Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwanini Man United ipambane kumnasa Kane

Harry Kane Galla Harry Kane

Sat, 29 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mweyekiti wa Tottenham Hotspur, Daniel Levy amepewa maagizo ya kuhakikisha anamuuza straika Harry Kane kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kama atashindwa kumshawishi asaini mkataba mpya.

Jambo hilo linafungua milango kwa Manchester United kurudi upya kwenye msako wa straika huyo. Hata hivyo, Bayern Munich ndiyo wanaonekana kuwa siriazi kwenye kuhitaji saini ya Kane baada ya kupeleka ofa zao mbili, ikiwamo ya Pauni 70 milioni na bila ya shaka wataongeza dau na kurudi tena kwa mara ya tatu huko Spurs ili kung'oa saini ya mshambuliaji huyo.

Paris Saint-Germain nao wametajwa kuingia kwenye mbio za kuhitaji saini ya Kane endapo kama wataachana na straika wao Kylian Mbappe kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Hata hivyo, Man United inahitaji zaidi huduma ya Kane, hivyo watalazimika kupambana kuzipiku timu zote zinazomtaka mchezaji huyo ili wamnase wao kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kuna uwezekano mkubwa wa Man United kunasa saini ya Kane kama wataweka jitihada kutokana na mshambuliaji huyo mwenyewe kufikiria kubaki kwenye Ligi Kuu England ili kuvunja rekodi ya mabao ya muda wote inayoshikiliwa na Alan Shearer. Hizi hapa sababu za Man United kupambania Kane atue Old Trafford kuliko kwenda Allianz Arena au Parc des Princes.

Ndiye Namba 9 wa kweli

Kocha Erik ten Hag amesisitiza kwamba anahitaji Namba 9 wa kweli na wa kiwango cha dunia kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi ili kikosi chake kiwe cha kibabe zaidi. Na kwenye hilo, Kane ni chaguo sahihi kwa mastaa waliopo sokoni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Uzuri wa kuwa na Kane kwenye kikosi chako ni kwamba anakupa uhakika wa mabao zaidi ya 30 kwa msimu mmoja. Magwiji kibao wa klabu ya Man United wameshauri mabosi na kocha wa timu hiyo kuhakikisha wanapambana kumnasa Kane kwani ni Namba 9 atakayewafanya wawe washindani wa kweli kwenye Ligi Kuu England.

Sababu nzuri ya kupiga chini kibao

Man United tayari imeshatumia zaidi ya Pauni 100 milioni kuwanasa Mason Mount kutoka Chelsea na Andre Onana kutoka Inter Milan. Jambo hilo limewafanya bajeti yao kuwa ndogo sana kwenye usajili na bado wanahitaji straika na kiungo mkabaji.

Lakini, kama watahitaji kumwongeza Kane na ili kufanya hivyo italazimika wachezaji wengine waondoke, hakuna shabiki wa soka atawashangaa Man United kwa kuwaondoa wachezaji kama Harry Maguire kwenye kikosi ili kufungua milango ya kumnasa straika huyo. Man United inaweza kuwaondoa Anthony Martial, Donny van de Beek na Fred ili kumleta Kane na hakuna atakayeshangaa.

Hushindani na Man City ukiwa na Hojlund

Mwanzoni walipoona kuna ugumu wa kumsajili Kane, Man United walihamia kwenye vita ya kunasa saini ya straika wa Atalanta, Rasmus Hojlund. Kinda huyo si mbaya na uchezaji wake unamfanya alinganishwe na Erling Haaland na hivyo kupachikwa jina la "Erling Haaland wa Denmark".

Hojlund kwenye ligi ya Serie A msimu uliopita alifunga mabao 10. Sawa kuna matumaini makubwa ya straika huyo kuwa moto kwa siku za baadaye, lakini kama atauzwa Pauni 80 milioni kwenda juu, kwanini pesa hiyo isilipwe kunasa saini ya Kane? Ipo wazi Man United ikiwa na Kane itaweza kuchuana na Manchester City kwenye mbio za ubingwa, lakini hawatakuwa na nguvu hiyo kwa kuwa na huduma ya Hojlund kwenye fowadi yao.

Kwenda ng'ambo sio chaguo la kwanza

Kwa mujibu wa gazeti la Bild, mke wa Kane ameonekana akitafuta nyumba huko Munich ikiwa ni maandalizi ya mumewe kujiunga na Bayern wanaojiandaa kupeleka ofa ya tatu huko Spurs ili kumnasa mkali huyo.

Wanandoa hao wanatarajia mtoto wa nne na familia yao inaonekana kutulizana England, kitu ambacho Kane atapenda kuendelea kubaki kwenye makazi aliyoyazoea kuliko kwenda kwenye makazi mapya. Kingine, chaguo la kwanza la Kane ni kubaki England kama atapata fursa kwenye timu itakayompa uhakika wa kupambania mataji huku akifukuzia rekodi ya mabao kwenye Ligi Kuu England.

Kama Man United itaweka dhamira kidogo tu ya kuhitaji saini ya Kane ni uhakika mkubwa, straika huyo ataweka kando mpango wa kutimkia Ujerumani au Ufaransa.

Nini kinafuata?

Muda unakwenda kasi sana kwa Kane katika kutimiza ndoto zake za kuhama katika dirisha hili. Ni ama kuachana na Spurs sasa au klabu hiyo itapata hasara kama itamuacha hadi mwakani aondoke bure.

Kocha mpya wa Spurs, Ange Postecoglou anataka sakata la straika huyo likamilishwe mapema kabla ya dirisha kufungwa na msimu mpya kuanza. Kwa mambo yalivyo, Man United inapaswa kufanya kama klabu kubwa ambavyo inafanya, iingie kibabe kwa mchezaji huyo na kwenda kunasa saini yake.

Man United mara ya mwisho kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England ilikuwa 2013, lakini kama watapata saini ya Kane watakuwa na matumaini ya kushindana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England. Man United inahitaji saini yake.

Chanzo: Mwanaspoti