Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu machozi, jasho na damu

95305 Simba+pic Ligi Kuu machozi, jasho na damu

Tue, 11 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Simba na Yanga zikiteremka uwanjani leo kusaka pointi tatu, zitalazimika kutumia hesabu dhidi ya wapinzani wao ili kupata matokeo mazuri.

Timu hizo zitaungana na nyingine kukamilisha idadi ya mechi tisa za Ligi Kuu Tanzania Bara zitakazochezwa leo Jumanne kwenye viwanja tofauti.

Mbali na Simba, Yanga lipo kundi kubwa la timu zinazosaka pointi tatu ili kujiweka katika mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu.

Hesabu ya pointi na presha inayozikabili ni mambo mawili ambayo yatazifanya mechi hizo kufuatiliwa kwa karibu na wadau soka nchini.

Homa ya mechi hizo ipo kwa timu zilizopo katika nafasi mbaya Singida United, Ndanda, Mbeya City, Mwadui, Mbao, KMC, Alliance na Mtibwa Sugar.

Mbeya City inayoshika nafasi ya tatu kutoka mkiani itakuwa katika presha kati ya zile za chini ya msimamo wa ligi itakapocheza na Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia Soma

Advertisement
Ushindi unaweza kuifanya isogee pengine hadi nafasi ya 16 lakini sare au kipigo, vinaweza kuishusha zaidi na ikajikuta inaangukia nafasi ya pili kutoka mkiani ambayo ni 19.

Ni tofauti na Yanga ambayo ushindi utatoa presha kwa Simba na Azam katika msimamo wa ligi na vita ya kuwania ubingwa na ikipoteza inaweza kuporomoka kutoka nafasi ya tatu.

Nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi alisema pamoja na kuiheshimu Mbeya City wana imani ya kuibuka na ushindi kutokana na ubora wa kikosi.

Kocha wa Mbeya City, Amri Said alisema wanakutana na timu ngumu ambayo wanatakiwa kucheza kwa umakini dakika zote za mchezo.

“Vijana wangu wamejiandaa vyema kwa mchezo hasa baada ya kufanyia kazi makosa yaliyotokea katika mchezo dhidi ya Prisons. Kama wachezaji watafuata kile tunachoelekeza naamini tutafanya vizuri,” alisema Amri.

Sven macho yote Mtibwa

Mkoani Morogoro, baada ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya JKT Tanzania, Simba itakuwa na nafasi ya kujiuliza itakapokutana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri.

Timu hizo zinakutana huku kila moja ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi iliyopita ambapo Mtibwa ilichapwa bao 1-0 na Lipuli.

Mtibwa inapigania kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja kwani licha ya kushika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi, imeizidi timu inayoshika mkia kwa pointi 12 tu sawa na mechi nne.

Kocha wa Simba, Sven Vanderbroeck alisema anatumia muda mrefu kuwajenga kisaikolojia wachezaji. “Nimezungumza kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwa vitendo uwanjani ili kuepuka kurudia makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita,” alisema Sven.

Azam, Yanga kazi ipo

Azam itakuwa nyumbani uwanja wa Uhuru kuikaribisha Polisi Tanzania ikisaka pointi tatu na kuzidi kuifukuzia Simba iliyopo kileleni wakati kwa Polisi ushindi utawafanya wawe na fursa nzuri ya kunyemelea nafasi nne za juu.

Kocha msaidizi wa Azam, Idd Cheche alisema mechi hiyo ni ngumu kwa kila upande kutokana na ubora wa Polisi.

Kocha wa Polisi Tanzania, Malale Hamsini alisema hawako tayari kupoteza mechi ya pili mfululizo baada ya kufungwa na Coastal Union huku akifichua kufanyia kazi tatizo la safu ya ushambuliaji ambalo limekuwa likiwagharimu.

Hata hivyo, Malale atawakosa Hassan Maulid, Baraka Majogoro ambao ni majeruhi, William Lucian na Pato Ngonyani wanatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

“Kweli tunasumbuliwa na majeruhi wengi hivi sasa lakini hilo sio tatizo kubwa kwasababu tuna kikosi kipana ambacho kina wachezaji wengi naamini waliopo watafanya vizuri pia,” alisema kocha huyo.

Mkoani Iringa, Lipuli watakuwa wenyeji wa JKT Tanzania ambao wametoka kuisimamisha Simba kwa kuichapa bao 1-0 katika mchezo uliopita huku wenyewe wakiwa wametoka kuiadhibu Mtibwa Sugar ugenini kwa ushindi kama huo.

Baada ya kupokea kichapo cha ugenini kutoka kwa Kagera Sugar, Biashara United itakuwa na kibarua nyumbani dhidi ya Mbao ambayo ilitoka sare ya bao 1-1 na Alliance juzi Jumamosi.

Vibonde Singida United watakuwa wakijaribu kufufuka upya watakapokuwa nyumbani kwenye uwanja wa Liti kuwakaribisha Namungo ya Ruangwa, mkoani Lindi.

Wakiwa wanashika mkia na pointi zao 11, ushindi dhidi ya Namungo ndio unaohitajika ili angalau waweze kupunguza presha vinginevyo watazidi kuwa katika hali mbaya.

Mechi nyingine za ligi leo ni zile za Mwadui itakayoikaribisha Ndanda kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Ruvu Shooting itavaana na Prisons. Ruvu itaingia uwanjani kusaka pointi tatu baada ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Yanga.

Mkoani Kagera wenyeji Kagera Sugar watakuwa uwanja wa nyumbani wa Kaitaba kucheza na majirani zao wanaotokea Mwanza Alliance.

Imeandikwa na Charles Abel, Thomas Ng’itu, Charity James na Juma Mtanda

Chanzo: mwananchi.co.tz