Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu Bara 2021/22 ilikuwa bab'kubwa

Bab Kubwa Yanga.jpeg Bingwa wa Ligi kuu Tanzania Bara, Young Africans

Sun, 3 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ushindani kwa klabu zilizoshiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu uliomalizika wa 2021/22 ulikuwa mkubwa na uthibitisho wa ubora wa ligi yenyewe, japo wapo waliopotoka na kudai ni ligi dhaifu.

Ligi yetu imekuwa bora na ubora wake umekuwa ukiongezeka siku hadi siku na kuifanya iwe ligi ya ushindani zaidi, yenye mvuto na msisimko.

Baadhi ya mataifa jirani, hasa ya ukanda wa maziwa makuu, yanaionea gele ligi yetu na kutamani siku moja katika nchi zao wawe na ligi yenye kufanana walau kwa kiasi fulani na ligi ya Tanzania Bara.

Hapo tulipofikia, kwa ubora wa ligi yetu, tunapaswa kujipongeza, tuwapongeze TFF kwa mwongozo na utawala bora, TPLB kwa usimamizi na uendeshaji mzuri kabisa wa ligi, kuliko kuponda kwa kuwa tu unajisikia kufanya hivyo.

Kwa kiasi fulani, hata malalamiko yaliyokuwepo kipindi cha nyuma, sasa yameanza kuwa historia, mambo yamebadilika, mafanikio yamekuwa makubwa, changamoto zinakufa zenyewe tena kwa kasi, zinakufa kifo cha mende, miguu juu!

Lawama kwa waamuzi kushindwa kuzitafsiri vizuri sheria imepungua sana, maana waamuzi wengi wamekuwa makini, wanazisimamia kikamilifu sheria 17 za soka, ratiba kubadilikabadilika haipo tena, viporo kwa baadhi ya timu imefutika.

Ligi yetu imekuwa ya viwango, ligi inayozilazimisha timu kufanya maandalizi ya kutosha ya kiufundi, kuwa na benchi zuri la ufundi, wachezaji wa viwango na viongozi bora wenye kuufahamu vizuri mpira wa miguu na matakwa yake.

Ubabaishaji na wababaishaji katika ngazi zote za mpira wa miguu nchini, utaondoka, wataondoka wenyewe, maana tulipo sasa na tunakoelekea, ni kuwa na ligi yenye uwazi, ukweli, inayoendeshwa kitaalamu kwa kuzingatia kanuni na sheria, ligi ya haki na usawa.

Inawezekana ninaposema kwamba Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara imekuwa bora, wapo wasionielewa, hawanielewi kwa sababu hawaelewi, au wanaelewa ila tu kwa sababu zao hawaelewi kwakuwa hawataki tu kuelewa, wapendwa, tumekuwa na ligi bora sana msimu wa 2021/22, tukubali, maana huo ndio ukweli.

Vipo vigezo ambavyo vinathibitisha kwamba, ligi yetu sasa ni bora, mosi, udhamini wa mabilioni ya fedha unaorahisisha shughuli za uendeshaji ndani ya TFF, TPLB, na klabu shiriki.

TFF na TPLB wanao uwezo sasa wa kuajiri wataamu , wasimamizi na waendeshaji wa ligi na mambo mengine ya kiutawala kwa weledi, na wanawalipa vizuri, kwa sababu fedha ipo.

Kampuni binafsi, na taasisi za Serikali zinapokubali kudhamini jambo fulani, lazima ziwe zimejiridhisha ya kwamba, fedha wanazozitoa zinakwenda kwenye mikono salama, kwenye jambo zuri na bora, pia kutokana na ubora huo, wao pia wafaidike.

Kwa udhamini uliopo, klabu zinapata uwezo wa kuajiri benchi zuri la ufundi, viongozi wataalamu, wachezaji wenye viwango na bora, hivyo kuongeza ushindani kwenye ligi kwa ubora wa kila klabu.

Ligi Kuu ya NBC ina wadhamini watatu, Benki ya NBC ambao ni wadhamini wakuu, Azam media, wadhamini wa matangazo ya televisheni na TBC Taifa ambao wanadhamini matangazo ya radio, udhamini huo, unaonesha ubora wa ligi yenyewe.

