Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa nini umchukie Robertinho?

Robertinho Dubai 1 Kwa nini umchukie Robertinho?

Wed, 11 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Inabidi kumpenda tu. Kocha wa Simba Robertinho hakwepeki. Hakimbiliki. Hanuniwi. Ni Kocha ambaye ukienda uwanjani unaweza kumtukana, lakini ukirudi tufanye mahesabu ataibuka bingwa. Robertinho ni mtu aliyepo mtegoni.

Watu wengi wanatamani ajikwae ili wapate sababu ya kumtimua. Simba ilifika robo fainali msimu uliopita kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na Robertinho.

Bahati mbaya kwa mashabiki wa Simba robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika  Afrika kwao wanaona sio hatua kubwa. Wamezoea kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika. Wamezoea robo fainali. Hakuna mpya tena. Hawaoni kama ni hatua kubwa tena kwako. Wamezoea. Wanaijua sana timu yao. Wanawajua sana watani zao - Yanga.

Simba hawana amani wakiwaona watani wanafika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Bado inawauma. Huwa sijui ni kwanini Simba wanajiona wakubwa kama Al Ahly. Mashabiki wao sio tu wanataka ubingwa, bali wanataka kuona na mpira mkubwa ukipigwa. Watu  wanataka kuona pira biriani na mataji. Sema Robertinho amewashika pabaya. Ni ngumu sana kumkataa. Robertinho hakimbiliki.

Unahitaji roho kama ya mwendawazimu kumfukuza kazi Robertinho. Tayari ameiongoza Simba kwenye mechi 16 za Ligi Kuu Bara na kushinda mechi 14. Sare ni mbili tu alizotoka na hakuna mechi aliyopoteza tangu afike. Hakuna kocha yeyote nchini anayezipita hizo rekodi zake tangu achukue jukumu la kuiongoza Simba.

Aliikuta timu imefika hatua ya makundi msimu uliopita, lakini akaipeleka robo fainali. Kwa mashabiki wengi ni kuona Simba ilipiga hatua kubwa zaidi ambazo Yanga hawajawahi kuzipata. Hapo ndipo shida yetu ilipo.

Siku mashabiki wa Simba wakiitazama timu yao tu bila kuihusisha Yanga watamheshimu sana Robertinho. Kushinda mechi 14 kati ya 16 za Ligi Kuu sio jambo dogo.

Amekuwa na msimu mpya ambao wana Simba walikuwa na matumaini makubwa sana na timu yao, lakini kwa namna walivyofuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kumewatia wasiwasi mkubwa.

Hawajazoea kuiona timu yao inakwenda kwa kuungaunga namna hiyo. Hawajazoea kuiona timu inakwenda kwa kubahatisha namna hii. Lakini haiondoi ukweli kuwa Robertinho anafanya kazi nzuri sana mpaka sasa. Ni masta kwelikweli. Gari linaonekana kama linachanganya.

Kuna wachezaji tayari naona wameanza kurudi kwenye ubora wao. Namuona Saido Ntibanzonkiza amerejea kwenye ubora wake. Tayari mabao yameanza kumtii. Mechi dhidi ya Tanzania Prisons alitupia kambani. Mechi dhidi ya Singida Fountain Gate tena akafunga. Huyu ndiye Saido mfungaji bora wa ligi yetu msimu uliopita.

Namuona Clatous Chama akianzia pale alipomalizia msimu uliopita. Chama kaanza msimu huu akiwa kwenye ubora wake. Mabao mawili ugenini dhidi ya Power Dynamos yanaonyesha ubora wa Mwamba wa Lusaka.

Mpaka sasa kama unaniuliza usajili bora wa Simba msimu huu, Che Malone ndilo jina linalokuja kwa haraka. Jamaa hana muda. Yuko bize na ukuta wake. Ni mtu wa kazi hasa. Beki anayejiamini. Msela. Na kamanda kwelikweli. Nadhani Simba wamelamba dume kwenye usajili wa beki huyu. Unaweza usiuone mpira mwingi Simba inapocheza lakini takwimu zinambeba sana kocha.

Hata kama humpendi Robertinho namba ziko upande wake. Takwimu zinambeba sana. Kumfukuza kazi inataka mtu mwenye akili kama za mwendawazimu. Ni ngumu sana kumuondoa. Kashinda taji la Ngao ya Jamii. Kaizuia Yanga kwenye fainali. Kafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Inaongoza ligi. Unaanzia wapi kumfuta kazi mtu kama huyu? Hakuna.

Namuona Kibu Dennis ni kama ameanza kuwa na U-Ronaldinho flani hivi chini ya Robertinho. Nimeona dhidi ya Singida na Tanzania Prisons aliyeupiga mwiga. Ni Kibu ambaye taratibu anaanza kuingia sasa kwenye mioyo ya mashabiki wa Simba.

Ndiye mchezaji mpambanaji zaidi mzawa akifuatana na Mzamiru Yassin. Hata kama humpendi Kibu ukweli ni kwamba anaupiga mwingi sana.

Willy Onana hayupo benchi kwa bahati mbaya. Ana kazi kubwa ya kufanya. Simba aliyoikuta inaonekana ni kama wachezaji wale wote waliokuwa msimu uliopita wamerejea kwenye ubora wao. Ni kama msimu unataka kuanza upya.

Kuna maeneo mawili tu ambayo Ronertinho bado anateseka. Ni eneo la kipa na la ushambuliaji. Kuamini kuwa John Bocco atarejea kwenye ubora wake ni kujidanganya.

Bocco ni lejendari pale Simba. Ameshamaliza kila kitu. Anapaswa kuja kwenye mechi za kimkakati. Anapaswa kucheza kwenye mechi maalumu. Sio mchezaji tena wa mechi za kila wikiendi.

Robertinho ni lazima arudi kwa Jean Baleke na Moses Phiri. Hawa ndiyo washambuliaji wa kuibeba Simba msimu huu. Hakuna namna nyingine labda asubiri dirisha dogo. Kumtaka Bocco awe na kiwango kama yule wa miaka mitano ya nyuma ni kujidanganya.

Bocco apewe mechi zake za kimkakati. Apewe dakika zake uwanjani. Sio mchezaji tena wa kumtegemea aibebe timu. Ni kweli anaweza kufunga, lakini hakupi uhakika. Ukienda uwanjani huenda hautaridhika na kiwango cha Simba kwa asilimia mia moja, lakini kwenye takwimu huwezi kumuondoa Robertinho.

Chanzo: Mwanaspoti