Msimu wa mwaka 2022/23 wa soka nchini unahitimishwa rasmi Juni 12, mwaka huu kwa kusindikizwa na tuzo mbalimbali zitakazotolewa kwa wachezaji waliofanya vyema kwenye Ligi Kuu, Championship, First League, Kombe la Shirikisho, Ligi ya Wanawake na tuzo za heshima.
Mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Azam na Yanga utakaopigwa Juni 12, mwaka huu katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ndiyo utakuwa wa mwisho msimu huu kisha utafuatiwa na hafla ya tuzo zitakazotolewa usiku huo jijini Tanga.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeshatangaza orodha ya wachezaji walioteuliwa kuwania tuzo mbalimbali katika ligi zote nchini zikiwahusu makipa, mchezaji bora, mabeki, washambuliaji, viungo, makocha, timu yenye nidhamu na chipukizi bora.
Mwanaspoti imefanya tathmini yake na kubaini kuwa ni vigumu kwa orodha ya wachezaji waliopo hapo chini kukosekana katika kinyang’anyiro hicho, yaani tuzo hizo zinawahusu sana tu kwa kazi kubwa waliyozifanyia timu zao msimu huu;
FISTON MAYELE
Straika wa Yanga kutoka DR Congo, Fiston Mayele anastahili kubeba tuzo ya Mchezaji Bora kutokana na namna alivyopambana kuhakikisha klabu yake inachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na lile la Azam na kubeba ngao ya jamii.
Mkali huyo mwenye umbo refu, nguvu uwanjani, kasi na akili awapo mbele ya goli, amekuwa mwiba kwa mabeki watata, akifanikiwa kufunga mabao 16 ya ligi na kuwatengenezea wenzake manne kati ya mabao 56 yaliyofungwa na timu yake msimu huu, huku akifunga saba ya Shirikisho Afrika.
Mayele alikuwa na kasi uwanjani akifunga baadhi ya mabao kwa juhudi binafsi akiwa na uwezo wa kufunga kwa kichwa, tiktaka, mguu wa kushoto na kulia, ambapo alifunga mabao tisa kwa mguu wa kulia.
Msimu uliopita aliambulia tuzo ya bao bora la msimu ligi kuu, huku akifunga mabao 16 akizidiwa bao moja na George Mpole wa Geita Gold aliyefunga mabao 17 lakini msimu huu ana uhakika wa kuwa mfungaji bora. Juhudi zake za kusaka na kupachika mabao ndiyo maana anaingia kwenye kinyang’anyiro hiki.
DJIGUI DIARRA
Kama ilivyo kwa straika Fiston Mayele, huwezi kuyazungumzia mafanikio ya Yanga msimu huu katika mashindano mbalimbali bila kumtaja kipa wa kikosi hicho, Djigui Diarra ambaye amekuwa mhimili muhimu kwenye timu hiyo akiipa mafanikio lukuki.
Wasifu wake msimu huu unaweza kuufananisha na kiungo muhimu mwilini akiwa ni kipa mwenye cleen sheet nyingi Ligi Kuu (16) akifuatiwa na Aishi Manula (Simba) mwenye 12.
Kama ilivyokuwa msimu uliopita alipoibuka kuwa kipa bora basi msimu huu licha ya kukabiliwa na upinzani wa Aishi Manula wa Simba na Benedict Haule wa Singida Big Stars, wataalamu wa ufundi wa TFF hawatafanya makosa, kama watamchagua kuwa kipa bora wa Ligi Kuu.
HENOCK INONGA
Beki wa kati kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Henock Inonga amekuwa nguzo kubwa katika eneo la ulinzi la Simba msimu huu, licha ya timu hiyo kutoambulia kombe lolote msimu huu lakini ubora wake haukujificha.
Inonga ambaye alichukua tuzo hiyo msimu uliopita, kiwango chake hakikuwahi kushuka tangu msimu uliopoanza hadi ulipomalizika Juni 12, 2023 akiwa na uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi, kupora mipira kwa adui, kuchezea mpira na kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma akifunga mabao matatu msimu huu.
Mabeki wengi kama Dickson Job na Bakari Mwamnyeto wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe wa Simba wamefanya vizuri, lakini Inonga anastahili kuchaguliwa kuwa beki bora kwani ukuta wa Simba ukiongozwa naye umeruhusu mabao machache kwenye ligi (15).
