Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lameck Nyambaya na ndoto ya kumaliza makundi kwenye soka

41b5db9b862efaaccec53f42707537e8 Lameck Nyambaya na ndoto ya kumaliza makundi kwenye soka

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UKIMWONA ni mpole lakini ukipata wasaa ukazungumza naye ndio utajua kuwa ni muongeaji mzuri. Mara nyingi nakutana naye katika viwanja vya soka kwa sababu ni msimamizi wa ligi mkoa wa Dar es Salaam.

Akiwa kwenye kazi yake kama msimamizi wa ligi huwezi kumsikia akipigizana kelele na watu, yeye anapenda kuwaachia watu aliowakasimisha madaraka kutekeleza majukumu yao na yeye kubaki kuwa msimamizi tu.

Huyu si mwingine ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania, Lameck Nyambaya ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Soka la Vijana Tanzania.

Nyambaya kwenye soka ameanza mbali licha ya kucheza wakati akisoma na kuwa nahodha wa timu, pia alianza kuongoza soka katika ngazi ya wilaya. Safari yake ilianza katika Chama cha Soka Wilaya ya Ilala (IDFA) akiwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho.

Mwaka 2008 aligombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF lakini kura hazikutosha akarudi kujipanga na mwaka 2017 akagombea na akachaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji akiwakilisha Kanda ya Dar es Salaam.

UMOJA KATIKA SOKA

Nyambaya ni kiongozi asiyependa makundi jambo ambalo anatamani liondoke kwa afya ya mpira wa miguu, kwani linakwamisha masuala mbalimbali ya maendeleo ya soka.

“Nafahamu kuwa makundi yanakwamisha maendeleo, kwani baadhi ya viongozi baada ya kuchaguliwa wanabaki kuangalia maslahi kwa manufaa ya makundi badala ya kupigania maendeleo ya soka letu kwa ujumla,” alisema Nyambaya.

SOKA LA VIJANA

Nyambaya anasema soka la vijana ndio msingi wa kuwa na timu ya taifa yenye nguvu, hivyo uwekezaji kwenye soka hilo ndio jambo la msingi.

“Kipindi cha uongozi wa Malinzi nilikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Vijana, Mwenyekiti alikuwa Ayoub Nyenzi, tulifanya vizuri kwani timu yetu ilifuzu kucheza fainali za vijana za Afrika zilizofanyika Gabon 2017,” alisema.

Alisema pia TFF imeendelea kufanya vizuri zaidi katika soka la vijana na kufanikiwa kuandaa fainali za Afrika zilizofanyika hapa nchini 2019, ambazo zilitajwa kufanikiwa zaidi na Shirikisho la Soka Barani Afrika (Caf).

Alisema TFF wana sera ya uwekezaji na kuzalisha vijana licha ya kuwa linatakiwa lifanywe na klabu na akademi wao wabaki kuwa kama walezi tu.

“Kwa sasa kuna vikosi vya U-14, U-17, U-20 na TFF inafanya kazi ya kuwalea na kuendeleza, baadhi yao wapo Fountain Gate Academy na wengine wanaendelea na masomo katika shule ambazo zinaupa kipaumbele soka,” alisema Nyambaya ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa kamati ya soka la Vijana ya TFF.

AJIVUNIA KELVIN

Kelvin John ni mshambuliaji Mtanzania, aliyetokana na fainali za vijana za Afrika zilizofanyika Gabon 2017, ambaye hivi karibuni alijumuishwa kwenye orodha ya wachezaji 60 duniani wanaotarajiwa kuwa hatari siku za hivi karibuni.

Kelvin kwa sasa yupo England kwenye kituo cha kukuza soka cha Club Brooke House College, na amewekwa kwenye orodha hiyo iliyotolewa na gazeti la The Guardian la England.

Gazeti hilo lilieleza kuwa ni ngumu mno kwa mchezaji asiyecheza soka la kulipwa kuingia kwenye orodha hiyo inayotoka kila mwaka, lakini kutokana na kiwango bora cha mshambuliaji huyo aliyezaliwa Juni 10, 2003 imebidi awekwe.

Kwenye orodha hiyo inayoangalia wachezaji chipukizi kutoka duniani kote kuna wachezaji wawili tu kutoka Afrika, mbali na Kelvin yupo Isaac Tshibangu raia wa DR Congo anayeichezea TP Mazembe.

Mshambuliaji huyo alianza kuonekana kuwa ni hatari alipokuwa na umri wa miaka 13 tu kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 iliyofanyika Gabon.

Alisema Kelvin alichukuliwa na kituo hicho cha kukuza soka kilichopo Leicestershire, England, mwaka jana ambapo atakaa hapo mpaka mwakani atakapofikisha umri wa miaka 18 unaomruhusu kusajiliwa na klabu yoyote Ulaya.

AGAWA MIPIRA

Septemba 10, mwaka huu alikabidhi mipira kwa wilaya tano za mkoa wa Dar es Salaam.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa MIGUU Tanzania (TFF), Wallace Karia na Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani.

Karia alitoa shukrani za dhati kwa mjumbe huyo kwa kujitoa kukuza na kuinua soka hapa nchini kwani mipira hiyo itakwenda kusaidia ligi mbalimbali Dar es Salaam.

Pia alisema jambo hilo halijawahi kufanywa na kiongozi yoyote wa kanda ya Dar es Salaam na kuwaomba viongozi wengine kuiga mfano wa Nyambaya kama hamasa ya kuongeza juhudi katika kukuza soka nchini na kusema viongozi wote wana mchango katika kila wanachokifanya hivyo anaheshimu na kutambua juhudi zao.

“Mipira hii imekuja sehemu sahihi katika kanda hii ya Dar es Salaam kwa sababu ni moja ya kanda ambayo ina timu nyingi zinazoundwa na wilaya tano hivyo mipira hii itakwenda moja kwa moja kutumika katika ligi za ndani ya mkoa na itapunguza kwa kiasi fulani changamoto za ukosefu wa mipira katika Kanda ya Dar es Salaam,” alisema Karia kwa furaha.

ATOA NENO

Nyambaya ambaye ni mwepesi kusaidia makundi mengine yanayojihususisha na soka alisema anajua ana deni kwa waamuzi hasa wa mkoa wa Dar es Salaam na kusema anatarajia kufanya jambo kwa ajili yao.

Hivi karibuni alitoa Sh milioni 1 kuwapiga jeki waandishi wa habari za michezo waliokwenda Kenya kuisapoti Taifa Stars.

“Najua waamuzi wanajitolea sana katika soka la mkoa wa Dar es Salaam, hivyo na wao sijawasahau nitafanya jambo kwa ajili yao,” alisema Nyambaya.

UONGOZI

Kuhusu uongozi ameweka wazi nia yake ya kutaka kuwania nafasi ya uongozi katika Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), lakini akasema ni mapema kusema anawania nafasi gani, kwani muda wa uchaguzi haujafika.

Chanzo: habarileo.co.tz