Sijui itakuwaje leo Jumatano. Mashabiki wa soka wa Ligi Kuu England wanaamini ndiyo itakayokuwa siku ya mwisho ya hukumu ya mbio wa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu. Itakuwa soo huko Etihad.
Lakini, kwa sasa presha kubwa ipo kwenye kambi ya Arsenal, ambapo beki wao wa kati, kisiki William Saliba kuripotiwa kwamba ana asilimia ndogo sana ya kuwapo kwenye mchezo huo muhimu kabisa uliobeba hatima yao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Ni wakati watakapokwenda kuwakabili mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City. Mechi hiyo inakutanisha watu kadhaa wanaofahamiana vyema. Pep Guardiola na Mikel Arteta. Gabriel Jesus na Oleksandr Zinchenko dhidi ya mastaa wa Man City.
Lakini, mashabiki wa Arsenal baada ya kumkosa Saliba kwenye mchezo huo, mmoja wao alisema: "Tumekwisha"
Saliba amekuwa nje ya uwanja tangu Machi na tangu wakati huo, Arsenal imeruhusu mabao tisa katika mechi tano. Na mbaya zaidi, kiwango cha timu hiyo kwa sasa kinaonekana kama kimetetereka kidogo, ikivuna pointi tisa tu kati ya 15.
Shabiki wa pilia alisema: "Hatuna tena nafasi. Mchezaji mmoja ambaye alitufanya tuwe washindani, hatuwezi bila ya yeye. Man City wana bahati sana." Shabiki wa tatu aliandika: "Hii imeisha jamani. Kuna nini tena." Shabiki mwingine alisema: "Holding vs Haaland itakuwa kama filamu."
Wakati huu ambao Saliba hayupo, kocha Mikel Arteta amekuwa akimtumia beki Rob Holding, huku chaguo jingine alilonalo ni Jakub Kiwior.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Man City na Arsenal zimekutana mara 51. Arsenal imeshinda mara nyingi, 23, mara 12 nyumbani na 11 ugenini kwenye uwanja wa Man City, ambao wao wameshinda 18, mara 11 nyumbani na saba tu ugenini. Kuna mechi 10 baina yao zilimalizika kwa sare. Lakini, kinachowatisha Arsenal ni rekodi za miaka ya karibuni, ambapo katika mechi tano za mwisho, kikosi hicho cha Emirates kimechapwa zote, kikifungwa mabao 12-2. Safari hii itakuwaje, wakati kitakapopigwa kipute cha kuamua ubingwa. Msimamo unavyosoma, Arsenal wameizidi Man City pointi tano, lakini wapo mbele michezo miwili.
-Arsenal ubingwa wao Arsenal kwa sasa inasubiri tu muujiza wa kubeba ubingwa na hasa kama itashindwa kupata ushindi Etihad kesho. Arsenal inasaka taji lake la kwanza la Ligi Kuu England baada ya miaka 19.
Kikosi hicho kipo vizuri, ukuta mzuri, viungo mahiri na fowadi yao moto yenye wakati kama Bukayo Saka, Gabriel Martinelli na Martin Odegaard.
Kwa mechi walizobakiza Arsenal, njia pekee ya kupata ubingwa ni kuiombea dua mbaya Man City ipoteze kwenye mechi zake nyingine, maana wao njia yao ni ngumu wakimalizana na Man City watakuwa na shughuli mbele ya Chelsea, kisha Newcastle United na Brighton, zote zinazohitaji nafasi za kucheza michuano ya Ulaya mwakani.
Arsenal kama itashinda mechi zote itafikisha pointi 95, ambazo hazitafikiwa na Man City. Kama watafungwa na Man City, basi watamaliza na pointi 90 wakishinda zilizobaki na hapo hawatabeba taji hilo, wakitoka sare watamaliza na pointi 91, ambazo zitafikiwa na Man City. Pagumu kwelikweli.
Hicho ni kipute cha kesho. Mchakamchaka wa Ligi Kuu England utaendelea pia leo Jumanne, ambapo Wolves watakuwa nyumbani kukipiga na Crystal Palace katika mechi matata kabisa, huku Aston Villa wakiwa kwenye kiwango bora kabisa chini ya kocha Unai Emery itakuwa Villa Park kucheza na Fulham na Leeds United watamaliza ubishi na Leicester City.
Leo kipute cha Etihad pekee, bali huko City Groud, Nottingham Forest watakuwa nyumbani kuwakaribisha Brighton, Chelsea wakijimwaga Stamford Bridge kumtafutia ushindi wa kwanza Frank Lampard kwa kukipiga na Brentford, huku West Ham United, ambao kwa sasa wanaonekana kuwa gari limewaka watakuwa London kuwakaribisha Liverpool.
Usiku wa Alhamisi, kutakuwa na mechi tatu ambapo Everton watakuwa Goodison Park kuwakaribisha Newcastle United, huku Southampton wakikipiga na Bournemouth na Tottenham Hotspur watakuwa na nafasi ya kujaribu kufuta machozi ya kupigwa 6-1 kwenye mechi uliopita wakati watakapokuwa nyumbani kuwakaribisha Manchester United. Ni wiki ya moto.
Kipigo kwa Spurs kitakuwa kimefuta rasmi ndoto zao za kukamatia nafasi kwenye Top Four ili kufuzu mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Straika Harry Kane atakuwa na shughuli pevu ya kukabiliana na timu hiyo inayotajwa kuhitaji saini yake, huku Man United ikiamini staa wao Marcus Rashford atarudi kwenye ubora wake.