Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwani Ligi za Wilaya, Mikoa zilikufa?

Karia 1?fit=1280%2C720&ssl=1 Kwani Ligi za Wilaya, Mikoa zilikufa?

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ndiyo, Simba na Yanga zinatupumbaza! Zinasababisha tujione tunakua kisoka, kumbe ndio tunazidi kudidimia.

Ukiona maelfu ya watu wamezifuata klabu hizo mbili na kongwe nchini, utaamini mpira wetu umefikia kiwango kikubwa cha klabu za Misri, Algeria, Morocco na Tunisia. Kumbe, kiuhalisia bado tuko huko Djibout na Somalia.

Ukigeukia vyombo vya habari kufuatilia habari za michezo, utakuta vimejaa mambo yanayohusu klabu hizo mbili.

Habari zinaweza kuwa tano tofauti, lakini zinahusu Simba na Yanga, ila zimegeuzwageuzwa kupumbaza msomaji au mfuatiliaji.

Mijadala imejaa mambo ya Simba na Yanga na sasa hata maoni ya wapenzi wa michezo au soka, yanaelekezwa kuzizungumzia Simba na Yanga.

Ndio maana hakuna hata mazungumzo kuhusu ligi za chini kwa kuwa Simba na Yanga zimetuteka akili.

Huwezi kuonekana una busara au akili, ukizungumzia masuala mengine muhimu ya michezo, bali utaonekana una hoja ukizungumzia Simba na Yanga. Kweli tumepumbazwa akili.

Wakati Morocco inatwaa kila kombe, wengi walifuatilia kutaka kujua siri ya mafanikio. Na jibu lilikuwa jepesi wamezingatia soka la watoto. Na soka la watoto si suluhisho pekee la matatizo ya mpira, bali mfumo mzima unaoweza kuwapokea hao watoto kuwapa ushindani kabla ya kufikia ligo za juu.

Mpira wa sehemu yoyote hauwezi kuendelea kama utazungumziwa kwa kuangalia juu, bali kuanzia chini kwa sababu haupo hewani. Ni lazima una misingi. Ajabu ni kwamba wetu upo hewani.

Wakati tunakua tulizoea kwenda viwanjani kushuhudia mechi za ligi za wilaya. Na kwa kuwa tulikuwa karibu na uwanja wa klabu ya Sigara (TCC) na hivyo kutokosa mazoezi yao, uongozi wa kampuni uliandaa usafiri kwa ajili ya mashabiki kwenda kushuhudia mechi zao za ligi ya wilaya na baadaye mkoa na hata kanda pale zinapofanyika Dar es Salaam.

Kwa hiyo tulizoea viwanja vingi wa Dar es salaam kama Tandika Mabatini kwa Temeke na Karume, Na si hivyo tu, tulijua wapinzani wa Sigara wilayani, mkoani na katika mashindano ya kanda. Na zaidi, tulijua hata wachezaji wazuri wa timu pinzani.

Kwa hiyo ilikuwa rahisi kuzungumzia timu kama Tambaza, Ashanti, Temeke Squad, Bora na Cargo.

Walipomaliza ligi ya mkoa, tulifuatilia timu ambazo itakutana nazo katika kanda na zipi zinaweza kuwa kikwazo. Na hadi tulipokua, bado tuliendelea kufuatilia ukuaji wa timu, ambayo baadaye ilikuja kuzaa nyota kama Abubakar “Sure Boy” Salum, Gregory Luanda, Mohamed Chopa, Abdul Ntila na wengine.

Ndivyo ilivyokuwa kwa vijana wengine wa wilaya za Tanzania. Wachezaji nyota wa wilaya hadi mkoa walijulikana kwa kuwa kulikuwa na ligi zenye ushindani wa hali ya juu na mvuto wa aina yake.

Leo hii, husikii hata ligi ya mkoa inanza lini na kumalizika lini. Husikii hata kiongozi wa Chama cha Soka Ilala, Temeke, au Kinondoni wakizungumzia maandalizi ya ligi za wilaya zao au hatua za mwisho za kupata bingwa.

