Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kyombo: Simba kugumu, aota kucheza Ulaya

Kyombo Aliekuwa Mshambuliaji wa Simba SC, Habib Kyombo

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ndoto ya kucheza soka Ulaya kila mchezaji nchini anayo. Wengine wamefanikiwa kufika huko wakarudi, wengine wanaendeleza moto huko na kuna wale wanaojitafuta ili kutimiza ndoto zao hizo.

Habib Kyombo ni mmoja wa wanaojitafuta ili kuvuka boda. Si kucheza tu Afrika, anaitaka Ulaya na hasa Ligi Kuu England.

Nyota huyo wa Simba aliye Singida Fountain Gate kwa mkopo inayoshiriki Ligi Kuu Bara amewahi kupita kwenye moja ya timu kubwa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na hivyo anajiona ana safari ya kufika mbali na mambo yakikaa sawa yatatimia.

ALIKOTOKEA

Anasema wengi wanawaona mastaa waliko kwenye timu zao, lakini wajue tu wametoka mbali. Si kazi rahisi kufika levo kubwa.

“Sio kazi ndogo. wengi wanawafahamu mastaa kwa kuwaona kwenye timu zao, lakini wametokea mbali kufika walipo na wamechezea timu nyingi ambazo hazifahamiki kama wanazozitumikia kwa sasa.”

Kyombo kabla ya kujiunga na Mamelodi alianzia kwenye Akademi ya Kampuni ya ujenzi ‘DQ’iliyopo Mbezi Beach akiwa kijana mdogo. Baadae alijiunga na Simba B ingawa mambo hayakuwa kama alivyotarajia, kabla ya kupata shavu la kujiunga na Lipuli ya Iringa iliyokuwa ikishiriki ligi daraja la kwanza.

Baada ya kudumu nayo kwa nusu msimu, aliibukia Mbao FC kwa msimu mmoja na nusu kisha Singida alikocheza kwa msimu mmoja ndipo Simba ikamwona na kuinasa saini yake.

ALIVYOTUA MAMELODI

Haikuwa bahati. Ndivyo anavyosema Kyombo ambaye anakumbuka jinsi dili lake la kutua Mamelodi lilivyobuna kutokana na majeraha.

Anasema alienda mamelodi kwa ajili ya majaribio na alifanikiwa na kusaini dili la miaka mitatu.

Hata hivyo, wakati anasubiri msimu wa Ligi Kuu Bara uishe ili akajiunge nao, alipata majeraha yaliyomsababishia kukaa nje kwa muda mrefu.

“Niliona kama ni mkosi. Nilishasaini mkataba wa miaka mitatu, lakini majeraha yakatibua. Hali hiyo ilinikatisha tamaa. Kukaa nje msimu mzinma na nusu sio jambo jepesi kwani unapoteza muda na uwezo unashuka.

Hata hivyo, niliendelea kukaa Sauzi kwa ajili ya matibabu na sikuvunjiwa mkataba. Sikuwa na furaha na maisha ya kule kwani lililonipeleka sikulitimiza. Moyo wangu ulikuwa na shauku ya kurudi tu nyumbani.”

SIMBA MAMBO MAGUMU

Anasema baada ya kupona hakukata tamaa na kuamua kurejea uwanjani akijiunga na Mbeya Kwanza na alicheza kwa miezi sita na kuonyesha uwezo mkubwa ulioleta vita kwa Simba na Singida zilizokuwa zikimhitaji.

Hata hivyo, aliamua kwenda Simba na kilichomvutia ni kwa sababu ni kutimiza ndoto zake za kucheza kimataifa kwani timu hiyo ilikuwa ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Niliingia safari hii Simba kwa heshima, sio kama kipindi kile cha majaribio, hapo nimeshakua hivyo najua ninachokitaka na kwa wakati gani. Hivyo nilichagua kikosi hicho ilikutimiza ndoto zangu za kuonekana kimataifa.”

Hata hivyo, anasema alivyotua Simba hakupata mafanikio makubwa kwani hakupata muda mwingi wa kucheza kutokana na wingi wa wachezaji wenye uzoefu na uwezo mkubwa zaidi yake hali iliyomfanya awe nje au kucheza dakika za mwishoni katika baadhi ya mechi.

“Simba kwangu ilikuwa ngumu sana kupata nafasi na nilikuwa nimetoka kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kabla ya kucheza muda mfupi Mbeya, hivyo nilihitaji muda zaidi kuwa katika uwezo na nguvu ya kucheza mashindano makubwa yanayoshiriki.”

