Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu England ni mshikemshike ndege tunduni

City Vs Chelsea Today Ligi Kuu England ni mshikemshike ndege tunduni

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

MCHAKAMCHAKA chinja. Ndicho kinachokwenda kutokea kwenye Ligi Kuu England wikiendi hii, ambapo vita imezidi kuwa kali kwenye kilele cha mikikimikiki hiyo ya kibabe kabisa.

Liverpool bado inapiga miluzi kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 54 katika mechi 24.

Nyuma yao wapo Manchester City, ambao wamekusanya pointi 52, lakini wamecheza mechi moja pungufu, hivyo wakishinda kiporo chao, watawaondoa Liverpool kileleni kwa tofauti ya pointi moja.

Chini yao ipo Arsenal, ambayo pia imekusanya pointi 52 kama Man City, lakini wao wakicheza mechi 24, sawa na Liverpool kwenye mbio hizo za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu.

Wanaokamilisha Top Four ni Tottenham Hotspur iliyokusanya pointi 47 katika mechi 24, kisha wanakuja Aston Villa na pointi zao 46, wakati Manchester United wanaojitafuta, wapo kwenye nafasi ya sita na pointi 41 baada ya kushuka uwanjani mara 24. Mambo ni moto.

Kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya tatu, chochote kinaweza kutokea kwenye msimamo kutokana na timu hizo kutofautiana pointi mbili tu.

Hivyo, kuepuka kuachwa mbali, hakuna timu itakayokubali kupoteza mchezo wake, hilo likitokea basi imekula kwao.

Kwenye nafasi ya nne, kuna vita nyingine muhimu, ambapo Spurs imeizidi Aston Villa kwa pointi moja tu, ambao wapo kwenye nafasi ya tano. Spurs ikipoteza kisha Aston Villa ikashinda, basi msimamo utabadilika. Vita ni kali. Man United na wababe wenzao wengine wa Big Six, Chelsea bado wanajikongoja kutafuta namna ya kupenya na kupata nafasi kwenye Top Four ya mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England ili kukamatia tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Patachimbika.

Liverpool itakuwa ya kwanza kurusha kete, watakapokuwa huko Gtech Community kukipiga na Brentford kwenye mchezo unaotazamiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na ugumu wa timu hiyo inapokucheza na vigogo kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Miamba hiyo imekutana mara tano kwenye Ligi Kuu England, ambapo Liverpool imeshinda tatu na zote nyumbani Anfield, huku Brentford ikishinda moja, ambayo pia ni nyumbani na mchezo mmoja baina yake ulimalizika kwa sare.

Kwa maana hiyo mechi za Brentford na Liverpool kila mmoja anashinda kwakwe, ambapo mara ya mwisho Liverpool ilipoifuata Brentford kwao, ilikumbana na kichapo cha mabao 3-1, Januari 2, 2023.

Liverpool itahitaji pointi hizo tatu za ugenini ili kuendelea kubaki kileleni kwa sababu wapinzani wake kwenye mbio za kuwania nafasi kwenye kilele cha ligi hiyo, Arsenal na Man City zenyewe pia zitashuka uwanjani kupambana Jumamosi hii. Chama la Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta, lenyewe litakuwa ugenini huko Turf Moor kukipiga na Burnley inayonolewa na Vincent Kompany. Mechi hiyo itakutanisha wababe wawili kwenye mabenchi ya ufundi ambao waliwahi kuwapo huko Man City yenye maskani yake Etihad.

Kwenye upande wa takwimu, Burnley na Arsenal zimekutana mara 17 kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, ambapo katika mechi hizo, mara nne walitoka sare, huku The Gunners ikishinda 12, saba nyumbani na tano ugenini, huku Burnley yenyewe ikishinda moja tu, tena ugenini.

Hiyo ina maana, Arsenal itakwenda Turf Moor kwenye uwanja ambao haijawahi kupoteza mechi katika michezo 17 iliyopita kwenye Ligi Kuu England. Bila shaka, Arteta atakuwa na matumaini makubwa ya kuendeleza joto kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Man City wao kasheshe lao litakuwa Etihad kukabilisha na Chelsea, ambao sasa wanaonekana kujipata chini ya kocha wao Mauricio Pochettino baada ya kushinda mechi zao mbili zilizopita. Mtihani mkubwa kwa The Blues ni kwamba wanakutana na Man City, ambayo itahitaji kuendelea kukimbizana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Chelsea yenyewe pia itakwenda ugenini kwenye mchezo huo kujaribu kushinda ili kupata pointi za kuwasogeza nafasi za juu katika msako wao wa kusaka tiketi ya walau kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.

