT tutafanya vizuri,” alisema  Katembo

Kocha wa JKT Queens, Esther Chabruma alisema mchezo wa juzi ulikuwa mgumu na wenye ushindani kwani Geita Gold Queens walipaki basi wakiitaka point moja.

“Karibu wachezaji tisa wa Geita walirudi nyuma na ilikuwa ngumu  kufungua na kwani tulipata nafasi nyingi za mabao lakini shida ilikuja namna ya kuwafungua, tunashukuru dakika za jioni tukafunga bao na kuondoka na point zote tatu,” alisema Chabruma.

Kocha wa Yanga Princess, Charles Haalubono alisema wachezaji wake walicheza kulingana na walivyofundishwa mazoezini na anaiona kasi ya ushindani katika kikosi chake.

Chanzo: Mwanaspoti