Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Daraja la Kwanza ni safari ya machozi, jasho na damu

71506 Ligi+picha

Thu, 15 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiu ya kupanda daraja, utani wa jadi kutokana na sababu za kijiografia, upinzani wa asili na maandalizi yanayoendelea kufanywa na klabu mbalimbali vinaifanya Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao kuwa ngumu kutabirika.

Tofauti na msimu uliopita ambapo kila kundi lilikuwa na timu chache ambazo zilionekana mapema zitafanya vizuri kama iivyokuwa kwa Namungo ya Ruangwa, Lindi ambayo ilipanda Ligi Kuu, hali huenda ikawa tofauti safari hii kutokana na namna makundi ya ligi hiyo yalivyo.

Wakati kila kundi likiwa na timu 12, zipo zaidi ya tano katika kila kundi ambazo zinafanya maandalizi makubwa kipindi hiki, hali inayotoa ishara huenda timu zitakazopanda Ligi Kuu msimu ujao zikajulikana katika raundi za lala salama za Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Ikiwa utaratibu uliotumika msimu uliopita kuamua timu za kupanda Ligi Kuu ukatumika msimu huu, ni wazi ushindani wa FDL utaanzia katika mechi za mwanzoni tofauti na ilivyozoeleka.

Ushindani huo utaletwa na kiu ya kila timu kukusanya pointi mapema ili ijihakikishie uongozi wa kundi na kufuzu moja kwa moja Ligi Kuu badala ya kusubiri kucheza mechi za mchujo 'Play Off'.

Kingine kitakachonogesha ligi ni utani wa jadi baina ya kundi kubwa la timu kutokana na ukaribu wao kijiografia na upinzani wa kiasili iliopo kwa baadhi ya timu.

Pia Soma

Vita kubwa itakuwepo katika Kundi B itakayohusisha timu za Pamba, Gwambina FC, Stand United, Geita Gold na Gipco ambazo zinatoka mikoa ya jirani.

Pamba na Gwambina kupangwa kundi moja, tayari kuna msisimko wa kundi hilo kwani zote zinatoka mkoa wa Mwanza kama ilivyo kwa Geita Gold na Gipco zinazotoka Geita jambo linalochochea upinzani baina yao.

Kiasili Mwanza na Geita imekuwa na upinzani kisoka, hivyo kitendo cha timu zao kupangwa pamoja, kitaongeza msisimko na ushindani kwenye kundi hilo.

Uwepo wa Stand United ya mkoani Shinyanga, unaongeza idadi ya mechi zitakazokuwa na msisimko kwani itafufua uhasama kisoka uliopo baina ya mkoa huo na Mwanza. Stand United ilipopanda daraja ilizitumia Pamba na Toto Africans kama ngazi ya kwenda Ligi Kuu.

Lakini uwepo wa timu nne ambazo zimekuwa chini ya umiliki na sapoti ya vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama, unaongeza upinzani baina ya zenyewe kwa zenyewe lakini pia ushindani baina yao na zile za kiraia.

Timu hizo ni Mashujaa, Rhino Rangers, Transit Camp na Green Warriors.

Kundi A kutakuwa na vita ya mkoa wa Mbeya ambayo itahusisha timu tatu za jiji hilo ambazo zote zimepangwa pamoja kwenye kundi hilo.

Timu hizo ni Mbeya Kwanza, Boma na Ihefu. Pia kuna vita baina ya timu nne za Dar es Salaam African Lyon, Friends Rangers, Reha FC na Ashanti United.

Lyon na Rangers ni wapinzani wa asili ambao ulikolezwa msimu wa 2017/2018 baada ya Lyon kuipokonya tonge mdomoni Friends katika dakika za jioni na kupanda Ligi Kuu.

Lakini presha kwenye kundi hilo inaongezwa na uwepo wa Dodoma FC ambayo ni moja ya timu zinazofanya maandalizi kabambe baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu miwili mfululizo.

Ligi hiyo itashirikisha jumla ya timu 24 ambazo zimepangwa katika makundi mawili tofauti.

Kundi A lina timu za Ashanti, Friends Rangers, African Lyon na Reha FC (Dar es Salaam), Majimaji na Mlale FC (Ruvuma), Mbeya Kwanza, Boma FC na Ihefu (Mbeya), Njombe Mji (Njombe), Dodoma FC (Dodoma) na Mufindi United (Iringa).

Kundi B zipo Transit Camp na Green Warriors (Dar es Salaam), Geita na Gipco (Geita), Gwambina na Pamba (Mwanza), Rhino Rangers (Tabora), Mashujaa (Kigoma), Sahare All Stars (Tanga), Stand United (Shinyanga), Mawenzi Market (Morogoro) na Arusha FC (Arusha).

Akizungumza jana, Katibu wa Dodoma FC, Fortunatus Johnson alisema timu yake imejipanga kuhakikisha inafanya vizuri katika ligi hiyo.

"Tunaamini ligi itakuwa ngumu na kila timu imejiandaa. Hakuna timu tunayoona ni nyepesi na tunaziheshimu zote," alisema Johnson.

Mratibu wa Friends Rangers, Heri Mzozo alisema wachezaji wake wako tayari kuhimili mikiki mikiki ya ligi hiyo. Ligi Daraja la Kwanza imepangwa kuanza mnamo Septemba 14.

Chanzo: mwananchi.co.tz