Namba zinaonyesha kwamba Man City na Chelsea zimekutana mara 53 kwenye Ligi Kuu England, huku mechi nane baina yao zilimalizika kwa sare.

Mechi tatu zilizopita, Man City imeshinda mbili na sare moja, huku rekodi ikionyesha Chelsea imeichapa Man City mara 27, huku mechi 14 ilifanya hivyo kwenye uwanja wake wa Stamford Bridge na mara 13 ugenini huko Etihad, huku Man City ikishinda mara 18 mara saba ugenini na 11 nyumbani. Kwa maana hiyo, Chelsea itakwenda Etihad kusaka ushindi wake wa 14 kwenye Ligi Kuu England, wakati Man City yenyewe itahitaji ushindi wa 12 dhidi ya The Blues katika uwanja huo. Mechi ya kibabe kwelikweli.

Spurs kwenye vita yao ya Top Four itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa London kukipiga na Wolves. Hii ni mechi nyingine yenye mvuto wa kutazama. Spurs inafahamu wazi haipaswi kupoteza mchezo huo, kwa sababu wapinzani wao Aston Villa kama watapata ushindi ugenini huko Craven Cottage basi watawaporomosha kwenye nafasi hiyo ya nne.

Spurs na Wolves zimekutana mara 19 kwenye Ligi Kuu England, ambapo kwenye mechi tatu zilimalizika kwa sare, huku Wolves ikishinda saba, tatu nyumbani na nne ugenini, wakati Spurs yenyewe imeshinda tisa, nne nyumbani na tano ugenini. Lakini, mechi mbili zilizopita, Spurs zote alichapwa na Wolves. Kwa maana hiyo, shughuli ni pevu.

Aston Villa ya Unai Emery wao kwenye msala wao wa kumenyana na Fulham, wamekutana na mara 31 kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England, ambapo kwenye mechi 11 zilimalizika kwa sare, huku Fulham imeshinda saba, sita nyumbani na moja tu ugenini, huku Aston Villa imeshinda 13, mara 10 nyumbani na tatu ugenini. Mechi mbili zilizopita, Aston Villa ilishinda zote, lakini ilikuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, hivyo itakwenda ugenini Craven Cottage, ambako mara ya mwisho walichapwa 3-0.

Newcastle United itakuwa nyumbani St. James’ Park kukipiga na Bournemouth katika mchezo mwingine utaotazamiwa kuwa na upinzani mkali katika mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England. Namba zinasoma miamba hiyo, Newcastle na Bournemouth imekutana mara 11 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi nne zilimalizika kwa sare, huku nne nyingine ikishinda Newcastle na Bournemouth imeshinda tatu. Mechi nne za Spurs, mbili ilishinda nyumbani na mbili nyingine ugenini, huku Bournemouth wao, moja walishinda nyumbani na mbili ugenini.

Nottingham Forest shughuli yao itakuwa huko The City Ground kwenye uwanja wao wa nyumbani kukipiga na West Ham United ya kocha David Moyes.

Rekodi zinaonyesha kwamba Forest na West Ham zimekutana mara 11 kwenye Ligi Kuu England, ambapo The Hammers imeshinda sita, tano nyumbani na moja ugenini, huku Forest wao imeshinda mbili, moja nyumbani na nyingine ugenini, huku kwenye mechi tatu miamba hiyo ilitoka sare.

Mchakamchaka huo utaendelea Jumapili kwa mechi mbili tu, ambapo Sheffield United itakuwa nyumbani kucheza na Brighton, huku Luton Town itakuwa mwenyeji wa Manchester United.

Kwenye Uwanja wa Bramall Lane, wenyeji Sheffield United itakutana na Brighton kwa mara ya sita kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England na katika mechi hizo, Brighton haijawahi kushinda hata moja, huku mechi tatu zikimalizika kwa sare. Mechi ambazo Sheffield ilishinda, moja ilikuwa nyumbani na nyingine ugenini.

Man United wao kasheshe lao la ugenini huko Kenilworth Road, watakwenda kumenyana na Luton kwa mara ya pili kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, ambapo mara ambayo timu hizo zilikutana, Man United iliibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani Old Trafford. Je, Luton italipa kisasi? Ngoja tuone.

Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja tu, huko Goodison Park, ambapo wenyeji Everton watawakaribisha Crystal Palace. Miamba hiyo imekutana mara 29 kwenye Ligi Kuu England, ambapo tisa zilimalizika kwa sare, huku Everton ikishinda mara 14, saba nyumbani na saba ugenini, huku Palace yenyewe ilishinda sita tu, mbili nyumbani na nne ugenini. Safari hii itakuwaje?

Chanzo: Mwanaspoti