CLATOUS CHAMA
Kiungo wa Simba, Mzambia Clatous Chama, ameingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya Kiungo bora kutokana na namna alivyoisaidia timu hiyo tangu mwanzoni mwa msimu katika mashindano mbalimbali akitengeneza nafasi za mabao na kufunga pia.
Licha ya kutokuwa na uwezo mkubwa wa kukaba, Chama ndiye injini ya Simba kwani alichezesha timu vile inavyostahili, na alikuwa na uwezo wa kufunga pia. Mabao yake manne na assisti katika Ligi ya Mabingwa Afrika yaliisaidia Simba kufika robo fainali.
Chama ndiye kinara wa assisti kwenye ligi kuu akiwa nazo 15 na kufunga mabao manne akihusika kwenye mabao 18 kati ya 66 yaliyofungwa na timu hiyo kwenye ligi na kuisaidia Simba kukamata nafasi ya pili, huku ikifika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.
NASREDINNE NABI
Ndiye Kocha bora wa msimu uliopita akiiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam na ngao ya jamii, msimu huu mambo yamemuendea vyema akidhihirisha jina la utani ambalo wadau wengi wa soka wamempachika la ‘Profesa Nabi’.
Nabi mwenye uraia wa Tunisia na Ubelgiji amekuwa tishio msimu huu kwenye mbinu, uendelezaji na ukuzaji wa viwango vya wachezaji, upana wa kikosi, ufundi na mabadiliko ya maana ya wachezaji kadri ya ugumu wa mechi, uwanja na ratiba.
Ameiongoza Yanga kubeba taji la Ligi Kuu, ngao ya jamii, ameifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, huku akiiongoza timu hiyo kuandika historia kwa kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
SAIDO NTIBAZONKIZA
KIUNGO Mshambuliaji, Saido Ntibazonkiza raia wa Burundi amekuwa na msimu mzuri akizitumikia Geita Gold na Simba katika Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam.
Staa huyo aliyejiunga na Simba dirisha dogo amekuwa panga pangua katika kikosi cha kwanza chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, Ntibazinkiza ndiye mchezaji aliyehusika na mabao mengi zaidi msimu huu kwenye ligi (22).
Amefunga mabao 10 na kutengeneza mengine 12, huku akifunga mabao saba kwa mguu wa kulia na kufunga hattrick moja dhidi ya Tanzania Prisons ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 7-1.
BRUNO GOMES
Kiungo wa Singida Big Stars, Bruno Gomes ni miongoni mwa wachezaji wanaoingia kwenye kinyang’anyiro cha uchezaji bora na viungo bora kutokana na namna alivyojitolea klabuni mwake licha ya ugeni wake na soka la Afrika na ikiwa ni mara yake ya kwanza nchini.
Bruno mwenye mwonekano wa mwili mdogo na sura ya upole ambaye ukimuona unaweza kumdharau, lakini alikuwa hatari mbele ya mabeki wa timu pinzani, mkali wa mipira ya kutenga, kutengeneza mabao, kucheza kwa akili na kasi.
Kiungo huyo raia wa Brazil ambaye amekuwa akitumika kama kiraka kwenye timu hiyo akiwa na uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali katika eneo la kiungo na ushambuliaji ndiye kinara wa mabao wa Singida BS akifunga tisa.
CLEMENT MZIZE
Mshambuliaji huyu kinda wa Yanga ameingia kwenye vipengele vinne vya tuzo ya Mchezaji Bora chini ya umri wa miaka 20 (tuzo ya Ismail Khalfani), chipukizi bora, Mchezaji Bora Kombe la Shirikisho (FA) na mfungaji bora shirikisho.
