Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa tizi hili Kaizer hawaponi, Luis, Chama, Manula wapiga spesho

Tizi Pic Data Kwa tizi hili Kaizer hawaponi, Luis, Chama, Manula wapiga spesho

Sat, 22 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KAMA wanachofanya Simba mazoezini kikikubali Msauzi ana hali mbaya. Hali imebadilika kimkakati na umakini mkubwa umeongezeka ndani ya Simba kuelekea kwenye mechi dhidi ya Kaizer Chiefs.

Ndani ya kambi wachezaji wamekuwa muda mwingi wakijadiliana na kupeana mbinu kuhusiana na mchezo huo wa leo Jumamosi huku Kocha Didier Gomes akiwapa somo mmoja mmoja lengo likiwa na kupindua meza.

Mastaa wa Simba wamepania kuanzia kambini mpaka mazoezini kubadili matokeo ya mchezo huo na kusonga mbele na wamekuwa wakipeana mbinu na motisha kila mara. Kwenye mazoezi ndani ya MO Simba Arena umakini umekuwa ni mkubwa na Gomes amezidisha programu zake kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa.

Ametengeza programu za pamoja lakini pia za mmoja mmoja kwenye nafasi zote. Wakati mazoezi hayo yanapokuwa yakiendelea Gomes akiona mchezaji wake anafeli kufanya anavyotaka anasimamisha na kumfuata fasta kumuelekeza.

Kwenye mazoezini ya juzi jioni, mchezaji wa kwanza kupewa maelekezo mara nyingi alikuwa Luis Miquissone ambaye hakutakiwa kukosea kufunga, kutoa pasi na kushindwa kukaba pindi alipopoteza mpira.

Gomes hakuishia hapo alitenga muda mwingine kuongea na Miquissone akiwa na msaidizi wake Selemani Matola wote wakimpa maelekezo wakati wachezaji wengine wakiendelea na mazoezi.

Mwingine aliyepewa maelekezo kwa muda mrefu na kwa nyakati tofauti alikuwa beki wa kulia, Shomary Kapombe.

Wakati mwingine wakati wachezaji wakiendelea na mazoezi alimwita Kapombe na kuongea nae mpaka aliamua kuufanya mpira kuwa kiti kwa muda na kuukalia ili kumsisitiza vizuri zaidi ya alivyokuwa amesimama na ndipo beki huyo alipomuinua akimaanisha ameelewa.

Wakati mazoezi yakiendelea Gomes na Matola waliendelea kuwaelekeza wachezaji kama Clatous Chama, Joash Onyango, Chriss Mugalu, John Bocco, Pascal Wawa kwa ukaribu zaidi. Baada ya mazoezi hayo kumalizika, Gomes aliliambia Mwanaspoti alisema wakati huu mbali ya mazoezi ambayo anayatoa anahitaji kuongea na kila mchezaji binafsi ili kumueleza la kufanya kulingana na mahitaji ya nafasi yake ilivyo.

Alisema ili kupata matokeo ambayo yatakuwa bora kwa upande wao lazima wachezaji wanatakiwa kuwa sahihi katika kila kitendo kwa kuzuia na kushambulia.

“Nilichokuwa naongea na wachezaji hao ni kuwaelekeza pamoja na kuwandaa akili zao kufikiria mahitaji ya mechi na kuacha mambo mengine ambayo si muhimu kwetu,” alisema Gomes

“Ndio maana mbali ya kuongea na Miquissone, Kapombe nilikuwa nikifanya hivyo kwa wachezaji wengine wote ili kufanya kile ambacho nahitaji kutoka kwao,”alisisitiza na kuongeza kwamba hakuna kukata tamaa.

“Inatubidi kujitoa kwa moyo zaidi naamini hakuna kitakachoshindikana kwani hata mimi kilichotokea wikiendi iliyopita sikuelewa shida ni nini, maana mchezo huo ndio wa kwanza kufungwa idadi hiyo ya magori,”alisema Gomes.

Kwa upande wake Nahodha wa Simba John Bocco alisema; “Tumepoteza ugenini basi na sisi uwezo wa kutumia vyema uwanja wa nyumbani tunao, tutahakikisha tunapambana kupata matokeo kwa kuwa nia yetu na malengo ni kuhakikisha Simba inatinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa,”alisema Bocco ambaye ni staa wa zamani wa Azam.

Alisema kila mchezaji ana kiu ya mchezo huo na yaliyopita sio kwa mashabiki tu hata wao wachezaji waliumizwa na matokeo hayo. Naye Bernard Morrison alipoulizwa juu ya mchezo huo alijibu “Niko poa najipanga kwa ajili ya mechi jumamosi.”

MATIZI YENYEWE

Katika mazoezi ya juzi, yalianza saa 10;30 jioni lakini kocha wa makipa, Milton Nienov alifika saa 9:50 alasiri akiwa na makipa wake wote watatu walioanza mazoezi yao saa 10:00 jioni. Baada ya wachezaji wengine kuwasili waliingia katika mazoezi ya mbinu ambayo yalisimamiwa na Didier Gomes pamoja na msaidizi wake, Selemani Matola na kutumia dakika 32.

Gomes aliwagawa wachezaji wake katika makundi mawili la kwanza lilikuwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ Shomary Kapombe, Bernard Morrison, Joash Onyango na Chriss Mugalu, Taddeo Lwanga, Clatous Chama, Larry Bwalya, John Bocco, Pascal Wawa, Mzamiru Yassin na Luis Miquissone.

Kundi la pili walikuwepo, Ibrahim Ame, Kennedy Juma, Gadiel Michael, David Kameta, Said Ndemla, Ibrahim Ajibu, Miraji Athumani, Parfect Chikwende, Francis Kahata, Hassan Dilunga na Meddie Kagere

Gomes alitaka wachezaji wa kundi la kwanza, wanapokuwa na mpira kupasiana haraka na kufika katika lango la timu pinzani, kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao.

Baada ya hapo Gomes alitaka pindi walipopoteza kuutafuta mpira kwa nguvu zote na ndani ya muda mfupi kuupata jambo ambalo kuna wachezaji kama Wawa, Onyango, Taddeo na Mzamiru walikuwa wanawachezea rafu wenzao ili kuupata mpira na wala mazoezi hayakusimamishwa. Gomes hakutaka kumuona mchezaji yoyote katika kundi la kwanza anatembea, anapoteza mpira, anapiga pasi mbaya, anashindwa kukaba, anakosa bao pamoja na mambo mengine ya msingi alikuwa mkali kwa kuongea sauti ya juu huku akisimamisha zoezi na kwenda kumuelekeza mchezaji huyo jambo la kufanya kwa wakati huo.

Mwanaspoti lilipomuuliza Gomes, kuhusiana na umuhimu wa zoezi hilo, alisema hataki kuona mchezaji wake anafanya mzaha hata katika katika dakika zote 90, kwenye mechi ya Kaizer.

Gomes alisema zoezi hilo linaitwa ‘High pressing’ maana yake wanatakiwa kushambulia kwa haraka na hakuna mchezaji kukaa na mpira kwa muda mrefu lakini wakipoteza wanatakiwa kuutafuta kwa haraka na kwa nguvu.

Alisema wanapopoteza mpira wanatakiwa kuziba mianya yote ili wapinzani wasipate nafasi ya kuleta madhara langoni kwao lakini kuongeza umakini katika kutengeneza nafasi za kufunga mabao na zikipatikana zitumiwe vizuri.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz