Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Leeds kumrudisha kocha wa zamani

Leeds Coach Leeds kumrudisha kocha wa zamani

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ndo hivyo. Leeds United inatarajia kumfuata kocha wa West Brom, Carlos Corberan ili kumpa mikoba ya kuinoa baada ya kumfuta kazi Jesse Marsch. Klabu hiyo yenye maskani yake Elland Road ipo juu ya shimo la kushuka Ligi Kuu England kwa tofauti ya mabao tu na mbele yao kuna mechi mbili za kukabiliana na mahasimu wao Manchester United.

Kocha Marsch, 49, alifutwa kazi baada ya kichapo cha mabao 1-0 kutoka kwa Nottingham Forest na hivyo kucheza mechi saba bila ya kushinda. Na sasa Leeds United wanataka kuzungumza na Mhispaniola, Corberan, 39, ambaye aliwahi kuwa Elland Road kwa miaka mitatu kutoka 2017 hadi 2020.

Corberan amekuwa moto West Brom akiiongoza kuingia kwenye mchujo licha ya kurithi kikosi Oktoba mwaka jana kikiwa kwenye hali ngumu.

Ameshinda mechi 11 kati ya 16 alizokuwa Albion, lakini kikosi hicho kinakabiliwa na ukata wa kifedha jambo linaloweza kumshawishi Corberan akatimkia zake Leeds, ambako anafahamiana vyema na Andrea Radrizzani.

Mmiliki wa Leeds anataka kufanya mabadiliko makubwa ya benchi la ufundi baada ya Rene Maric, Cameron Toshack na Pierre Barrieu nao kufutwa kazi. Taarifa ya klabu ilisomeka: “Tungependa kumshukuru Jesse na benchi la ufundi na tunawatakia kila la heri kwenye maisha. Mpango wa kuajiri kocha mpya unaendelea na tunaendelea kuwapa taarifa mashabiki wetu.”

Leeds itashuka Old Trafford leo kukipiga na Man United kwenye Ligi Kuu England. Katika mechi hiyo, Leeds itakuwa chini ya makocha wa muda Michael Skubala, Paco Gallardo na Chris Armas.

Chanzo: Mwanaspoti