Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Leo ni shoo shoo Estadi Olimpic Lluis Companys

H8VXWG Leo ni shoo shoo Estadi Olimpic Lluis Companys

Sat, 28 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Barcelona, Xavi amesema kipute cha leo Jumamosi dhidi ya Real Madrid ni mechi muhimu kwelikweli na kuwaambia vijana wake “kazeni buti” wakati miamba hiyo itakapokutana kwa mara ya kwanza kwenye El Clasico msimu huu.

Kipute hicho kitapigwa Estadi Olimpic Lluis Companys, uwanja wa nyumbani utakaotumiwa na Barcelona kwa muda, ambapo timu hizo zitakutana kwa mara ya kwanza tangu Aprili mwaka huu, wakati Real Madrid walipoichapa Barcelona 4-0 kwenye marudiano ya nusu fainali ya Copa del Rey.

Real Madrid kwa sasa inaongoza msimamo wa La Liga ikiwa na pointi 25, moja zaidi ya Barca iliyopo kwenye nafasi ya tatu, huku mabingwa hao watetezi wakiwa hawajapoteza mchezo wowote msimu huu.

“Kwa upande wetu hii mechi ni muhimu sana, mechi ambayo kila mchezaji anataka kucheza,” alisema Xavi.

Barca ilionekana kuwa bora zaidi msimu uliopita, wakati ilipobeba ubingwa wa La Liga ikiwa na mechi nne bado mkononi na ilimaliza pointi 10 juu ya timu iliyoshika nafasi ya pili, Real Madrid.

Lakini, huu ni msimu mpya na mambo ni tofauti. Chama hilo la Xavi limekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu, ambapo kwenye mechi 10 ilizocheza kwenye La Liga, imeshinda saba na kutoka sare tatu, dhidi ya Getafe, Mallorca na Granada na kukusanya pointi 24 zinazowaweka kwenye nafasi ya tatu, pointi moja nyuma ya Girona na Real Madrid. Barca ilishinda 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao kwenye mchezo wa ligi wikiendi iliyopita, shukrani kwa bao la kinda wa miaka 17, Marc Guiu na ilishinda pia 2-1 dhidi ya Shakhtar Donetsk kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Jumatano iliyopita.

Barca ilishinda katika mechi mbili za mwisho ilizokutana na Real Madrid kwenye La Liga. Hata hivyo, mechi hiyo haitapigwa Nou Camp, jambo linaloweza kuleta ugumu kwelikweli. Katika michuano yote, Barca imeshinda mechi nne kati ya sita za mwisho zilizokutana na Real Madrid, licha ya kwamba ubingwa bado, lakini kupata matokeo chanya ni kitu kinachowindwa na makocha wote kwa mchezo huo wa El Clasico.

Real Madrid, nao kwa upande wao walishinda 2-1 katika mchezo wao uliopita wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Braga, usiku wa Jumanne iliyopita. Kocha Carlo Ancelotti atahitaji kuendeleza makali yake.

Real Madrid inategemea makali ya kiungo wake Jude Bellingham kufanya kweli kwenye mechi hiyo, ambapo supastaa huyo wa England amefunga mabao 11 na kuasisti mara tatu katika mechi 12 zilizopita za michuano yote na kuanza kwa moto akiwa na Los Blancos. Hii itakuwa El Clasico yake ya kwanza.

Real Madrid inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi tamu ya safu ya ulinzi kwenye La Liga msimu huu, ikiwa imeruhusu mabao saba tu, wakati Barca imeruhusu 10. Lakini, Barca ni kiboko kwa kufunga, imefanya hivyo mara 22 dhidi ya 21 ya mabao yaliyofungwa na Real Madrid.

Kuhusu kipute hicho, Gary Lineker alisema: “Nikiwa kama mtu wa Barcelona, napata shida sana kumzungumzia mchezaji wa Real Madrid, lakini ukweli Bellingham amekamilika.”

Barca haitakuwa na huduma ya mastaa watatu katika mechi hiyo, ambao ni Jules Kounde, Sergi Roberto na Pedri huku Joao Felix akitarajiwa kuanza licha ya kutolewa kwenye mechi ya Shakhtar. Raphinha naye anaweza kucheza, huku kulidaiwa kuwapo na hofu juu ya wachezaji Frenkie de Jong na Robert Lewandowski.

Kwa upande wa Real Madrid, mastaa Thibaut Courtois na Eder Militao wataendelea kukosekana huku Dani Ceballos akizua hofu kubwa kama ilivyo kwa Arda Guler, huku matarajio ni kumwona Eduardo Camavinga kwenye beki ya kushoto, huku kiungo ikiwa na wakati Toni Kroos, Aurelien Tchouameni na Federico Valverde. Bellingham kama kawaida atakuwapo sambamba na Wabrazili wawili, Vinicius Junior na Rodrygo.

Vikosi vinavyotarajiwa;

Barcelona: Ter Stegen; Cancelo, Araujo, Martinez, Balde; Gavi, Romeu, Gundogan; Yamal, Lewandowski, Felix

Real Madrid: Kepa; Carvajal, Rudiger, Alaba, Camavinga; Valverde, Tchouameni, Kroos; Bellingham; Rodrygo, Vinicius

Chanzo: Mwanaspoti