Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lazaro atetea mastaa Coastal

Coastal Union Pic Lazaro atetea mastaa Coastal

Sat, 1 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro amesema licha ya timu yao kushika nafasi ya 13, lakini wachezaji waliowaongezwa dirisha dogo wamefanya kazi kubwa, isipokuwa matokeo ya ushindi hayakuwa upande wao.

Wachezaji waliosajiliwa dirisha dogo ni Yusuph Athuman (Yanga), Yema Mwamba (Kakamega Homeboyz), Juma Mahadhi (Geita Gold), Felly Mulumba (Bandari FC), Justin Ndikumana (Bandari FC) na Omary Banda (Huru).

“Wakati mwingine matokeo ya kukosa ushindi yasiwafanye wachezaji waonekane hawana kiwango, soka ni mchezo wa kikatili, kuna muda timu inaweza ikamiliki mpira mwanzo mwisho ila mpinzani akitumia nafasi moja ya kukufunga biashara inaishia hapo,” alisema beki huyo wa kushoto wa zamani wa kimataifa aliyekipiga Coastal, Yanga na Taifa Stars na kuongeza;

“Tuliowaongeza dirisha dogo wamefanya kazi kubwa sana, haijalishi tupo nafasi 13 ukitaka kuamini hilo kipa wetu Ndikumana kaonyesha uwezo mkubwa kaitwa timu yao ya taifa.”

Akimzungumzia Athuman aliyetoka Yanga kwamba alikuwa chaguo lao la kwanza, lakini amekuwa na bahati mbaya ya kuumia mara kwa mara, kutokana na mazoezi magumu.

“Mara aumie kucha, mara goti tena unakuta mechi inatakiwa kucheza siku mbili mbele ama tatu amekuwa na bahati mbaya sana, lakini kama kocha lazima nimpe moyo ili asikate tamaa,” alisema Lazaro na kuongeza;

“Mechi zilizosalia kila mchezaji anataka kucheza, mazoezi yanakuwa magumu wengi wanaumia huko, kila kocha anahitaji mtu aliye tayari kumpa matokeo hasa sisi ambapo tunapambana tusishuke daraja.”

Alisema mbele yao wana mchezo mgumu Aprili 9, wataifuata Dodoma Jiji, hivyo kila mchezaji anapambana kuona anapata nafasi ya kuisaidia timu kupata matokeo ya ushindi ili kuiweka sehemu salama kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Chanzo: Mwanaspoti