Na baada ya hapo husikii viongozi wa Chama cha Soka cha Dar es salaam wakizungumzia hatua zinazofuata. Mara ya mwisho nilisikia wakizungumzia Ndondo Cup.

Ndio, najua kuna ligi ya mabingwa wa mikoa. Hawa wanapatikanaje bila ya taarifa za ushindani wao kujulikana?

Ndio maana hata zile timu zenye historia katika soka la nchi hii, hazijibidiishi kutafuta nafasi ya kurudi ligi ya juu. Zinachofanya ni kuangaliaangalia kuna timu gani imepanda kugikia Ligi Daraja la Kwanza au Championship ili zizinue na baadaye kubadilisha jina kurudia lile maarufu.

Ndivyo klabu kongwe kama za Pan Africans, Cosmopolitan na Pamba zinavyohangaika kurudi Ligi Kuu, lakini inakuwa ngumu kwa kuwa timu inakuwa haijakua pamoja au ya kuungaunga na matokeo yake kuendelea kuwa chini.

Hizi ligi za wilaya ndio msingi wa mpira wetu na ndiko ambako vijana wadogo wanaweza kuanza kupata nafasi ya kujifunza ushindani na ndiko ambako mashabiki wanaweza kuanza kujenga mapenzi na uzalendo kuliko hivi sasa watu wanakutana na timu katika ligi ya juu na wala hawajui imetoka wapi. Haina mizizi.

Ni ajabu sana unaposikia kiongozi wa mkoa akizungumzia kuweka nguvu kuhakikisha mkoa unapandisha timu hadi Ligi Kuu.

Hiyo si kazi ya chama cha mkoa. Ni kazi ya viongozi wa klabu. Wajibu wa viongozi wa mkoa ni kuhakikisha wanakuwa na ligi bora inayovutia mashabiki na hata wadhamini.

Fikiria DRFA ingekuwa na ligi imara ya mkoa ingekuwaje. Si ajabu ingegombania wadhamini na Ligi Kuu kwa kuwa kila kitu kipo Dar es salaam.

Lakini wilaya zake zinaingia kwenye mashindano kama mikoa na hivyo DRFA kuendelea kuelea juu juu bila ya mashindano yoyote makubwa.

Kazi ya viongozi wa mikoa sasa imekuwa ni kuidhinisha mashindano ya mchangani kama ya diwani, mbunge au ya mitaa. Wakimaliza hayo, wanasubiri mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF) na kazi kubwa zaidi ni pale uchaguzi unapokaribia wanapogeuzwa wafalme kwa ajili ya kura zao.

Tunahitaji ligi bora katika ngazi za wilaya na mkoa ili kutoa nafasi zaidi kwa vijana wetu kuandaliwa kiushindani, kujenga mapenzi ya mchezo na klabu kwa mashabiki, kukaribisha wadhamini na mambo mengine muhimu.

Tusiporudisha umuhimu wa ligi za wilaya na mkoa, tutakuwa tunasubiri miujiza kama ya kina Mbwana Samatta, Novatus, Simon Msuva na wengine ambao wameibukia katika ligi za Ulaya na kaskazini mwa Afrika kwa njia ambazo wengi tunashangaa, ingawa wachache wanaojua Simba na Yanga zimetupumbaza wanaweza kujivuna kuwa wao ndio siri ya mafanikio ya nyota hao.

Kwa nini tuwe na viwanja kama Bandari, Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Kifa, Mabatini na Msasani lakini hatuna ligi yoyote muhimu? Nani ataona umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya soka kama hakuna mahitaji?

Ingawa vyama vya mikoa ni huru baada ya kuondolewa FAT, bado TFF ina wajibu wa kuangalia kwa makini na kufuatilia maendeleo ya soka katika ngazi ya wilaya.

Naelewa kuwa moja ya wajibu wa wajumbe wa mkutano mkuu kutoka mikoani ni kuwasilisha ripoti zao za utendaji za mwaka.

Hizi huwa zina ripoti gani kama si uendeshaji wa mpira katika ngazi ya wilaya na mkoa?

TFF ina wajibu wa kujua huko wilayani na mikoani kunaendelea nini kinachoweza kusaidia kukua kwa mpira wetu kwa jumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live