Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu inahitaji V.A.R au uamuzi bora?

Var Mkapaaa Ligi Kuu inahitaji V.A.R au uamuzi bora?

Mon, 18 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kati ya matukio ya kukumbukwa katika fainali zilizopita za soka za Mataifa ya Afrika (Afcon 2021) zilizofanyika Cameroon ni waamuzi wawili kutoka Gambia na Afrika Kusini kuchezesha mechi za hatua za mtoano kwa dakika 120 bila ya kuitwa kuangalia vizuri maamuzi waliyoyafanya.

Papa Gassama wa Gambia alikuwa mwamuzi wa kwanza kuchezesha mechi kwa dakika 120 bila ya Refa Msaidizi wa Video (V.A.R) kumuita aende kuangalia vizuri runinga ya pale uwanjani uamuzi alioufanya ili kama hakuona vizuri abatilishe uamuzi wake.

Gassama alichezesha mechi ya nusu fainali baina ya vigogo wa Afrika, Cameroon na Misri, ambayo ilimkosoa kuwa hakuwa na utimamu wa kumudu mechi za michuano hiyo.

Lakini Gassama aliyapa kisogo maneno yao na kuichezesha mechi hiyo kwa utulivu, akifanya maamuzi kwa makini, ikiwemo kumtoa kutoka benchi, Kocha wa Misri, Carlos Quiros baada ya kubishana naye mara mbili na hivyo kustahili kadi mbili za njano.

Refa huyo wa Gambia amejizolea sifa kutokana na uwezo wake wa kumudu mechi za mashindano ya Afrika na duniani. Alichezesha mechi ngumu ya hatua ya makundi baina ya Nigeria na Misri na ya 16 Bora kati ya Mali na Equatorial Guinea na hakuwa na dosari.

Mwingine aliyeonyesha ukomavu na weledi kwenye fainali hizo ni Victor Miguel de Freitas Gomez wa Afrika Kusini ambaye alichezesha mechi ngumu zaidi ya fainali baina ya Senegal, ambao waliibuka mabingwa, na Misri waliokuwa wakitetea ubingwa.

Gomez naye alichezesha dakika zote 90 na 30 za nyongeza bila ya kuitwa na V.A.R kwenda kuangalia vizuri uamuzi wowote alioufanya kwenye mechi hiyo. Alitoa penalti kwa Senegal mapema katika mchezo huo iliyopotezwa na Sadio Mane na baadaye kuwaonyesha kadi za njano nyota wa timu hizo mbili, Sadio Mane na Mohamed Salah, huku akimuuliza nyota huyo wa Liverpool “unataka nikuachie filimbi uchezeshe?”

Wawili hao walionyesha kiwango cha juu cha umakini, uzoefu na uwezo katika kipindi ambacho Afrika ilitambulisha matumizi ya teknolojia ya mwamuzi wa video katika fainali zake kuhakikisha kunakuwepo na usahihi wa maamuzi unaoweza kutoa mshindi anayestahili.

Lakini hoja moja ambayo wawili hao waliiweka mezani ni kwamba unahitaji kwanza uwe na waamuzi makini, wenye weledi na uwezo wa kumudu kuchezesha mechi kabla ya kuanza kufikiria teknolojia kusaidia uamuzi.

Na kibaya zaidi ni kwamba hata ukiweka teknolojia, bado anayefanya uamuzi wa mwisho ni binadamu anayeitwa refa. Ndio maana leo hii Waingereza bado wanasumbuka na matumizi ya V.A.R pamoja na taifa hilo kuwa moja ya nchi zilizoendelea kiteknolojia.

Taarifa iliyotangazwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kuwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeahidi kuwapa mashine za V.A.R kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu zinaweza kuwa njema na nzuri sana, lakini zisizoakisi mazingira mazuri ya matumizi ya teknolojia hiyo kwa sasa.

Teknolojia si suluhisho la uamuzi mbovu katika soka iwapo huna watu wenye ujuzi, uwezo, uzoefu, weledi na umakini. V.A.R inaweza kugeuka kuwa chukizo kuliko hili la sasa lililopo.

Cha muhimu ni kwamba kuwa na waamuzi wanaoweza kumudu mechi bila ya matatizo kama Gassama na Gomez ili matatizo tata kama ya golini, penalti, kadi nyekundu na utambuzi wa mchezaji aliyefanya kosa yatatuliwe kwa msaada wa video. Hata nchi zilizoendelea kisoka na kiteknolojia bado zinasumbuka na V.A.R, vipi huku kwetu?

Ligi Kuu ya England bado inasumbuka na waamuzi wasaidizi wa video ambao wamekuwa wakishindwa kufanya mambo ya muhimu kama vile kuchora mistari ya kumuwezesha mwamuzi wa kati kuamua kwa usahihi matukio ya kuotea au kutomwita kabisa mwamuzi wa kati aende kwenye runinga iliyopo pembeni ya kuangalia upya uamuzi wake dhidi ya matukio.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Waamuzi wa Mechi za Michezo ya Kulipwa (Professional Game Match Officials Limited, PGMOL), Michael Webb amekuwa akilazimika mara kwa mara kutoa taarifa za kuomba radhi kwa makosa ya waamuzi wake yaliyozigharimu timu kama Arsenal, Liverpool, Newcastle na Manchester City au kutoa ufafanuzi wa baadhi ya maamuzi.