ATUA SINGIDA

“Nikarudi tena Singida msimu huu baada ya kupelekwa kwa mkopo, ila bado nafurahia kucheza kwani ni kikosi ambacho kimeanza kuniamini na kunipa nafasi, hivyo kwangu naona ni fursa ya kuzidi kujitengeneza kuwa bora, lakini zaidi kujiuza kwa kuwa na rekodi nzuri mpaka kufikia mwisho wa msimu.”

“Msimu kwangu ulianza kwa kutokupata nafasi licha ya uwezo wangu wa kuchezea nafasi zote za mbele (7,10,11,9) lakini ngoma bado ilikuwa ngumu, lakini silaumu chochote, furaha yangu ni sasa nafanya mazoezi na juhudi binafsi zilizo washawishi makocha wapya kunipa namba,” anasema Kyombo ambaye soka amerithi kutoka kwa ndugu zake waliomtangulia licha ya kutokucheza timu kubwa kama yeye.

MBAO, LIPULI DUH!

Anasema maisha yamebadilika kwa kiasi kikubwa kwenye safari yake ya soka, kwani alivyokuwa akiishi wakati anapita kwenye klabu za Mbao FC na Lipuli ni tofauti na aliko sasa.

“Lipuli na Mbao, huko maisha hayakuwa mepesi kwani ndio safari ya soka ilikuwa imeanza, hivyo sikuzoea shida za soka na umri hauku mkubwa, hivyo hata uwezo na uvumilivu ulikuwa mdogo kuliganisha na sasa.”

SAUZI KUTAMU

Anasema mazingira na huduma wanazopata wachezaji ndio jambo linalotofautisha Bongo na Sauzi alikoishi akiwa na Mamelodi.

“Mazoezi, muda wa kula, mazingira viko tofauti na ndivyo vianavyowafanya wao kuwa bora zaidi yetu, pia wanaweza kushindana hata na mataifa yaliyoendelea kwenye soka duniani kwani jamaa wanapesa.”

“Mashabiki wa huku kwetu wana mapenzi ya dhati na soka jambo ambalo linawavutia wengi kwa kuendelea kukuza soka letu ambalo sasa limeanza kufahamika kwa kasi ndani na nje ya Afrika.”

AIGOMEA MAMELODI

Anaeleza maisha ya kule yalkimchosha na kuomba kutolewa kwa mkopo kwenye timu yoyote Tanzania, kwani hakuwa amemaliza mkataba aliosaini na klabu hiyo.

“Nilichoka maisha ya kule. Nilikuwa mpweke. Maisha hayakuwa mabaya, ila niliona bora kurudi nyumbani kwani majeraha yalinifanya nisitamani kuendelea kuwa kule, bila kusahau yalitumia muda mrefu na wao hawakuchoka kuniuguza na kunionyesha wananihitaji.”

EPL FRESHI TU

Anasema moja kati ya ndoto zake kubwa ni kurejea tena kucheza nje ya nchi hasa timu za Ulaya na anaamini kupitia juhudi alizonazo atafika mbali zaidi, kwani ligi sasa inakua hivyo uwezekano wa kufika huko upo.

Anasema anatamani kucheza ligi hizo na hasa Ligi Kuu England kwani ni ndoto za wengi.

“Sasa idadi ya wachezaji wanaocheza nje inaongezeka kwa kasi, mimi bado ni mdogo, naweza kupata nafasi ya kutumika huko, hivyo sina mashaka, naamini nitafikia malengo yangu niliyoyapanga kwa muda mrefu. Hata EPL freshi kwangu kama nitafika huko.”

STAILI YA USHANGILIAJI

Anaeleza maana ya staili yake ya kushangilia pale anapofunga goli; “Huwa natembea kama bosi kwa sababu ukifunga lazima watu washangilia ndio maana naonyesha ishara ya kuvimba na maringo.”

HAKUNA ZAIDI

Kuhusu nani anayemkubali Ligi Kuu hasa katika nafasi anayocheza, anasema hakuna zaidi, kwani wote kwake ni wachezaji wazuri ndiyo maana wamechaguliwa kucheza.

“Hakuna aliye zaidi, wachezaji wote ni sawa kwangu kwani katika nafasi hii wanaocheza ni wengi na ni rafiki zangu hivyo utakuwa mzozo nikiona mwingine namkubali kuliko wengine.”

MKATABA SIMBA

Habibu anaeleza kuhusu mkataba wake na Simba baada ya kwenda Singida kwa mkopo na jinsi ilivyokaa, “Nilisaini Simba miaka miwili inayoisha msimu huu na baada ya hapo nitakuwa huru, siwezi kusema sana kuhusu masharti yake lakini bado mimi ni mchezaji wao.”

Chanzo: Mwanaspoti