Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu inakua na ushirikina wake

Simba Vs Yanga Chama Yulee.jpeg Ligi Kuu inakua na ushirikina wake

Mon, 6 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna shaka kila mpenzi wa soka anajivunia ukubwa na hata ubora wa Ligi Kuu Bara ambayo sasa inafuatiliwa sehemu nyingi za Bara la Afrika.

Si kwa sababu Azam Media wanaonyesha karibu mechi zote za ligi na kuonekana sehemu kubwa barani Afrika tu, bali kwa jinsi inavyozidi kuvutia nyota kutoka nchi tofauti.

Tena awali ilikuwa tunachukua wachezaji ambao huko kwao hawana thamani kubwa, wengine majina yao ni kichekesho kila yanapotamkwa kwa kuwa yanatukumbusha enzi za giza, lakini baadaye tukageukia wachezaji nyota lakini ambao wanakaribia kustaafu kuja kuongeza uzoefu wao kwenye ligi yetu.

Sasa angalau wale nyota wanaoanza kuchipukia wanakuja kwetu. Sio Banda, Si Pape Sakho, si Aziz Stephane Ki na vijana wengine, lakini kilicho dhahiri ni uwezo wa kupokonyana wachezaji walio na umri kuanzia miaka 21 au 22 dhidi ya klabu za huko nje umeanza kujengeka miongoni mwa klabu zetu.

Mambo yakiendelea hivi na klabu zikaendelea kujijenga kifedha, kiuongozi, kimuundo na kiufundi, hapo baadaye ligi yetu itakuwa moja ya ligi za mfano Afrika na macho ya wengi yataelekezwa Tanzania kama ilivyokuwa wakati fulani tulipokuwa tunafuatilia Ligi Kuu ya Afrika Kusini, achilia mbali hiyo Ligi Kuu ya England ambayo ni kama imeturoga.

Lakini kupanda kwa ligi yetu hadi kufikia nafasi ya tano kwa ubora Afrika hakuendani na baadhi ya mambo katika ngazi ya klabu.

Pengine jambo hilo ambalo ni tofauti na mpira wa kisasa na kisayansi zaidi, ndilo linazidi kukua katika enzi hizi za mwangaza.

Imani za kishirikina! Ndio aibu yetu kuu inayofanywa kwa ufahari. Ni kama vile tunajivunia kufanya vitendo vya ushirikina.

Timu inafanya vitendo vya kishirikina kama suala lililopitishwa kwenye vikao rasmi vya klabu.

Wachezaji wanafanya vitendo vya kishirikina kana kwamba wameelekezwa na walimu wao kuwa ndio njia pekee ya kufanikiwa na pale inapokuwa ni kugombea nafasi kwenye kikosi cha kwanza, hapo ndipo huonekana dhahiri imani za kishirikina zimejikita hadi kwa mchezaji mmoja mmoja.

Wapo wachezaji walionukuliwa wakisema wanafanyiana mambo mabaya kwenye timu, hadi mmoja kuamua kupotea. Wapo walionukuliwa wakisema wanakuwa katika utimamu mzuri wa mwili kabla ya mechi, lakini zinapokaribia huumwa magonjwa ambayo hayaeleweki. Hapo ni wewe kufanya majumuisho wanamaanisha nini.

Kuonyesha kukithiri kwa vitendo hivyo vinavyoaminika ni vya imani za kishirikina, hivi sasa wachezaji wanafanya waziwazi.

Katika moja ya mechi kubwa jijini Dar es salaam ya hivi karibuni, kiungo wa Azam FC, Feisal Salum na wa Yanga, Mudathir Yahya walitegeana kuingia uwanja hadi wenzao waliotangulia waliposhikana mikono ya kutakiana mchezo mwema ndipo walipojiunga na wenzao.

Ingawa wameadhibiwa kwa makosa ya kukataa kushikana mikono na wenzao, lakini kutokana na wawili hao kucheza nafasi moja, inawezekana kabisa wataalamu wao waliwaambia ‘wasishikane mikono kabla ya mechi’ sijui alikuwa mganga mmoja!

