Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwanini kila mtu anamtaka Moises Caicedo?

Skysports Moises Caicedo Brighton 6016302 Moises Caicedo

Thu, 29 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Brighto ipewe maua yake. Miaka mitatu iliyopita Moises Caicedo alikuwa akiichezea Independiente del Valle inayocheza Ligi ya Serie A huko Ecuador. Usingesikia kitu kuhusu yeye. Na hatukuwa tukimsikia.

Lakini, Brighton wao walimsikia. Walimnasa Caicedo kwa Pauni 4.5 milioni tu. Miaka mitatu baadaye, ikimtoa kwa mkopo mara moja, sasa hivi Brighton wanamuuza kwa Pauni 80 milioni. Faida mara ngapi hiyo?

Na sasa, klabu kibao ikiwamo Arsenal waliojaribu kumnasa Januari na sasa Chelsea, wanahitaji saini yake. Manchester United, Manchester United na vigogo wengine kuna nyakati vilitajwa pia kuhitaji saini ya mkali huyo.

Lakini, ni kwasababu gani?

Kwa bei ya Pauni 80 milioni kwa mchezaji aliyeonyesha ubora kwa msimu mmoja tu ni pesa nyingi. Ada hiyo ya Pauni 80 milioni kama italipwa, basi itamfanya Caicedo kuwa kiungo wa sita ghali zaidi duniani. Lakini, umri wake wa miaka 21 na kuimarika kwa ubora wake uwanjani, unafanya bei anayouzwa Caicedo kuwa ya kawaida.

Je, ni kitu gani kinachowavutia wanaomtaka?

Caicedo ni injini ya mafanikio ya Brighton kwa msimu wa 2022-23. Alicheza kwa kiwango bora kuisaidia timu hizo kumaliza nafasi za juu kwenye Ligi Kuu England na kufuzu kucheza michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza kwenye historia yao.

Kuna wachezaji wawili tu (Pascal Gross na Lewis Dunk) waliocheza dakika nyingi 3,140 kumzidi Caicedo kwenye kikosi cha Brighton. Alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Brighton kwenye kiungo huku kingine ni uwezo wake wa kucheza beki ya kulia, nafasi ambayo alitumika kwenye mechi ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Manchester United mwanzoni mwa Mei. Amekuwa akitumika kwenye safu ya viungo wawili ama Gross au Alexis Mac Allister, aliyetimkia Liverpool.

Wakati wengine wakitumika kwenye ubunifu, Caicedo yeye alikuwa na kazi ya kukaba tu na kunyang'anya mipira. Shughuli ya kukaba inayofanywa na Caicedo ndiyo inayofanya timu nyingi kuhitaji saini yake. Caicedo alikaba uwanja mzima.

Shughuli ya kuwalinda mabeki wa Brighton ilifanywa na mkali huyo kwa ustadi mkubwa. Caicedo alionyesha uwezo mkubwa wa kukaba, kupora mipira na kuirudisha kwenye umiliki. Huko nyuma shunguli kama ya Caicedo ilikuwa ikifanywa na N'Golo Kante.

Kwenye kazi ya kukaba, Caicedo amefunika kwenye maeneo mengi. Ni Joao Palhinha wa Fulham peke yake ndiye aliyepiga takolin nyingi kumzidi kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita (144 kwa 100), na ni Declan Rice pekee aliyenasa mipira mara nyingi njiani kumzidi (63) zaidi ya Caicedo (56).

Alikuwa bila ya mpira, Caicedo aliwafundisha wachezaji wote wa Brighton namna ya kukaba. Sio ishu ya kutibua mipango, nguvu moja kubwa ya Caicedo ni kurudisha mipira kwenye himaya ya timu yake na kuanzisha mashambulizi ya haraka. Kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, Caicedo alipora mipira na kuanzisha mashambulizi mara kibao, akipiga mashuti 18 kwa staili hiyo. Alizidiwa na Rodri tu, (19).

Kwa msimu huo uliopita, mashambulizi yaliyoanzishwa na Caicedo yalishiia kwa Brighton kufunga mara 11. Kingine kwenye ubora wa Caicedo ni kwamba anaponyang'anya mipira, anapiga pasi kali sana, usahihi wa pasi zake ni asilimia 88.9. Alikuwa sahihi kwa asilimia 92.5 kwa pasi fupi, asilimia 90.5 kwa pasi saizi ya kati na asilimia 79.2 kwa pasi ndefu.

Mara zote, ndiye mchezaji wa kwanza kupokea mipira kutoka kwa mabeki wa kati wa Brighton katika kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma. Caicedo alitengeneza nafasi 41 kwa msimu uliopita.

Wakati sasa N’Golo Kante akitimkia zake Saudi Arabia, Caicedo atakuwa mkali mpya, anayekaba kuzidi maelezo na ndio maana Chelsea inahitaji huduma yake ili akazibe pengo litakaloachwa wazi na Mfaransa huyo.

Chanzo: Mwanaspoti