Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa refa huyu Yanga ishindwe yenyewe

Bouh Kwa refa huyu Yanga ishindwe yenyewe

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Abdel Aziz Mohamed Bouh kutoka Mauritania, ndiye refa aliyepangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Yanga na Al Ahly itakayochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Yanga imekuwa na historia nzuri na refa huyo kwani ndiye alichezesha mechi kati yao na TP Mazembe ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, ushindi ambao uliweka hai matumaini yao ya kusonga mbele kwenye kundi lake.

Kama Yanga ingepoteza mechi hiyo dhidi ya TP Mazembe ambayo ilichezeshwa na Bouh, ingejiweka katka mazingira magumu ya kusonga mbele kwenye kundi lake kwani ilipata ushindi huo ikiwa imetoka kupoteza mbele ya Monastir ya Tunisia kwa mabao 2-0, katika mchezo ambao ilianzia ugenini.

Refa huyo mwenye umri wa miaka 31, alipewa beji ya uamuzi ya kimataifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) mwaka 2019 na tangu hapo amechezesha mechi 11 za mashindano ya klabu Afrika kuanzia mwaka 2020.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa timu za nyumbani zimekuwa na bahati na refa Bouh kwani katika mechi hizo 11 alizochezesha, ni michezo miwili tu ambayo wageni walipata ushindi huku wenyeji wakiibuka na ushindi mara saba mechi mbili zilimalizika kwa sare.

Ni refa ambaye amekuwa na bahati ya mabao kufungwa katika mechi anazochezesha kwani katika mechi hizo 11 alizoshika filimbi katika mashindano ya klabu Afrika, ni mchezo mmoja tu ambao ulimalizika kwa sare tasa.

Mechi 10 zilizosalia, zilikuwa na idadi ya mabao 33 ikiwa ni wastani wa mabao 3.3 kwa mchezo na michezo miwili tu kati ya hiyo ambayo nao moja lilipatikana katika kila mchezo huku mingine iliyosalia yakifungwa mabao mawili au zaidi kwa kila mechi.

Lakini sio tu Yanga bali hata Al Ahly nao imekuwa na bahati narefa huyo kwani imekutana naye mara moja na katika mechi hiyo, iliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad.

Mchezo wa hivi karibuni ambao refa Bouh alisimama katikati kabla ya huo wa Yanga ni ule ambao Pyramids FC iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya APR ya Rwanda katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa suala la refa hawalipi kipaumbele na badala yake wanajiandaa ili kuwa bora uwanjani waweze kupata matokeo mazuri.

"Kwa sasa tunachoendelea nacho ni maandalizi ya mchezo huu ambao ni muhimu zaidi kwetu kuibuka na ushindi ili tuweze kufanya vizuri. Ni mechi ngumu ambayo tunapaswa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha tunapata matokeo mazuri," alisema Gamondi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: