TAIFA lipo kwenye majonzi makubwa kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli ambaye jana na leo anaagwa na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Magufuli alikumbwa na mauti katikati ya wiki na anatarajiwa kuzikwa kijiji kwao huko Chato wiki inayoanza kesho, huku wadau wa michezo na burudani wakimlilia kutokana na mchango wake mkubwa kwenye sekta hiyo.
Wengi wameshamzungumza marehemu Magufuli na kueleza namna Watanzania wanavyopitia kwenye kipindi kigumu cha msiba wa JPM.
Niseme kwa ufupi naungana na Watanzania wote kumwombea kiongozi wetu huyo katika safari yake ya mwisho duniani kwa kutambua kila nafsi itaonja mauti na JPM ametangulia tu, nasi tu nyuma yake.
Wakati michezo ikiwa imesimamishwa kupisha maombolezo ya wiki tatu ya msiba huu mzito, bado kuna baadhi ya wadau bado wanamsimanga, Mrisho Ngassa ‘Anko’, wengine wanamteta Ibrahim Ajibu. Sababu ya kuwasakama nyota hao wa soka nchini ni kitendo chao cha kupiga teke fuko la fedha.
Ndio, nyota hao walibahatika kupata ofa ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Ngassa alitakiwa na Al Merrikh ambayo juzi kati tu walikuwa hapa nchini kuvaana na Simba.
Hata hivyo, Ngassa alilikaushia dili hilo. Mahaba yake makubwa dhidi ya Yanga yakamfanya aamue kusalia nchini. Sudan na hasa klabu ya El Merrikh ama Al Hilal zinajulikana kwa uwezo wake kiuchumi.
Tena kipindi hicho hakuna janga la corona. Taifa hili la Afrika Kaskazini, lilikuwa juu kiuchumi na klabu zake zikiwa na uwekezaji mkubwa.
Anko alipotezea dili hilo nono. Wakati mwenyewe amesahau, wadau bado wanaendelea kulia naye. Baada ya muda kupita likaibuka dili jingine kwa Ajibu. Alitakiwa TP Mazembe ya DR Congo.
Inadaiwa aliamini na kuona mkwanja wa Msimbazi ilikuwa bonge la dili kuliko kwenda kuosha nyota yake nje ya nchi.
Wapo wanaodai hakushtushwa na mafanikio makubwa aliyoyapata Mbwana Samatta aliyewahi kuichezea Mazembe kabla ya kuibukia Ubelgiji kisha England na sasa akikipiga Uturuki.
Hakuhamasishwa na mafanikio ya Thomas Ulimwengu aliyerejea klabuni hapo baada ya kuichezea kwa miaka mitano kisha kwenda Sweden, Algeria na Sudan.
Hata hivyo, wapo wanaodai, muda utakuja kuwahukumu baadaye watakapostaafu soka. Binafsi sina cha kuwalaumu nyota hao na wengine ambao wamekuwa wakiimbiwa wimbo huu kwa muda mrefu juu ya kutakiwa kutoka nje na kudharau. Wameibuliwa kutoka wapi? Wanajua faida ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi? Wanao uvumilivu wa kuhimili ‘homesickness’?
Bahati nzuri ni kwamba kwa sasa mambo yamebadilika na jeshi la wachezaji wa Kitanzania linalokwenda nje ni kubwa kulinganisha na miaka ya nyuma.
Vijana wanaoibuka kwa sasa wamekuwa na kiu ya maendeleo. Wanacheza kwa malengo. Wanaangalia wenzao wanaotamba nje wanavyoishi kifalme.
Nao wanapambana kwa kila hali kuvuka mipaka ya nchi. Mafanikio ya Samatta, Simon Msuva na wengine yamekuwa ni chachu kwao. Hata watu wanaowasimamia wengi wao wanawatia moyo katika kuchangamkia dili nje ya nchi.
Nilidhani sasa umefika muda wa kuwatia ndimu makocha wetu nao wachangamke kutoka nje ya nchi kwenda kufundisha.
Vuta picha namna makocha wazawa wanavyochukuliwa ndani ya klabu za soka nchini. Wengi wao pamoja na kuwa na kiwango vikubwa vya elimu ya taaluma hiyo, hawana udhubutu wa kutoka nje. Wameridhika kugeuzwa deiwaka ndani ya Simba na Yanga.
Wanaridhika kutumikishwa chini ya makocha wa kigeni ambao wakati mwingine cv zao ni za kawaida sana. Sijui ni uoga, kutojiamini ama hofu ya kukabiliana na changamoto nje ya nchi ndizo zinazowafanya wahofie kwenda nje ya nchi?
Makocha wazawa wanapaswa waangalie wenzao Warundi wanavyopishana kwenye mipaka ya nchi yao na ile ya majirani. Wajaribu kuwahesabu makocha kutoka Burundi waliopo nchini wapate wivu na wao kutoka nje ya nchi.
Wahesabu makocha kutoka Rwanda, Uganda na Kenya wanavyochakarika kutoka nje ya mipaka ya nje yao.
Kwa nini wao wasifanye kama hivyo, ilihali wana uwezo? Kama Dan Korosso, Sunday Kayuni, Dennis Kitambi na wengine wachache walitesti zali na kufanya makubwa nje ya nchi, makocha wa zama hizi wanashindwaje?
Inawezekana watu wamesahau kuwa, AFC Leopards ‘Ingwe’ ya Kenya inaendelea kuliota jina la Kayuni, kwani ndiye kocha wa mwisho kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya mwaka 1998.
Tangu Kayuni aondoke, Leopards haijawahi kunyakua tena ubingwa wa ligi. Yaani miaka 23 sasa tangu Kayuni awape taji wanalisaka bila mafanikio.
Heshima aliyoiweka Kayuni, ni rahisi ingekutumiwa na makocha wengine kujipenyeza Kenya.
Hawajaiona fursa ilivyo. Ndio maana nataka ile hamasa iliyotumiwa kwa wachezaji, sasa ihamie kwa makocha.
Tanzania ina makocha wenye uwezo, wengine vijana ambao kama wataamua kujilipua wanaweza kufungua soko lao nje ya nchi na kuondokana na hizi dharau wanazopata kwa klabu za nyumbani hasa vikubwa kupenda kuwatumia kama deiwaka.
Inawezekana Burundi au Uganda na hata Kenya wanatushinda kwa kuandaa mipango ya kuzalisha makocha wengi na kuwahamasisha kwenda nje ili kupata ujuzi na kukuza cv zao, tofauti na labda Chama cha Makocha (TAFCA) na hata Shirikisho la Soka (TFF), lakini bado makocha wenyewe wanapaswa kupambana kukuza heshima yao nje ya nchi.
Wakati mwingine wanachukuliwa poa kwa sababu wenyewe wameamua kujiweka katika hali hiyo.
Kama wataamua kuamka sasa na kutafuta malisho mapya hata nchi za jirani kama wenzao wanavyofanya ni wazi watajijengea heshima kubwa.
Zile tabia za kuchukuliwa kama madeiwaka ana makocha wasaidizi wa wageni pale wanapoletwa nchini zitakoma na wataheshimika. Kama tulivyowahamasisha wachezaji kutoka nje, tuigeuzie kwa makocha wetu nao watoke nje.
Sio kutoka nje tu, pia tunahimize kukataa dharau za kugeuzwa madeiwaka katika baadhi ya timu ama kurasimishwa kuwa makocha wasaidizi wa kudumu, wakati uwezo wa kufanya kazi kama makocha wakuu upo.
Imeandikwa na Badru Kimwaga