Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu England, ukizubaa inakula kwako

Manchester City.jpeg Ligi Kuu England, ukizubaa inakula kwako

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Liverpool imekomaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kukusanya pointi 63 katika mechi 27.

Manchester City ushindi wao kwenye Manchester derby umewafanya wazidi kuwapa presha Liverpool kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya kukusanya pointi 62 katika mechi 27.

Pointi moja tu, inazitenganisha timu hizo kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo baada ya mechi ya wiki ya 27 katika mikikimikiki ya ligi hiyo.

Arsenal ilikuwa na kibarua usiku wa jana Jumatatu kuona kama itaweza kukimbizana na wapinzani wake hao kwenye mbio hizo za ubingwa.

Kabla ya mchezo huo wa usiku wa jana dhidi ya Sheffield United, Arsenal ilikuwa imekusanya pointi 58 katika mechi 26.

Ushindi wa vijana wa Mikel Arteta utawaweka kwenye wakati mzuri na pengine unaweza kuongeza presha kwa Jurgen Klopp na Pep Guardiola wa Liverpool na Man City mtawalia kwenye mchakamchaka wa kusaka ubingwa.

Aston Villa imezidi kujiimarisha kwenye nafasi ya nne, jambo linaloonyesha kwamba kocha Unai Emery yupo siriazi katika kuitafutia timu hiyo nafasi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa kuhakikisha inamaliza ligi ndani ya Top Four.

Ushindi wa mabao 3-2 iliyoupata Aston Villa ugenini kwenye kipute dhidi ya Luton Town, umewafanya wakusanye pointi 55 baada ya mechi 27, pointi tano dhidi ya timu inayoshika nafasi ya tano, Tottenham Hotspur. Hata hivyo, Spurs imecheza mechi 26, hivyo endapo itashinda, itapunguza pengo hilo na kubaki pointi mbili kwenye mbio hizo za kusaka nafasi kwenye Top Four ili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Macho kwenye ubingwa

Baada ya Liverpool kushinda kwa bao la utata kwenye dakika za majeruhi dhidi ya Nottingham Forest presha ilibaki kwa wapinzani wake kwenye mbio za ubingwa, hasa Man City, ambao walikuwa na kibarua kigumu cha kuikabili Manchester United kwenye kipute cha Manchester derby uwanjani Etihad.

Darwin Nunez alifunga kwa kichwa katika dakika 99 kuhakikisha Liverpool inamaliza mzunguko wa wiki ya 27 ikiwa bado kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England, ikiweka pengo la pointi kufikia nne dhidi ya Man City ambao wao walikuwa bado hawajamalizana na Man United.

Guardiola alitambua kwamba Man City yake inakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya mahasimu wao, Man United na presha ilikuwa kubwa baada ya Marcus Rashford kufunga bao la utangulizi kwenye dakika ya nane tu. Hadi mapumziko, Man City ilikuwa nyuma kwa bao hilo.

Kipindi cha pili mambo yalibadilika, Phil Foden alifunga mara mbili na Erling Haaland mara moja, kuipa Man City ushindi wa mabao 3-1 na hivyo kuamsha matumaini ya kutetea ubingwa wa ligi hiyo, ambapo watakuwa wanausaka kwa msimu wa nne mfululizo. Shughuli sasa ilibaki kwa Arsenal kwenye vita hiyo ya kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Usiku wa jana, The Gunners ilikuwa huko Bramall Lane na kilichotokea, kimetokea.

Man United yarusha taulo Top Four

Man United ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, nafasi mbili tu nyuma ya Top Four, ambayo ndiyo hasa inayotoa tiketi ya mwisho ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kutumia ligi ya ndani. Lakini, kwa hali ilivyo, Man United ni kama imeamua yaishe kwenye msako huo wa nafasi ya kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Vipigo viwili mfululizo kwenye ligi hiyo, vimeifanya Man United sasa kuachwa pointi 11 na timu inayoshika nafasi ya nne, Aston Villa. Kinachotishia Man United ni kwamba hadi kwenye raundi ya wiki ya 27 kwenye Ligi Kuu England, tayari imeshapoteza mechi 11 baada ya kipigo kutoka kwa Man City.

Kwenye Top Four kwa sasa vita inaonekana imebaki kwa Aston Villa na Spurs, ambapo kwa sasa zimetofautiana pointi tano, huku vijana wa Ange Postecoglou wakiwa na mchezo mmoja mkononi, endapo watashinda basi watampa presha Emery kwa kubakiza pointi mbili tu. Spurs yenyewe iliichapa Crystal Palace mabao 3-1 katika mchezo wa wikiendi, wakati Aston Villa iliibabua Luton mabao 3-2.

Chelsea yarudi 10 la chini

Bila shaka kocha Mauricio Pochettino atahitaji sana mchezo wake mmoja wa mkononi ili kujiondoa kwenye orodha ya timu za 10 la chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu England. Sare ya mabao 2-2 dhidi ya Brentford, tena Chelsea ikisawazisha dakika za saba za mwisho, ziliifanya The Blues kukusanya pointi 36 katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 26.

Kikosi hicho chenye maskani yake Stamford Bridge kinashika nafasi ya 11 kwenye msimamo huo, pointi 16 juu ya timu inayoshika nafasi ya 18, Luton Town iliyopo kwenye hekaheka za kujinusuru kushuka daraja. Mahali ilipo Chelsea ni mbali kuifikia Aston Villa kwenye Top Four, kuliko Luton Town kwenye kushuka daraja. The Blues kufikia Aston Villa kuna tofauti ya pointi 19 na kufika kwa Luton kuna pointi 16.

Haaland hataki kuachia buti

Baada ya kuganda na mabao yake 17 kwa muda mrefu na kutishiwa na Ollie Watkins mwenye mabao 16. Lakini, Haaland alitikisa nyavu katika mchezo a Manchester derby na hivyo kufikisha mabao 18 katika mechi 22 alizocheza kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Watkins amecheza mechi 27.

Kwenye mchakamchaka huo wa kusaka Kiatu cha Dhahabu, Mohamed Salah wa Liverpool amekwama kwenye mabao 15 aliyofunga katika mechi 21 kutokana na kuwa majeruhi, huku Jarrod Bowen wa West Ham United akishtua wengi baada ya kufunga mabao 14 katika mechi 26. Bukayo Saka wa Arsenal amefunga mara 13 katika mechi 25, sawa na Son Heung-Min wa Spurs, aliyefunga mabao 13 katika mechi 13. Vita hiyo ni kali.

Vita ya kushuka daraja ni balaa

Sheffield United usiku wa jana ilikuwa na kazi moja tu ya kujaribu kuisukumia Burnley mkiani kabisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu England endapo kama watakuwa wameshinda au kutoka sare dhidi ya Arsenal. Sheffield kabla ya mchezo wa usiku wa jana ililingana pointi na Burnley, pointi 13 kila moja na kufanya vita ya kupambana kujinusuru kwenye kushuka daraja kuwa kali.

Luton Town presha yao si kubwa baada ya kukusanya pointi 20, pointi nne tu chini ya timu inayoshika nafasi ya 17, Nottingham Forest na pointi tano chini ya timu inayoshika nafasi ya 16, Everton. Kwa mechi ambazo zimebaki, vita ya kushuka daraja bado mbishi na huenda ikawahusu hadi Crystal Palace waliopo kwenye nafasi ya 14 na pointi zao 28 walizovuna kwenye mechi 27.

Chanzo: Mwanaspoti