Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

La Liga ukizubaa imekula kwako!

Watu 7 Waadhibiwa Sakata La Ubaguzi Wa Mchezaji Wa Real Madrid La Liga ukizubaa imekula kwako!

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye msimamo wa La Liga unavyosoma, Real Madrid imeketi kileleni ikiwa na pointi 61 katika mechi 24. Imefunga mabao 52 na kufungwa 15, huku ikishinda 19, sare nne na kichapo kimoja tu. Unachoweza kusema hapo, vijana wa Carlo Ancelotti wapo moto si mchezo.

Chini yake, ipo Girona iliyovuna pointi 56 katika mechi 24.Kisha zinafuatia Barcelona na Atletico Madrid nafasi ya tatu na nne baada ya kukusanya pointi 51 na 48 mtawalia katika mechi 24. Patamu hapo. Wikiendi hii, zinapigwa mechi za raundi ya 25, huku vipute vikitajwa vitatoa mwanga kwenye mbio za ubingwa wa ligi hiyo na vita ya kufuzu michuano ya Ulaya msimu ujao.

Real Madrid watakuwa na nafasi ya kufikisha pengo la pointi nane endapo wataichapa Rayo Vallecano Jumapili.

Katika mchezo huo Kocha Carlo Ancelotti ataendelea kukosa huduma za mabeki mahiri Antonio Rudiger, Eder Militao na David Alaba na kiungo Jude Bellingham anayesumbuliwa na maumivu ya enka.

Wasiwasi unazidi kwa sababu hata Brahim Diaz, ambaye alichukua nafasi ya Bellingham kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya RB Leipzig katika Ligi ya Mabingwa Ulaya naye yupo kwenye hatihati kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kigimbi.

Rayo itaikaribisha Real Madrid ikiwa na rekodi ya kushinda mechi moja kati ya 14 ilizocheza La Liga msimu huu na ilimshuhudia kocha wake Francsico Rodriguez akifutwa kazi na mikoba hiyo kukabidhiwa Inigo Perez, ambaye ataanza kibarua chake kwa kazi ngumu kwelikweli.

Girona watawakaribisha kundini kocha wao Michel Sanchez, beki Daley Blind na kiungo Yangel Herrera ambao walikuwa na adhabu na sasa wapo fiti kuwakabili Athletic Bilbao ugenini katika Uwanja wa San Mames.

Athletic ipo nafasi ya tano katika msimamo na ingeweza kupanda hadi nafasi ya nne kama ingeichapa Almeria, Jumatatu iliyopita. Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Ernesto Valverde hakijapoteza mchezo uwanjani kwao tangu kuanza kwa msimu huu kikishinda sita katika mechi sita za mwisho.

Mastaa wa Athletic wanaweza kuwa na uchovu baada ya mechi ngumu ya Copa del Rey, lakini watapata nguvu kutoka kwa Nico Williams na Gorka Guruzeta wanaorejea uwanjani wakitokea majeruhi.

Barca ilizidi kuangusha pointi wikiendi iliyopita na sasa itakwenda kuwakabili Celta Vigo, leo Jumamosi, huku wakiwa na mawazo pia ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya unaokuja ambao watakwenda kukipiga na Napoli huko Italia. Celta ushindi wa mabao 3-0 walioupata huko Pamplona wikiendi iliyopita ulionyesha matumaini, lakini bado wapo kwenye vita kali ya kupambana wasiporomoke daraja.

Atletico Madrid watatumia wikiendi hii kwenye La Liga watakapokipiga na Las Palmas kama sehemu ya kupasha kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki ijayo.

Cadiz kipigo walichokumbana nacho kutoka kwa Real Betis wikiendi iliyopita ina maaana sasa wamefikisha mechi 20 tangu mara ya mwisho walipopata ushindi kwenye ligi, na wikiendi hii wataifuata Osasuna Valencia iliyofaidika kwa mabao mawili ya dakika za mwisho dhidi ya Las Palmas mchezo uliopita, itakuwa nyumbani kukipiga na Sevilla.

Wa pili kutoka mkiani, Granada watakuwa na kasheshe na wanaoshika mkia Almeria katika mechi inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali baada ya timu hizo kufanya vizuri wikiendi iliyopita na Granada ilipata pointi mbele ya Barcelona na Almeria iliigomea Athletic Bilbao ikiwa na watu 10 uwanjani. Almeria matumaini ya kutoshuka daraja yametoweka, lakini kama watashinda mbele ya Granada wataamsha kidogo morali kupambana ili kubaki kwenye La Liga msimu ujao.

Mallorca itakipiga na Real Sociedad ikiwa zimepita siku 10 tangu zilipokutana kwenye mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Copa del Rey iliyomalizika kwa suluhu na baada ya siku 10 nyingine mbele zitarudiana kwenye kipute hicho cha Copa del Rey.

Mechi ya mwisho kesho Jumapili, Betis ambayo haitakuwa na huduma ya Ayoze Perez na Isco, itajaribu kusogelea nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya kwa kukipiga na Alaves, ambao wamekuwa tishio sana na huduma ya straika wao hatari, Samu. Mambo ni moto La Liga.

Chanzo: Mwanaspoti