Kwa madaraja ya timu zinazokutana kwenye mchezo wa leo, natarajia kuona mpira uliotulia, pasi nyingi na kupeana nafasi ya kucheza sio kukamiana na kugongana ‘kuvamiana.’
Kwa siku za karibuni, Simba imeruhusu magoli matatu katika mechi mbili za mashindano ya CAF [CAF Champions League] dhidi ya Power Dynamos ya Zambia. Simba iliruhusu magoli mawili ugenini na goli moja nyumbani.
Lakini pia Simba imefunga magoli matatu kwenye mechi mbili za kimataifa dhidi ya Power Dynamos, ilifunga magoli mawili ugenini [Zambia] halafu ikafunga goli moja nyumbani [Dar, Tanzania].
Kwa upande wa Al Ahly, kwenye mechi mbili zilizopita za mashindano ya CAF wamefunga magoli saba bila kuruhusu goli. Mechi ya kwanza ugenini dhidi ya St. George ya Ethiopia, Ahly ilishinda 3-0 na mchezo wa marudiano Cairo, Misri wakashinda 4-0.
Ukiangalia kwenye upande wa Ligi, Simba inaongoza Ligi ya Tanzania lakini pia Al Ahly inaongoza Ligi ya Misri.
Simba inabebwa na historia ya mechi mbili zilizopita dhidi ya Al Ahly kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Mnyama kashinda mechi zote lakini kwa michezo miwili ya hivi karimbuni ambayo Simba ugenini imepoteza yote. Kwa hiyo kila timu inatamba kwake.
Mchezo wa leo ni tofauti na michezo kadhaa iliyozikutanisha hizi timu, kwa sababu timu hizi zilikutana kwenye hatua ya makundi ambako alama ndio ilikuwa kitu muhimu. Sasa timu hizi zinakutana kwenye mechi mbili za mtoano ambapo mshindi atapatikana baada ya matokeo ya jumla ‘aggregate.’
Al Ahly ni timu inayoogopwa sana kwenye michezo ya mtoano, wanaweza kusuasua kwenye michezo inayohitaji kukusanya alama kama ilivyokuwa msimu uliopita kwenye hatua ya makundi la Ligi ya Mabingwa Afrik, lakini wakifika hatua ya mtoano habari inakuwa nyingine.
Kwa upande wa Simba bado kikwazo chao kimekuwa kwenye hatua za mtoano kwenye mashindano ya CAF, pengine wanaweza kuanzia hapa kwenye African Football League kuvuka kikwazo hicho na kwenda mbele.