Kama ulidhani Simba inaiogopa Al Ahly ya Misri sahau, kwani mastaa tisa wa kikosi hicho cha Msimbazi wanaijua vyema timu hiyo na wamepewa kazi maalum ya kumalizana nayo hapo Oktoba 20 kwenye Uwanja wa Mkapa katika uzinduzi wa michuano mipya ya Africa Football League (AFL).
Si unakumbuka kwamba Al Ahly walipokuja kwa Mkapa mara zote mbili zilizopita walikufa kwa kipigo cha bao 1-0 kila mechi msimu wa 2020/2021 na 2018/2019? Sasa kuna wanaume tisa hao wako pale Unyamani ambao wameshakula sahani moja sana tu na wababe hao wa Afrika na wamepewa rungu la kuhakikisha Al Ahly Kwa Mkapa hawatoki.
Mastaa hao wa Simba waliowahi kukutana na Al Ahly na kuwapelekea pumzi ya moto ni Aishi Manula, Mohamed Hussein, Shomary Kapombe, Kennedy Juma, Clatous Chama, John Bocco na Luis Miquissone, ambao walikutana nayo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa misimu miwili tofauti.
Kocha mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amethibitisha uwepo wa mastaa hao ni turufu muhimu kwenye mchezo huo na atawatumia kama silaha za kuimaliza Ahly lakini akasisitiza lengo lao ni kushinda na kuweka heshima.
“Wachezaji wetu wengi wana uzoefu na mechi za namna hii na hiyo ni faida kwa timu nzima.Tunaendelea na maandalizi ambapo lengo la kwanza ni kushinda tu,” alisema Robertinho ambaye rekodi zake ndani ya Simba zinambeba licha ya kelele za mashabiki na wadau kwamba timu haichezi soka la kuvutia.
Luis alirudi msimu huu akitokea Ahly ambayo ilimsajili mwaka 2021 baada ya kuitungua bonge la bao katika moja ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa unaambiwa jamaa amepania kuwaonyesha kwamba yeye ndiye yuleyule aliyewafunga wakati ule hadi wakamsajili.
Simba inajua kuutumia Uwanja wa Mkapa licha ya kwamba ugenini ilifungwa 5-0 na pia 1-0 katika misimu hiyo, hivyo Oktoba 20 Mnyama amesema ana jambo lake.
Sambamba na wakali hao saba, wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho, beki Che Malone na kiungo Fabrice Ngoma nao wanaijua vyema Ahly kwani waliwahi kukutana nayo kabla ya sasa.
Malone alikutana na Ahly mara mbili msimu uliopita wakati akiichezea Cotton Sports ya kwao Cameroon, kwani walipagwa kundi moja kwenye Ligi ya Mabingwa na Ahly kushinda mechi zote mbili kwa matokeo ya 4-0 na 3-0 na Malone alicheza dakika zote 180.
Upande wa Ngoma naye anaijua vyema Al Ahly kwani walikutana mwaka 2021 katika mechi ya Africa Super Cup, wakati kiungo huyo akiichezea Raja Casablanca na mechi hiyo Ngoma alicheza dakika zote 90 licha ya kwamba mwisho wa mchezo chama lake lilipoteza kwa matuta 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya mabao 1-1.
Uzoefu wa mastaa hao unaifanya Simba kutembea kifua mbele huku ikiamini watakuwa na faida kwenye mechi hiyo ngumu.
Kwa upande wa nyota wa zamani wa Simba, Dua Said alisema Simba haipaswi kuiogopa Ahly kwani inafungika na anaamini wachezaji waliopo kwa sasa wanaweza kufanya hivyo.
“Naipa Simba asilimia 90 itashinda kwakuwa iko nyumbani na imekuwa na rekodi nzuri kwenye Uwanja wa Mkapa, pia ina wachezaji wengi wenye uzoefu na mechi kubwa.
Hawapaswi kuingia kwa woga, wajiamini na kufuata vyema maelekezo ya benchi la ufundi na ushindi utapatikana,” alisema Dua.
Wakati maandalizi hayo yakiendelea, Mwanaspoti linajua wachezaji wa Simba walio katika timu zao za taifa tayari wameombewa ruhusa na kufika Oktoba 18 (siku mbili kabla ya mechi), watakuwa tayari wamejiunga na kikosi hicho.
Mastaa hao ni Clatous Chama (Zambia), Henock Inonga (DR Congo), Ally Salim, Israel Mwenda, Mzamiru Yassin na Kibu Denis (Tanzania).
Baada ya mechi hiyo ya Oktoba 20 kwa Mkapa, Oktoba 24, itapigwa mechi ya marudiano jijini Cairo, Misri na mshindi wa jumla atatinga hatua inayofuata ya robo fainali.
Timu nyingine sita zinazoshiriki michuano hiyo mipya ya pesa ni Petro de Luanda ya Angola, TP Mazembe (DR Congo), Enyimba (Nigeria), Wydad (Morocco), Mamelodi (Afrika Kusini) na Esperance ya Tunisia.