Klabu Bingwa nchini England Manchester City imempa ofa ya mkataba mpya beki wa England, Kyle Walker ili kujaribu kumshawishi abaki katika klabu hiyo msimu huu wa majira ya joto, kwa mujibu wa Tovuti ya 90minutes.
Walker ameingia katika miezi 12 ya mwisho ya mkataba wake wa sasa na amekuwa akilengwa na Mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich, ambao wanatazamiwa kufanya mabadiliko katika beki ya kulia huku Benjamin Pavard akitaka kuondoka Allianz Arena.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, bado hajafanya uamuzi kuhusu mustakabali wake.
Kuachwa nje ya kikosi cha kwanza wakati wa mchezo wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inaeleweka kumuumiza Walker na kuzua maswali juu ya kuendelea kwake hapo Manchester.
City wanatamani kumuona Walker akifanya uamuzi hivi karibuni na wanatumai kuwa beki huyo mkongwe atachagua Kubaki.
Vyanzo vimeiambia 90min kwamba wameongeza ofa ya mkataba mpya kwa Walker ili kujaribu kumbakiza.
Walker ndiye anayepewa kipaumbele na Bayern katika nafasi yake ya beki wa kulia ingawa miamba hao wa Bundesliga bado hawajakataa ofa mpya ya mchezaji mwenza wa City, Joao Cancelo, ambaye walitumia miezi sita iliyopita.
Pia Walker ana ofa kutoka Saudi Arabia, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham anaamini kuhamia Mashariki ya Kati kunaweza kuharibu nafasi yake kwenye kikosi cha England kwenye Euro 2024.