Si kawaida yangu kuandika kuhusu uzuri wa mchezaji mmojammoja katika safu hii, ingawa pia sio dhambi wala kosa la jinai kufanya hivyo. Lakini nimeamua kufanya hivyo kutokana na jinsi Pacome Zouzoua anavyofanya jitihada uwanjani kiasi cha kuwa mfano wa kuigwa, si tu na wachezaji wa klabu yake, bali wengine wote wanaofikiria kuwa nyota.
Ndio, Pacome kiungo mshambuliaji wa Yanga ambaye juhudi zake, mbinu, kupambana kwa dakika zote na uwezo wake mkubwa umeifanya Yanga inusurike kupata kipigo mara mbili na kuondoka uwanjani na pointi moja, hapa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kule Kumasi Ghana.
Pengine jina lake la utani ‘Zidane’ lilikaribisha mizaha na kebehi nyingi dhidi yake wakati alipotambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga mwanzoni mwa msimu huu. Ingawa uchezaji wake ni tofauti na Zinedine Zidane ‘Zizzou’, nyota wa Ufaransa, lakini mambo makubwa ambayo amekuwa akiyafanya yameanza kusababisha watu waanze kumkubali na kidogo kuanza kutaja jina la Zidane.
Ni mchezaji anayeonekana haamini kwamba mechi imeisha bila ya kusikia filimbi ya mwisho na anaona kuna uwezekano wa kupata matokeo mazuri wakati wowote.
Alifanya kazi kubwa wakati Yanga ilipocheza mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, lakini siku haikuwa nzuri kwa vigogo hao wa Tanzania baada ya kuondoka uwanjani na kipigo cha mabao 3-0.
Lakini jitihada zake zilizaa matunda katika mchezo wa pili dhidi ya watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri. Ahly walitangulia kufunga katika dakika ya mwisho ya mechi hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Katika hali ya kawaida ilionekana kama Yanga ameshakubali kipigo na kilichokuwa kikisubiriwa ni filimbi ya mwisho tu.
Pacome hakuwa anafikiria hivyo. Alichukua mpira kutoka katikati ya uwanja na kukimbia nao kuingia eneo la penalti. Ni kama vile Kennedy Musonda alielewa kilichokuwa akilini mwake, akaamua kukimbia kuelekea kwenye kona ya eneo la miguu sita. Na hapo ndipo Pacome alipoona haja ya kuwapeleka mabeki wa Ahly kwa Musonda na hali wakijiandaa kumzingira, Musonda alimtengea Pacome mpira na bila ya kusita alifyatua kombora lililojaa wavuni, kuwaacha Waarabu wakishangaa.
Imani yake kwamba mchezo haujaisha hadi filimbi ya mwisho ipulizwe ilionekana baada ya bao hilo. Badala ya kukimbilia kibendera kwenda kushangilia bao lake, Pacome alikwenda nyavuni kuchukua mpira na kuanza kukimbia nao kurudi katikati.
Wenzake walikuja kumpongeza, lakini alinyoosha njia kuelekea katikati, akiamini Yanga ingeweza kupata bao jingine. Tabia hii ya kujiamini kwa jinsi hiyo, huchanganya wachezaji wa timu pinzani na ikitokea kosa kidogo wanaweza kujikuta wakiruhusu bao bila ya kujua.
Na akili ya aina yake kuamini kuwa katika dakika tano za nyongeza siku ile, Yanga ingeweza kufunga bao jingine na kumaliza mechi kwa ushindi, lakini hiyo haikuwezekana na zawadi ya juhudi na imani yake iliisha kwa kupata pointi moja nyumbani.
Mechi ya tatu pia ilikuwa ngumu kwa Yanga. Ikiwa imejaza wachezaji wengi vijana, Medeama iliwanyima nafasi Yanga kutumia vyema uwanja wa ugenini. Ililazimisha mashambulizi hadi ikajipatia bao kwa njia ya penalti. Lakini alikuwa ni Pacome tena aliyewaamsha mashabiki wa Yanga vitini.