Mzize ambaye ameaminiwa kwa mara ya kwanza na Kocha Nasredine Nabi katika kikosi cha Yanga amekuwa na kiwango kizuri msimu huu katika kufunga mabao likiwamo bao pekee na la ushindi dhidi ya Kagera Sugar lililowapa Yanga pointi muhimu kwenye mchezo huo mgumu uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Chipukizi huyo amefunga mabao sita katika Kombe la Shirikisho la Azam akizidiwa bao moja na Andrew Simchimba wa Ihefu mwenye mabao saba, hata hivyo Mzize ana nafasi ya kufunga zaidi katika mchezo wa fainali dhidi ya Azam Juni 12, mwaka huu katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kwa alichokifanya msimu huu akionyesha ubora na mwendelezo wa kiwango chake na kuwaweka benchi mastaa wa nje na wazawa katika kikosi cha Yanga, anastahili kuchaguliwa kuwa mchezaji bora chipukizi msimu huu mbele ya Edmund John (Geita Gold) na Lameck Lawi (Coastal Union).
MOHAMED HUSSEIN ‘TSHABALALA’
Huwezi kuwataja wakali wa Simba, ukamsahau beki huyu wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye kwa mwonekano ana umbo dogo, lakini alikuwa tishio kwa washambuliaji mbalimbali huku akiwa mmmoja ya wachezaji waliocheza mechi nyingi msimu huu bila kupata majeraha au kushuka ubora wake.
Hadi Simba inamaliza kwenye nafasi ya pili, sehemu kubwa ya mafanikio ya klabu hiyo yalitokana beki huyo. Alijua kuichezesha timu kwa kukaba na kupandisha mashambulizi, krosi zake za mwisho, ndiyo zilizalisha mabao ya kikosi hicho.
Ambapo, ni kinara wa mabeki wenye assisti kwenye ligi msimu huu akitengeneza assisti sita sawa na mwenzake, Shomari Kapombe.
SIXTUS SABILO
Mshambuliaji wa Mbeya City amefunga mabao tisa na kutengeneza mengine saba kwa wenzake kati ya mabao 31 ambayo timu yake imefunga msimu huu.
Alikuwa akikimbizana na Fiston Mayele (Yanga) na Moses Phiri wa Simba katika upachikaji mabao, lakini alikuja kudondoka dakika za mwishoni baada ya kupata majeraha huku timu yake ikipoteza mwelekeo kutokana na matatizo ya kiuchumi.
Kama angendeleza makali yake huenda Mbeya City na yeye binafsi wangekuwa kwenye namba nzuri ambapo angekuwa na idadi nzuri ya mabao na assisti huku timu yake ikiwa kwenye nafasi nzuri katika ligi.
DONISIA MINJA
Mshambuliaji wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake, JKT Queens amekuwa tishio msimu huu akiibeba timu yake mabegani na kuisaidia kutwaa ubingwa huo walioupoteza kwa misimu mitatu mfululizo mbele ya Simba Queens.
Amefunga mabao 15 katika mechi 18 za ligi hiyo msimu huu, huku akifunga hattrick tatu (kinara), hivyo wataalam kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF) hawatakosea kama watamchagua kuwa mchezaji bora wa ligi ya wanawake.
WINFRIDA CHARLES
Winga huyu kinda wa Alliance Girls ya Mwanza amefanya mambo makubwa katika Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu, akifunga mabao 13 katika mechi 18 na kuisaidia timu yake kumaliza kwenye nafasi ya tano. Winfrida ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Alliance, Mwanza amefunga hattrick mbili, licha ya uchanga wake lakini amekuwa tishio kwa nyota wa kimataifa katika upachikaji mabao.
Amekuwa na mwendelezo mzuri wa kiwango chake, ambapo msimu uliopita alifunga mabao 12, kwa alichokifanya msimu huu anastahili kuchaguliwa kuwa chipukizi bora wa Ligi ya Wanawake.
EDWARD SONGO
Straika wa JKT Tanzania ameteuliwa kuwania kinyang’anyiro cha tuzo ya Mchezaji Bora wa ligi ya Championship baada ya kuisaidia timu yake kumaliza kinara wa ligi hiyo na kupanda daraja kwenda Ligi Kuu.
Songo ambaye msimu uliopita alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi hiyo, msimu huu kiwango chake hakikushuka tangu mwanzo wa msimu akiibeba timu yake na kufunga mabao 18 katika michezo 28 na kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.
Mabao hayo ni mwendelezo wa alichokifanya msimu uliopita ambapo aliibuka pia mfungaji bora wa Championship akiweka kambani mabao 17. Songo anastahili kuchaguliwa kuwa mchezaji bora kutokana na umahiri wake wa kufunga.