Arsenal, Newcastle, Manchester City na Liverpool ni baadhi ya timu zilizoathirika na makosa ya waamuzi wasaidizi wa video, kiasi kwamba vyombo vya habari vya England hivi sasa vinafanya mzaha wa kutengeneza msimamo wa ligi unaoonyesha hali ambavyo ingekuwa bila ya makosa ya V.A.R.

V.A.R ni kifupi cha Video Assistant Referee au kwa Kiswahili ni refa msaidizi anayetumia video. Pamoja na jina kumtambulisha mtu mmoja, ukweli ni kwamba kwenye chumba cha V.A.R huwa kuna watu watatu muhimu; refa msaidizi ambaye ndiye huwa kiongozi, wa pili ni msaidizi wake na wa tatu ni yule anayeendesha mashine kwa ajili ya kufuatilia vizuri matukio.

Matukio yanayofuatiliwa ni mabao na matukio ya ukiukwaji wa sheria yanayotokea kabla ya bao kufungwa, kadi nyekundu, penalti na utambuzi wa mtu aliyefanya kosa. Katika baadhi ya matukio, uamuzi uliofanywa na refa unaweza kubatilishwa lakini ni lazima liwe kosa la wazi kabisa.

Mchakato wa uamuzi unaweza kufanywa kwa namna mbili. Kwanza kwa timu ya V.A.R kumshauri refa wa kati aende kwenye runinga kuangalia vizuri tukio la uamuzi alioufanya na pili kwa refa mwenyewe kuomba aonyeshwe marudio ya tukio hilo ili awe na taarifa sahihi zinazomuwezesha kufanya uamuzi.

Na hilo likifanyika, refa wa kati huweza kufanya mambo matatu. Kwanza anaweza kubatilisha mara moja uamuzi wake kwa kuzingatia ushauri wa V.A.R; pili anaweza kushikilia uamuzi wake wa awali au tatu mwenyewe kwenda kwenye runinga iliyopo pembeni ya uwanja kuangalia vizuri tukio alilolifanyia uamuzi.

Kwa maana nyingine, pamoja na teknolojia kutumika, bado ni uamuzi wa binadamu ndio utaamua matumizi mazuri ya nyenzo hiyo. Kwamba mwamuzi wa V.A.R anaweza asimshauri vizuri mwamuzi wa kati kuhusu tukio fulani; mwamuzi wa video au wa kati anaweza kutoa tafsiri mbaya ya sheria kuhusu tukio, mwendesha mashine anaweza asichore vizuri au asichore kabisa mistari ya kuonyesha kuotea au mpira kutoka nje kabla ya bao kufungwa.

Na kwa waamuzi ambao wamechezesha soka kwa miaka miwili tu ni vigumu kwao kuweza kuwa na ufahamu mpana wa sheria na tafsiri yake kuhusu matukio na hivyo kusababisha V.A.R kuwa chukizo zaidi kama ambavyo inawasumbua kwa sasa nchini England.

Makosa mengine ya V.A.R nchini England yamekuwa ni uchovu wa waamuzi wa wasaidizi. Kutokana na uchache wa watu wenye ujuzi huo, ambao kwa kawaida ni waamuzi waliofuzu mafunzo, baadhi wamelazimika kusimamia mechi kwa siku mbili mfululizo na hivyo utimamu wao wa afya kutokuwa vizuri na hivyo kuathiri maamuzi yao.

PGMOL imetangaza nafasi za kazi kwa waamuzi ikiwashauri hata wasio na ujuzi wa teknolojia lakini wamemaliza mafunzo ya uamuzi, waombe na kwamba watapatiwa mafunzo baadaye.

Kwa hiyo, wakati tunafurahia ahadi ya msaada wa mashine za V.A.R ni muhimu kujihoji kama tuko tayari kwa tknolojia hiyo? Tunayo nguvu kazi ya kutosha yenye ufahamu wa teknolojia hiyo? Tuna watu wenye weledi wa kuaminiwa kutumia teknolojia hiyo?

CAF watatupa msaada wa kamera za ziada za kuweka angalau kwenye viwanja vitatu au vinne kwa raundi moja au watatupa vifaa vya kuweka kwenye chumba cha V.A.R na hizo kamera nyingine tutegemee kwa Azam Media ambao bado hawajakuwa na vifaa vya kutosha kuonyesha usahihi wa matukio?

Lipi lafaa lije kwanza; vifaa vya teknolojia ya V.A.R au mkakati madhubuti wa kunoa waamuzi wetu wawe na uwezo wa kumudu mechi bila ya makosa mengi kabla ya kuanza kutumia teknolojia hiyo?

La kuchekesha ni ile Kamati ya Usimamizi wa Ligi, nayo itakuwa na nafasi gani kwenye V.A.R ikiwa sasa imeshaanza kubatilisha maamuzi ya refa na kutoa kadi zake nyekundu halafu kuadhibu kwa kufungia wachezaji! Bado tuna safari ndefu katika uamuzi na usimamizi wa mchezo wetu.

Maendeleo hayaji kama mvua. Yanahitaji mikakati ya muda mrefu yakipimwa kila baada ya muda kuona kama tumefikia kiwango tulichojiwekea kwa kipindi fulani au tumeshindwa. Ndio, misaada ni muhimu. Lakini ni lazima iendane na mahitaji yetu ya sasa ambayo ni uamuzi bora na si teknolojia ya kisasa.

Huko bado hatujafika!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live