Ebana eeh! Kocha wa Chelsea Gharam Potter amesisitiza kwamba haofii na hadhani kwamba anaweza kufukuzwa katika kipindi cha hivi karibuni licha ya kuwa kocha mwenye takwimu mbaya zaidi kuwahi kutokea kwenye kikosi cha Chelsea kwa miaka 30 iliyopita.
Potter, 47, ambaye ameichukua timu hiyo kutoka kwa Mjerumani Thomas Tuchel, hadi sasa ameiweka timu hiyo kwenye nafasi mbaya na takwimu zake zinaonyesha kuwa ni kocha aliyefanya vibaya zaidi kwa miaka 30 iliyopita.
Chelsea kwa sasa inashikilia nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na alama 25 ambazo zinaiweka kwenye hati hati ya kuwepo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa mwakani.
Amesaini mkataba wa miaka mitano Septemba mwaka jana na bosi wa Chelsea Toddy Boehly anamkubali sana kocha huyo. Licha ya kuonekana amekalia kuti kavu, katika mahojiano yake ya hivi karibuni Potter alisema:"Mmiliki ni bilionea, ni mtu anayejielewa na makini sana pengine kuliko mimi, hivyo anafahamu changamoto tunazopitia na sehemu ambayo tunahitaji kufika, nimekuwa hapa kwa miezi minne, lakini wiki tano hadi sita zote hatukuwa na wachezaji wetu muhimu ambao wengi walikuwa kwenye timu zao za taifa"
"lengo lamimi kuichukua timu hii ilikuwa ni kuijenga timu kwa sababu nilifahamu kwamba unapitia kwenye nyakati ngumu, nilifahamu kuwa nitakutana na changamoto na sio tu kwamba niliona ofa nikaamua kuja, hapana, niliongea na viongozi walionekana kuwa ni watu wazuri ambao wananisapoti kwenye kila kitu."
Baada ya kuajiriwa aliiwezesha Chelsea kushinda mechi tatu za kwanza ambazo ilikuwa ni dhidi ya Crystal Palace, Wolves na Aston Villa.
Lakini baada ya hapo walishinda mechi moha tu kati ya nane ilizocheza kwenye EPL na imepoteza jumla ya mechi nne kati ya hizo ambazo ni dhidi ya Brighton, Newcastle, Arsenal na Manchester City.
Makocha ambao waliwahi kuwa na takwimu mbovu kama hizi wakati wanaifundisha timu hii ni Ian Porterfield na Glenn Hoddle na Scot Porterfield alifukuzwa mwaka 1993, na nafasi yake ikachukuliwa na Hoddle ambaye mbali ya kuanza vibaya alidumu kwa miaka mitatu kabla ya kupata dili la kuifundisha timu ya taifa ya England.
Potter, ameshinda mechi nne, sare tatu na amepoteza mechi nne kwenye mechi zake 11 za kwanza na hiyo imesababisha kuwepo kwa rekodi ya kuwa kocha aliyeanza vibaya chini ya Toddy ikiwa ni tofauti kabisa na zama za Roman Abramovich.
Rekodi zinaonyesha kuwa kocha wa kwanza kuajiriwa na Chelsea baada ya Roman kuinunua timu hiyo alikuwa ni Guus Hiddink ambaye baada ya mechi 11 za EPL alikuwa ameshinda mechi tisa, akapoteza mechi moja na kutoa sare moja. Kocha mwingine chini ya Roman alikuwa ni Carlo Ancelotti ambaye pia alishinda mechi tisa kai ya 11 msimu wa 2009-10 na akaiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa.
Maurizio Sarri, Luiz Felipe Scolari, Jose Mourinho na Antonio Conte wote hawa walifanikiwa kushinda mechi nane kati ya 11 za Ligi Kuu England.
Avram Grant, Andre Villas-Boas na Frank Lampard hawa walishinda mechi saba wakati Rafael Benitez na Thomas Tuchel hawa walishinda mechi sita kati ya 11 na wakatoa sare nne na kufungwa tatu.
Ruud Gullit, Roberto Di Matteo, Claudio Ranieri na Gianluca Vialli wote hawa walishinda tano kati ya 11.
Hivyo makocha wote wanaonekana kuwa na rekodi nzuri zaidi ya ile ambayo Potter ameiweka akiwa na kikosi hicho kwa msimu huu.