Kiungo huyo wa Ivory Coast, ambaye ana uwezo mkubwa wa kukokota mpira, kwanza alinyang’anya mpira kutoka kwa mchezaji wa Medeama, kisha akakimbia nao kutoka karibu na mduara wa kati. Kadri mabeki wa Medeama walivyokuwa wakirudi nyuma kujaribu kuwabana wachezaji wa Yanga ambao wangeweza kupasiwa mpira, ndivyo Pacome alivyowasogelea akiamini hatimaye wataacha mwanya naye kufunga kirahisi. Na ndivyo ilivyokuwa. Alimchambua kipa kwa kiki ya mguu wa kushoto kuipa timu yake sare.
Mara zote unapomuangalia Pacome uwanjani, unamuona ni mchezaji anayejaribu kutumia stadi zake kuifungua ngome ya timu pinzani. Tofauti na viungo wengi wanaopenda kupiga pasi mshazari, Pacome hujaribu kupiga pasi zinazochana ngome, yaani kwa wachezaji waliotafuta nafasi katikati ambao wakifanikiwa kugeuka, hujitengenezea nafasi kubwa ya kufunga.
Pale mambo yanapoonekana kuwa magumu, Pacome hurudi nyuma na kusaidia kuzuia. Pindi anapopata nafasi huweza kukimbia na mpira umbali mrefu kutoka langoni mwake kuanzisha shambulizi la kushtukiza. Na mara nyingi mbinu hiyo imekuwa ikiifanya Yanga ipate nafasi na wakati mwingine kufunga, kama alivyofanya katika mechi dhidi ya Simba aliposababisha bao la kwanza.
Si mchezaji anayeonyesha kuchoka mapema na kumshawishi kocha ambadilishe. Mara nyingi huonyesha bado ana nguvu za kupambana, hivyo kumshawishi kocha amtafutie watu wa kusaidia kufanikisha jitihada zake. Si ajabu kwamba aliondoka Ivory Coast akiwa mchezaji bora wa msimu.
Tunahitaji kuzalisha wachezaji wa aina hii. Wenye kuutaka mchezo wakati wote, wenye kuthubutu kutumia stadi tofauti ambazo wamejifunza au wamezaliwa nazo na wasiokubali kushindwa hadi filimbi ya mwisho ipulizwe.
Si rahisi kuzalisha wachezaji wengi wa aina yake, lakini ukikuza watoto 20 kwa kuwafundisha mambo yote ya msingi ya soka na stadi tofauti, huwezi kukosa Pacome mmoja. Tatizo ni kwamba nani atawakuza? Nani mwenye jicho la kumuona Pacome katika umri mdogo?
Ukiona kijana anafanana stadi na Pacome hapa kwetu, ujue huyo anakaribia kustaafu. Ameshacheza sana mpira lakini umbile lake linaonyesha kuwa bado ni mdogo, kumbe anakaribia kustaafu.
Utambuzi wa vipaji vya watoto ni tatizo kubwa kwa makocha wetu. Wanapoambiwa waandae timu za watoto au vijana, huwaza ushindi kwanza na akili hiyo ya ushindi huwafanya wasichukue watoto au vijana ambao hawajapikwa vizuri na badala yake huchukua wazee wenye umri mdogo wa kimpira. Matokeo yake, hao wazee wenye umri wa vijana huwa hawadumu sana kwa kuwa huanza kusumbuliwa na majeraha yanayochelewa kupona, kitu ambacho ni dalili za uzee.
Lakini hatujachelewa. Tunahitaji kujenga utamaduni mpya wa kupika watoto ili kati yao wapatikane kina Prince Dube, Pacome, Clatous Chama na wengine na huko mbele tutumie rasilimali zetu humuhumu badala ya kukimbilia Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Congo DR kutafuta wachezaji.
Pamoja na kwamba bado hatujachelewa, kwa sasa nimsifu na kumpongeza Pacome kwa kuwa ndiye tunayemuona akijitofautisha na wenzake wengi uwanjani. Si tu kwa ustadi, bali akili na imani yake wakati wote wa mchezo. Yaani kwake haijaisha hadi iishe!