Ushindani unapokuwa mkubwa, ligi inakuwa bora, yenye mvuto, msisimko na kufuatiliwa na watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi.

Lakini pia, ligi inapokuwa bora, wachezaji, walimu na viongozi wa mpira kutoka mataifa ya nje hutamani kuingia, jambo ambalo kwa ligi yetu halina ubishi, tunao wachezaji lukuki kutoka mataifa ya nje, walimu kibao, na hata baadhi ya wataalamu, viongozi na watendaji wakuu, baadhi ya klabu zimewaajiri kutoka nje ya nchi.

Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ni bora, angalia hata zawadi zinazotolewa kwa washindi, ni kubwa, ambazo mataifa mengine jirani hawajaweza kuzifikia, huo pia ni ubora wa ligi.

Yapo mengi yanathibitisha ubora wa ligi yetu, ikiwemo ushindani wa timu katika ligi, msimu uliomalizika, hata timu zilizoshuka, Mbeya Kwanza na Biashara United zilikuwa bora, ndio maana mchezo wa mwisho wa kuhitimisha ligi ndio ulioamua nani anashuka daraja tena kwa achano dogo sana la alama tofauti na kipindi cha nyuma, timu zilizoshuka zilifahamika mapema.

Ushindani na ubora, uliochagiza ubora wa ligi yetu, ulikuwa pia kwa mfungaji bora na hata makipa waliweza kucheza michezo kadhaa bila kufungwa goli lolote (clean sheets).

Nani aliamini kwamba George Mpole wa Geita Gold, ataibuka mfungaji bora, kwa tofauti ya goli moja dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Fiston Mayele wa Yanga SC, ilifika wakati ushabiki ukahamia kwa mfungaji bora, hadi mechi ya mwisho, Mpole akafanikiwa kufunga goli lililompa ushindi dhidi ya Mayele, mzee wa kutetema!

Mbali na Mpole aliyeongoza kwa kufunga mabao mengi, mabao 17, Mayele 16, wengine waliofuatia, timu zao na idadi ya mabao kwenye mabano ni Reliants Lusajo (Namungo, 10), Idrisa Mbombo (Azam, 9), Rodgers Kola (Azam, 9), na Mateo Anton (KMC, 9), mazoea ya wachezaji wa timu kongwe kuibuka wafungaji bora, hilo msimu wa 2021, likawekwa kando, huo ni ubora wa ligi.

Makipa nao walinyukana vikali, walionyesha ubora na viwango vya juu, walijitahidi kuhakikisha hawafungiki kirahisi, kiasi cha kucheza mechi kadhaa bila kufungwa mechi yoyote (clean sheets).

Baadhi ya makipa waliofanya vizuri zaidi, timu na clean sheets zao kwenye mabano ni kinara Diarra (Yanga, 15), Mshery (Yanga, 12), Manula (Simba, 11), Kipao (Kagera Sugar, 9), Kadedi (8), Mnata (Polisi Tanzania, 8), Ssetuba (Biashara United, 8) na Mbisa (7)

Hakuna jambo ambalo linafanyika kwa mafanikio tu bila changamoto, pamoja na ligi yetu kuwa bora, changamoto hazikosekani, kikubwa ni wahusika kushughulikia changamoto hizo ili kuziondoa na kuifanya ligi yetu iendelee kuwa bora zaidi.

Kama kuna watu bado wanadai ligi yetu ni dhaifu, hao nadhani ni dhaifu zaidi ya udhaifu wanaouzungumza, tuwasamehe, na tuwasaidie watambue ubora wa ligi yetu.

Ligi yetu imehitimika Juni 29, 2022 kwa klabu ya Yanga kuibuka bingwa kwa kukusanya jumla ya alama 74, Simba alama 61, Azam alama 49 na Geita Gold alama 46.

Mpapaso unaipongeza sana klabu ya Yanga, na kuiombea ijipange na kujiandaa vema kwa ajili ya mashindano ya kimataifa, ikaliwakilishe taifa kwa mafanikio.

Klabu zilizoshuka daraja ni Mbeya Kwanza alama 25 na Biashara United pointi 28, zitakazocheza play off ni Mtibwa Sugar iliyomaliza pointi 31 na Tanzania Prisons alama 29.

Chanzo: Mwanaspoti