Msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2023/2024 umeanza kuchanganya na timu zote 16 tayari zimecheza mechi.
Yanga ndio watetezi wa taji hilo ikiwa imelichukua kwa msimu miwili mfululizo lakini pia kwa msimu huu kuna timu mpya tatu ambazo zimepanda.
Baada ya Ruvu Shooting, Polisi Tanzania na Mbeya City kushuka daraja msimu uliopita, nafasi zao zimechukuliwa na JKT Tanzania, Mashujaa na Kitayosce (Tabora United).
Timu 10, kati ya 16 kila moja imecheza mechi mbili huku sita pekee za Yanga, Azam FC, Tanzania Prisons, Singida Fountain Gate, Kitayosce na JKT Tanzania zimecheza mchezo mmoja kila moja.
Hadi sasa Simba ipo kileleni na alama sita baada ya kushinda mechi zake mbili dhidi ya Mtibwa na Dodoma Jiji lakini mkiani ipo Kitayosce iliyocheza mechi moja dhidi ya Azam na kuchapwa mabao 4-0.
Kupitia makala haya, hizi hapa ni baadhi ya namba za Ligi Kuu msimu huu katika maeneo tofauti.
MECHI 13 MABAO 29
Simba ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye ligi hadi sasa kiwa na sita, lakini kupitia mechi mbili, huku ikifuatiwa na Yanga iliyofunga matano katika mechi moja kama iliyocheza Azam, lakini yenyewe ina manne.
KMC baada ya juzi kuchapwa 5-0, na Yanga ikiwa ndio kipigo kikubwa zaidi kutokea kwenye ligi msimu huu, imekuwa timu iliyofungwa mabao mengi zaidi (6) hadi sasa kwani mechi ya kwanza dhidi ya Namungo iliisha kwa sare ya 1-1.
Rekodi zinaonyesha kuwa, katika mechi 13 zilizochezwa hadi sasa jumla ya mabao yaliyofungwa ni 29, huku wageni 11 wakifunga mabao 12 na wazawa 14 wakichangia jumla ya mabao 17, kinara akiwa ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam mwenye mabao matatu likiwamo bao la mapema zaidi hadi sasa la dakika tatu, kisha Matteo Antony wa Mtibwa Sugar na Jean Baleke wa Simba wakifuata wakiwa na mabao mawili kila mmoja.
Fei Toto ndiye mchezaji pekee aliyefunga hat trick hadi sasa ikiwa ni hat trick ya mapema zaidi katika Ligi Kuu kwa misimu ya karibu akifunga ndani ya dakika 10 tu akiipiku ile ya Saido Ntibazonkiza aliyofunga msimu uliopita akitumia dakika 11.
Pia, ni hat trick ya kwanza ya ligi kufungwa katika mechi za raundi ya kwanza kwa misimu ya hivi karibuni Kumbuka Kitayosce ilikuwa na wachezaji wanane tu na mechi ikavunjika dakika ya 15 tangu kuanza kutokana na wachezaji wawili wa timu hiyo ‘kujivunja’.
SAFU BUTU
Wakati Simba, Yanga na Azam zikionekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji kwa kufunga mabao mengi, timu nne za Tanzania Prisons, Singida, Kagera Sugar na Kitayosce ndizo zenye safu butu ya ushambuliaji kwani hadi sasa hazijapata bao kwenye ligi hadi sasa yakiwa yamefungwa jumla ya mabao 29.
SIDIBE, SIMBA HATARI
Ni mchezaji mmoja tu aliyeasisti mara mara mbili ambaye ni beki mpya wa Azam, Cheikh Sidibe aliyefanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Kitayosce, huku akifuatiwa na utitiri wa wachezaji wenye asisti moja moja akiwamo Maxi Nzengeli wa Yanga ambao ameanza kuwa gumzo katika ligi.
Lakini kama hujui ni Simba pekee ndio timu iliyoshinda mechi zake mbili kwa asilimia zote kwa zile zilizocheza raundi mbilimbili, kwani Mashujaa na Geita Gold kila moja imeshinda moja na kutoka sare moja, huku Ihefu imeshinda moja na kupoteza moja sawa na Dodoma Jiji huku, timu nyingine zikizocheza mechi mbili kwa kupoteza moja na kutoka sare moja kama KMC, Namungo, Coastal Union na Mtibwa Sugar.
KADI
Hadi sasa zimetolewa kadi za njano 35 kwa wachezaji tofauti wa ligi, lakini Justine Bilal wa Dodoma Jiji ndiye anaongoza kwa kuonyeshwa kadi mbili katika mechi zake mbili alizocheza huku wengine wengi wakiwa na kadi moja.
Dodoma Jiji inaongoza kwa kadi za njano ikiwa nazo saba ikifuatiwa na Geita na Ihefu zenye nne kila moja huku Yanga, Azam, Kitayosce na Singida Big Stars zikiwa timu zenye nidhamu hadi sasa kwani hazijapata kadi hata moja.
Kitu kizuri ni kwamba hadi sasa hakuna kadi nyekundu kwenye mechi hizo 13, wala bao la kujifunga na kuna penalti moja tu iliyofungwa na Namungo ilipotoka sare na KMC kupitia Fabrice Ngoy wa Ngoy.
CLEAN SHEETS
Kipa wa Geita Gold, Eric Johora na Lameck Kanonga wa Mashujaa ndio wanaongoza kwa ‘Clean Sheets’ kila mmoja akiwa nazo mbili hadi sasa na kuzifanya timu zao ziwe vinara wa Clean Sheet kwa ujumla.
Timu saba kati ya 16 ligi ndizo hadi sasa hazijaruhusu bao ambazo ni Azam, Yanga, Prisons, Singida, Mashujaa, Geita na JKT.
WASIKIE WENYEWE
Kocha wa Simba ambaye timu yake inaongoza ligi, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema msimu huu lengo lao ni kutwaa ubingwa licha ya ushindani uliopo.
“Tumeanza ligi vizuri. Tunatakiwa kuwa na mwendelezo wa kupata ushindi ili kutimiza lengo letu kwa msimu huu ambalo ni kutwaa ubingwa,” alisrma Robertinho.
Kocha wa Kitayosce inayoburuza mkia, Goran Kopunovic alijiondoa kwenye mbio za ubingwa na kuweka wazi mipango yao.
“Kwa msimu huu hatuwazi ubingwa. Timu bado ni mpya kwenye ligi na baadhi ya maandalizi ya msimu hayakukamilika kwa wakati. Lakini hilo halitupi sababu ya kushindwa kufanya vizuri na tumejipanga kupambana na kumaliza ligi tukiwa katika nafasi nzuri,” alisema Goran aliyewahi kuinoa Simba.
Nahodha wa Geita, Elias Maguli ambaye ndiye mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga bao wakati timu yake ikiizamisha Ihefu jijini Mbeya, alisema lengo lao msimu huu ni kumaliza katika nafasi nne za juu.
“Timu iko vizuri, licha ya ushindani uliopo kwenye ligi naamini tunaweza kupambana na kufanya vizuri, lengo letu msimu huu ni kumaliza katika nafasi nne za juu,” alisema Maguli.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Saidi alisema baada ya kupoteza Ngao ya Jamii iliyokwenda kwa mtaani wao, Simba, sasa nguvu nyingi klabi hiyo imezielekeza kwenye ligi na michuano ya kimataifa.
“Tulipoteza ngao, na mpira ndivyo ulivyo lakini sasa tunajipanga kuhakikisha tunatetea ubingwa wa ligi. Tumeandaa timu vizuri na tumejipanga kufanya hivyo,” alisema Hersi.