Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lameck Lawi huyooo Ubelgiji

Lameck Lawi Simba Coastal Lameck Lawi huyooo Ubelgiji

Fri, 19 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huku sakata lake likiwa bado halijaamuliwa, mchezaji ambaye amezua sintofahamu kati ya Simba na Coastal Union, Lameck Lawi, muda wowote kuanzia sasa anatarajiwa kuelekea nchini Ubelgiji kwa masuala yake binafsi, imeelezwa.

Simba ilipeleka shauri lake kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuhusu kuvunjiwa mkataba na Coastal Union wa kumsajili beki Lawi kungali walishafanya biashara na kukamilisha malipo, lakini wauzaji wa mchezaji huyo wakazirejesha wakidai malipo yalifanywa baada ya muda wa makubaliano kupita.

Hata hivyo, shauri hilo lilisikilizwa Jumanne wiki hii, kwa pande zote kutoa vielelezo, lakini bado halijatolewa uamuzi wa nani hasa anapaswa kummiliki mchezaji huyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Msemaji wa Coastal Union, Abbas El Sabri, alisema baada ya kurejea Tanga mchezaji huyo aliomba ruhusa ya wiki moja kwa ajili ya safari yake ya Ubelgiji. 

"Kwa sasa Lameck hayupo kambini ameomba ruhusa ya wiki moja kuelekea nchini humo, kwa mujibu wa ruhusa yake anatakiwa awapo kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Agosti 8, mwaka huu, dhidi ya Azam FC," alisema El Sabri.

Alisema kwa sasa wanasubiri maamuzi yatolewe na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kutokana na sakata la mchezaji wao huyo dhidi ya Simba.   Katika hatua nyingine, wakati hayo yakiendelea kikosi cha Simba chenye sura mpya ngingi kinaendelea na maandalizi ya msimu mpya mjini Ismailia, Misri na tayari Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids, amekuwa na nyota wake kwa ujumla. 

Fadlu amekimwagia sifa kikosi chake, akisema kinafundishika kwa urahisi, huku akifurahishwa na uwezo, kasi na nguvu kwa wachezaji wake.

Akizungumza jana akiwa jijini Ismailia, kocha huyo alisema wiki moja tu baada ya kuwapa mazoezi ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na kikosi cha wachezaji aliowakuta, wa zamani na wapya.

Alisema kuna mambo matatu ambayo yamemfurahisha tangu atue kutoka Raja Casablanca na kukinoa kikosi cha Simba.

"Wiki moja tu baada ya kufanya mazoezi na wachezaji wangu nimeridhika kwa kiasi kikubwa na timu niliyokuwa nayo, na sababu kubwa nimewakuta wachezaji wengi wana umri sahihi wa kucheza.

"Kwanza wapo kwenye umri sahihi wa kucheza mpira, miaka kuanzia 19 hadi 25 ndiyo umri wa mchezaji kuwa kwenye kiwango cha juu sana, wachezaji wa aina hiyo ndiyo wamejaa hapa.

"Pili nimefurahishwa na kasi  nguvu walizonazo wachezaji wangu, nadhani hii pia ni sababu ya umri, kwa hiyo wanaweza kucheza soka la kuvutia, lakini pia wanaweza kucheza soka la kutumia nguvu zaidi, kwa maana hiyo wanaweza kucheza katika mazingira yoyote, hivyo kunipa uwanja mpana wa jinsi ya kucheza mechi husika, au kulazimika kucheza kutokana na mpinzani anavyocheza," alisema kocha huyo.

Kingine alisema ni uwezo wao wa kupokea maelekezo haraka, ambapo inarahishia kazi kwenye kukinoa kikosi hicho.

"Tatu ni uwezo wa wachezaji kupokea maelekezo haraka, nina maana wanafundishika kwa urahisi, hiki pia kimenivutia sana," alisema kocha huyo.

Kuelekea msimu ujao, Simba imesajiliwa wachezaji wengi wa ndani na nje kuanzia miaka 18 hadi 25, ikiacha idadi kubwa ya wachezaji ambao umri wao umeanza kuwatupa mkono.

Wakati huo huo, kikosi hicho kitacheza mechi ya kwanza ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga, Agosti 8, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na TFF, mechi hiyo itachezwa saa 1:00 usiku, baada ya mechi ya nyingine kati ya Azam dhidi ya Coastal Union itakayopigwa siku hiyo hiyo, saa 10:00 jioni, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live