Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwako Pilato wa Dabi ya Kariakoo

Kayoko Nondo M Pc Kwako Pilato wa Dabi ya Kariakoo

Sat, 4 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu zenye kiwango bora zaidi kwa Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kipindi cha misimu saba sasa, ni Simba na Yanga.Simba imesumbua kwa muda mrefu, hasa kimataifa, wamekuwa wawakilishi wazuri wa Tanzania na Afrika Mashariki yote.

Mwendo wa Simba, umefanya soka la Tanzania taratibu kupata heshima kubwa kimataifa na ile heshima waliyowahi kuwa nayo Ethiopia au Sudan kwa muda mrefu, ikahamia Tanzania.

Imekwenda kuimarika zaidi msimu uliopita baada ya Yanga kufanya vizuri kimataifa. Yanga walikuwa wakiendelea kufanya vema nyumbani, lakini haikuwa hivyo kimataifa.

Msimu uliopita wakaamka na kusonga moja kwa moja hadi fainali ya Kombe la Shirikisho. Well and good, sasa Tanzania ina timu mbili kubwa.

Angalia, Simba iko katika 10 bora za ubora Caf, ni timu namba saba lakini wameshiriki African Football League, mashindano ghali zaidi kwa mara ya kwanza, rekodi imeandikwa.

Siku chache baadaye, unaiona Yanga iko katika tuzo za Caf ikiwania klabu bora ya Arika. Timu hizi mbili za Afrika Mashariki, ndio bora zaidi kwa wakati huu na zinapokutana ukanda wote wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla wanajua kuna jambo pale jijini Dar es Salaam kwa kuwa wakubwa wanakutana.

Sasa mechi inapokutanisha wakubwa kwa kiwango cha Simba na Yanga, hata kama ni mechi ya nyumbani, kuna mambo mengi ya kuzingatia.Kwanza ni kukumbuka hii ni moja ya Dabi bora tano barani Afrika kwa kilpindi hiki. Lakini inazikutanisha timu zilizo na ubora wa juu kabisa katika kipindi hiki.

Kwa msimu huu, tayari zimekutana mara moja na Simba wakafanikiwa kushinda kwa mikwaju ya penalti huku ikionekana ndani ya dakika 90 hakukuwa na mbabe aliyeweza kuziona nyavu za mwenzake.

Lazima kuna hali ya hofu, wasiwasi wa kupoteza, hamu ya kutaka kushinda na kadhalika. Lazima tukubaliane kuwa mwamuzi atakayechezesha mechi hii anapaswa kuwa na ubora wa juu kabisa.

Natuma salamu zangu kwa mwamuzi wa mchezo kuwa lazima ajue umuhimu wake mkubwa wa kutafsiri sheria 17 za soka katika mechi hiyo ambayo ndio tafsiri ya soka la Afrika Mashariki katika kipindi hiki.

Mwamuzi atakapokuwa makini, atakuwa sehemu ya kuufanya mchezo huo uwe katika nafasi bora ya kuzalisha kiwango bora cha uchezaji.

Wachezaji wakiona haki inatendeka, watawekeza nguvu yao kubwa kwenye mchezo husika na kuufanya uwe mchezo wenye ushindani mkubwa utakaotafsiri ubora sahihi wa Simba na Yanga.

Mechi hii haitaangaliwa Tanzania tu, ni ukanda wote wa Mashariki lakini Afrika nzima kwa ujumla na hii ni kutokana na mwendo mzuri wa Yanga na Simba katika michuano ya kimataifa.

Macho yatakuwa ni ya wengi, kwa maana si macho ya Watanzania pekee. Mwamuzi atakuwa na nafasi kubwa ya kuiongoza mechi hiyo iweze kutoa ubora wake.Mwamuzi akishindwa kuudhibiti mchezo, itakuwa chanzo cha madudu mengi na ikiwezekana kuonyesha si kile ambacho wengi wanakitarajia wanapokutana Yanga na Simba na zaidi ni kiwango.

Mwamuzi aliyeteuliwa kuuchezesha mchezo huo, maana yake anaaminika. Kuaminika kwake, ndilo jambo muhimu naye anapaswa kulichukulia hilo kwa uzito na kuutendea haki mchezo huo.

Katika mechi chache za Kariakoo Dabi hivi karibuni, hakika waamuzi wamekuwa wakijitahidi sana katika suala la uchezeshaji na ndio maana imekuwa vigumu sana kusikia suala la malalamiko.

Niwapongeze kwa hilo, lakini niwakumbushe kuwa kufanya kwao vizuri kumezidi kuzitangaza zaidi Simba na Yanga na mpira wa Tanzania na wanapaswa kuwa na mwendelezo katika hilo.

Mechi ya Dabi ya Kariakoo, inagusa sehemu nyingi sana katika suala la mpira nchini. Kukiwa na ubora wa mwamuzi na wasaidizi wake. Haki itaamuliwa na ubora wa kila mtu na hakutakuwa na malalamiko au kisingizio cha mwamuzi mbovu. NB: Picha haina uhusiano na makala haya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live