Kabla ya hapo, Cloutus Chama wa Simba na Stephane Aziz Ki nao walitegeana hivyo hivyo na baadaye kuadhibiwa na Bodi ya Ligi.

Wiki iliyopita mshambuliaji wa Singida Big Stars, Habib Kyombo aliadhibiwa na Bodi ya Ligi kwa kosa la kumwaga kitu kinachodhaniwa ni kimiminika kabla ya mechi dhidi ya Namungo.

Hayo ni matukio machache tu, lakini kila ukiangalia wakati wachezaji wanaingia uwanjani utaona jinsi wanavyoheshimu maelekezo ya waganga kuliko ya walimu. Mchezaji hasahau kuvuka mstari wa kuingia uwanjani kwa kutumia mguu mmoja au staili nyingine.

Wapo pia ambao hutumia vitendo vya imani za dini kabla ya kuingia uwanjani, kama vile kugusa chaki na kuweka alama ya msalaba au kusujudu.

Timu kukataa kutumia mlango rasmi na kupitia sehemu nyingine, ni mambo ya kawaida sana wanayokutana nayo wasimamizi wa mechi. Tuhuma za kuwekewa dawa za kulevya, huhalalisha timu kutotumia vyumba vya kubadilishia nguo kumbe ni imani za kishirikina.

Kuonyesha klabu zinabariki vitendo hivyo, viongozi hutuma watu wake kwa ajili ya kulinda vyumba watakavyotumia kubadilisha nguo. Watu hao, maarufu kwa jina la makomandoo, huenda kukesha kwenye vyumba hivyo kuzuia walozi wasifanye mambo yao.

Yuko mchezaji ambaye alikuwa katika orodha ya wachezaji waliotazamia kuanzia benchi, lakini akatumwa kuongoza watu kwenda kufanya ulozi saa nane mchana wakati mechi ilikuwa saa 10:00 jioni. Sijui ilikuwaje kocha akakubali mchezaji wake aende kuongoza walozi.

Kile kitendo cha kuwasha moto katikati ya uwanja, tena nje ya nchi, ndio kinakandamizia vitendo vyote vya imani za kishirikina kwa kuwa kilifanywa kifahari na kwa kujivuna katika zama hizi za sayansi na teknolojia.

Vyote hivyo vinafanya tujiulize, hivi kweli Ligi Kuu yetu inakua kwa ubora wake wote au kwa vigezo vichache sana.

Katika ligi inayokua na mambo yake yote, vitendo hivi vingekuwa vinapungua na sayansi kuonekana zaidi.

Haiwezekani ligi inayoshika nafasi ya tano kwa ubora Afrika ikajawa na vitendo vya imani za kishirikina badala ya sayansi na juhudi.

Vitendo hivi haviwajengi wachezaji wetu kimpira bali vinawafanya waone kwamba mafanikio hayatokani na juhudi pekee bali nguvu za ziada, hasa za giza.

Kwa hiyo, mchezaji wa aina hii anapoona anazidiwa na mwingine ndani ya timu au wa timu pinzani, anaamini kumzidi kwake kunatokana na nguvu za giza na si jitihada kubwa anazotia.

Ndio maana imekuwa si ajabu kwa wachezaji kutuhumiana kwa vitendo vya kishirikina.

Hata wachezaji, kama timu, wanapozidiwa na timu nyingine, wanaona kuwa hali hiyo imetokana na wenzao kutumia nguvu za giza.

Hawa ukiwaambia wawashe moto, wakatae kutumia mlango rasmi au kuingia vyumba vya kubadilishia nguo, hawatasita hata kidogo.

Hawa wanastahili kuwa kwenye ligi inayoshika nafasi ya tano kwa ubora Afrika? Au ndio kulinda utamaduni wetu?

Viongozi na walimu hawana budi kujiepusha au kukataa kabisa vishawishi vya kutumia nguvu za giza kufanikisha masuala ya kisayansi viwanjani.

Ni lazima tujenge timu zinazojua kuwa maarifa, ustadi, sayansi na jitihada ndio nguzo ya mafanikio na si vitu vya dhahania.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: