Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu kumalizika Julai 11

Ac33d9faec5fa2ea43d5ec20857bf2a1.jpeg Ligi Kuu kumalizika Julai 11

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kuchelewa kumalizika kwa ligi badala ya Juni 21 sasa itakwenda hadi Julai 11, mwaka huu.

Mabadiliko hayo yametokana na baadhi ya michezo kusogezwa mbele baada ya kutokea kwa kifo cha aiyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli ambapo serikali imetangaza siku 21 za maombolezo kuanzia Machi 17, mwaka huu.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Mtendaji wa TPLB, Almas Kasongo alisema wamekutana na changamoto hasa baada ya kutangazwa kwa siku 21 za maombolezo hivyo imewalazimu kusogeza baadhi ya michezo mbele na mingine imekufa na kupangiwa tarehe.

“Tumelazimika kupitia upya ratiba ili ianze baada ya kumalizika kwa maombolezo Aprili 7, mwaka huu. Kuna michezo imekufa imebidi itafutiwe tarehe nyingine, kuna michezo ya viporo na michezo ya kimataifa,” alisema.

Kasongo alisema kulikuwa na michezo ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA) ilitakiwa ichezwa Aprili 3 na 4 na sasa imekufa.

Pia, alisema michezo ya ligi ilitakiwa ichezwe Aprili 6 na 7 na sasa haitakuwepo imesogezwa mbele hadi Aprili 8, 9 na 10 mwaka huu, ambapo ndipo ligi itarejea rasmi baada ya kumalizika kwa maombolezo.

Michezo itakayochezwa Aprili 8, mwaka huu ni Mbeya City dhidi ya Kagera Sugar na Namungo dhidi ya Ihefu. Siku inayofuata Biashara United dhidi ya Polisi Tanzania, JKT Tanzania dhidi ya Mwadui na Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar.

Aprili 10, mwaka huu zitacheza Yanga dhidi ya KMC, Tanzania Prisons dhidi ya Dodoma Jiji na Gwambina dhidi ya Coastal Union.

Chanzo: www.habarileo.co.tz