Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu Bara imewapa heshima

Mayele X Inonga Ligi Kuu Bara imewapa heshima

Thu, 23 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ili kuthibitisha Ligi Kuu Bara imekuwa bora na ya kuvutia ni namna wageni wanavyokuja kwa wingi kucheza soka nchini, pia inawasaidia makocha na wachezaji kupata viwango bora vya kuzitumikia timu zao za taifa.

Mfano mzuri ni wa Mwinyi Zahera wakati akiifundisha Yanga na aliitwa kuifundisha timu ya taifa lake la DR Congo, baada ya kuona anafanya vizuri na Wanajangwani na kwenda kusaidiana na kocha mkuu aliyekuwepo wakati huo.

Hata hivyo, ligi hiyo imekuwa ikitoa nyota wa kigeni wanaoenda kuzitumikia timu zao za taifa na idadi imekuwa ikiongezeka kila msimu.

Msimu huu pia baadhi ya timu zimetoa wachezaji wa kigeni wanaoungana na timu zao za taifa kujiandaa na michuano ya kufuzu Afcon 2023, na hii ni kutokana na viwango bora walivyoonyesha kwenye Ligi Kuu bara na michuano ya kimataifa.

CLATOUS CHAMA (ZAMBIA)

Kiungo mtengeneza mabao Simba, Clatous Chama atakwenda kulitumikia taifa lake la Zambia baada ya kufunga mabao matatu na ni kinara wa asisti 14 kwenye Ligi Kuu Bara pia ana mchango mkubwa kwenye michuano ya CAF na ndiye mwenye hat-trick hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiifunga dhidi ya Horoya walipopata ushindi wa mabao 7-0 na jumla kuwa na mabao manne kwenye hatua hiyo.

PETER BANDA (MALAWI)

Winga wa Simba, Peter Banda ameitwa kuitumikia timu yake ya taifa ya Malawi, ingawa kwenye Ligi Kuu msimu huu hajaanza na kasi kwani hadi sasa anamiliki bao moja tu akiwa amekaa nje muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

PAPE SAKHO (SENEGAL)

Baada ya winga Pape Sakho kuifungia Simba mabao saba kwenye ligi msimu huu ana kiwango cha juu, ameitwa kulitumikia taifa lake la Senegal ambalo lina wachezaji wengi wanaocheza nchi mbalimbali, akiwemo Sadio Mane anaichezea Bayern Munich huyu ndiye mchezaji pekee kutoka Afrika ambaye ameitwa kutoka Afrika.

HENOCK INONGA (DR CONGO)

Beki wa kati wa Simba ambaye ni panga pangua kwenye kikosi cha kwanza licha ya kufanya vizuri eneo lake la ulinzi ameifungia timu yake mabao mawili msimu huu dhidi ya Kagera Sugar na KMC, kutokana na kiwango chake bora ameitwa timu ya taifa ya DR Congo ambayo ina kundi kubwa la wachezaji kutoka Ulaya.

MEDDIE KAGERE (RWANDA)

Straika wa Singida Big Stars (SBS), Meddie Kagere hadi sasa amefunga mabao saba kwenye Ligi Kuu ni kawaida kwake kuitwa timu yake ya taifa la Rwanda, hata wakati yupo Simba ilikuwa hivyo.

EMMANUEL MVUYEKURE (BURUNDI)

Mchezaji wa KMC, Emmanuel Mvuyekure anamiliki bao moja kwenye ligi na taifa lake la Burundi limehitaji huduma yake kwenye michuano ya kufuzu AFCON mwakani.

FISTON MAYELE (DR CONGO)

Tangu straika wa Yanga, Fiston Mayele aanze kucheza Ligi Kuu amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu uliopita aliibuka mfungaji namba mbili wa mabao 16 nyuma ya George Mpole aliyemaliza na 17 na sasa anaongoza kwa mabao 15, ameitwa kulitumikia taifa lake la DR Congo ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipoanza kucheza soka hapa nchini.

Mchango wa Mayele siyo kwenye ligi ya ndani bali amekuwa nguzo muhimu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika akiwa amefunga mabao matatu.

KENNETH MAGUNA (KENYA)

Mchezaji wa Azam FC, Kenneth Maguna ameifungia Azam FC mabao matatu kwenye ligi na sasa ameitwa kulitumikia taifa lake la Kenya kwenye michuano ya kufuzu Afcon.

STIVE NZIGAMASABO (BURUNDI)

Mchezaji wa KMC, Stive Nzigamasabo hadi sasa ana mabao matatu kwenye ligi, ameitwa kuungana na timu yake ya taifa ya Burundi kwenda kucheza michuano hiyo ambayo itaanza Ijumaa ijayo.

JUSTIN NDIKUMANA (BURUNDI)

Coastal Union imemsajili kipa Justin Ndikumana dirisha dogo na amekuwa akitumika zaidi kwenye kikosi cha kwanza ni kati ya wachezaji walioitwa kuitumikia timu yake ya taifa ya Burundi.

Ndikumana anasema; “Kabla ya kuja Tanzania nimekuwa nikiitumikia timu yangu ya taifa huu ni muendelezo wa kile ninachokifanya siku za nyuma.”

KWA HAPA NYUMBANI

Aishi Manula, Beno Kakolanya (Simba), Metacha Mnata, Kibwana Shomari (Yanga), Datius Peter (Kagera Sugar), Yahya Mbegu (lhefu FC), David Luhende (Kagera Sugar), Dickson Job, Bakari Mwamnyeto (Yanga), Abdallah Mfuko (Kagera), Ibrahim Baka, Mudathir Yahya (Yanga).

Wengine ni Sospeter Bajana (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba), Yusuph Kagoma (SBS), Ramadhani Makame (Bodrumspor, Uturuki), Abdul Suleiman (Azam ), Edmund John (Geita Gold ), Feisal Salum (Yanga), Khalid Habibu (KMKM), Anuary Jabir (Kagera), Simon Msuva (Al-Qadsiah – Saudi Arabia), Mbwana Samata (KRC Genk).

Wapo pia Novatus Dismas (Zulte Ware gem,Ubelgiji), Alphonce Mabula (FK Spartak Subotica ,Serbia), Kelvin John (KRC Genk), Ben Markle (Basford United, Uingereza), Haji Mnoga (Aldershot Town, Uingereza), Ally Msengi (Swallows, Afrika Kusini), Himid Mao (Ghazl El Mahalla SC Misri) na Said khamis (Al-Fujairah, UAE).

Chanzo: Mwanaspoti