Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa nini thamani ya Mao inapanda?

Himid Mao Mkami Kwa nini thamani ya Mao inapanda?

Wed, 3 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Thamani ya kiungo wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na Gaish ya nchini Misri imezidi kupanda mara mbili zaidi ya misimu minne aliyocheza nchini humo kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarkt.

Transfermarkt ni nini? ni mtandao wa Kijerumani ambao umekuwa ukichakata takwimu za wachezaji mbalimbali na kufanya makadirio ya thamani zao.

Mao amejiunga na Gaish Julai 22 mwaka jana akipanda thamani zaidi baada ya usajili wake kupanda kutoka Sh400 milioni hadi bilioni 1.1.

Alijiunga na timu hiyo baada ya kuitumikia El Mahalla kwa misimu miwili kuanzia Septemba 30, 2021 hadi Julai 22, 2023 akiwa na thamani ya Sh400 milioni.

Kiungo huyo ambaye alianza kuichezea Petrojet Julai mosi 2018 ambayo alijiunga nayo akitokea Azam FC akiwa mchezaji huru baada ya kuondoka timu yake ya zamani akiwa amemaliza mkataba.

Ndani ya kikosi sa Petrojet alihudumu kwa mkataba wa miaka miwili msimu wake wa kwada dau la usajili halikuwekwa wazi lakini msimu uliofuata thamani yake ilikuwa inakadiriwa kuwa Sh556 milioni baada ya hapo timu ilishuka daraja na kuamua kutimka.

Thamani yake haikubadilika hii ni baada ya kutimkia Enppi kwa dau la Sh556 milioni ambapo pia hakuhudumi kwa muda baada ya timu hiyo kushuka akatimka zake.

Julai 30, 2022 alitoka Enppi SC alijiunga na El-Entage El-Harby ambayo ameichezea kwa mkataba wa mwaka kuanzia Januari 30 hadi Septemba 30 na baadaye kujiunga na El Mahalla ambayo ilimchukua kwa dau la chini Sh400 milioni.

Licha ya thamani yake kuonekana kushuka alifanya makubwa ndani ya timu hiyo akicheza kwa asilimia kubwa kwenye mechi zote za msimu kitu ambacho kilimpandisha thamani.

Pamoja na timu yake kushindwa kucheza ligi msimu uliofuata aliamua kuondoka ndani ya kikosi hicho na kutimkia Gaish ambayo anaitumikia hadi sasa kwa thamani ya billioni 1.1.

Hivyo kiungo huyo ndani ya misimu yake mitano nchini Misri amefanikiwa kuvuna mamillion ya fedha ambayo yanaendesha maisha yake ya nje ya uwanja hadi sasa.

MWENYEWE AFUNGUKA Akizungumzia thamani yake kupanda anasema kujituma na kupambana akiamini kila kitu kinawezekana na ndio siri kubwa ya mafanikio ndani ya nchi hiyo.

“Huwezi kupanda thamani kama uwezo wako unaporomoka msimu hadi msimu. Naamini ili uwe bora sokoni unahitajika kuwa na uwezo mzuri uwanjani na kuzishawishi timu pinzani,” anasema.

“Licha ya kucheza timu ambazo zinashindwa kuendelea kucheza ligi msimu unaofuata, lakini nazishawishi timu kutamani kuwa na mimi kwenye vikosi vyao.

“Hii inatokana na namna ninavyotumia fursa ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza kwenye kila timu niliyopata nafasi ya kucheza na nimekuwa nikicheza kwa ubora.”

Kiungo huyo mkatabaji ambaye pia ana uwezo wa kucheza kama beki wa kati au wa pembeni (namba 2), amepanga kutumia vyema fursa aliyopata ya kucheza Ligi Kuu Misri kuwa daraja la kumvusha kwenda Ulaya.

Staa huyo ambaye kiwango chake kinazidi kukua na kuendelea kujihakikishia nafasi ndani ya kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ameliambia Mwanaspoti; “Hakuna mabadiliko makubwa maisha ni yaleyale kinachobadilika ni timu tu, lakini maisha nafikiri hayana mabadiliko kwani timu nyingi za Misri vipato vyao vinafanana,” anasema.

“Timu zote nilizocheza nilikuwa napewa kila kitu nyumba ya kuishi na gari la kutembelea kutokana na kutokuwa na camp (kambi), hivyo gari ni muhimu kwa ajili ya kuendea mazoezini.”

Mao anasema anachofurahia sasa akiwa nchini humo ni kuzoea maisha ya huko kwani mwanzo alikuwa anapata changamoto ya lugha, lakini sasa amekielewa Kiarabu.

“Mbali na hilo pia suala la joto licha ya nilipotoka kuwa na joto huku ilikuwa zaidi sasa nimeshazoea na nimekuwa kama mwenyeji kutokana na kucheza sehemu moja kwa muda mrefu,” anasema.

Himid anayesifika kucheza kibabe, alianza kucheza soka ngazi ya chini ya timu ya vijana Azam Academy, iliyotwaa ubingwa wa mashindano ya vijana Uhai Cup mara mbili mfululizo.

Pia ametoa mchango kwenye makombe mengine ya Azam FC, kama vile Kombe la Ujirani Mwema mwaka 2012 nchini Congo DRC, Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014, walilotwaa bila kufungwa.

Himid ambaye ni nahodha msaidizi wa Taifa Stars, amepitia timu zote za vijana za Tanzania za miaka chini ya 17, 20 na 23 akiwa mmoja wa wachezaji tegemeo na hadi sasa ana nafasi yake kikosi cha Taifa Stars.

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo raia wa Brazil, ndiye aliyemuibua Himid katika Kituo cha Kukuza Vipaji cha TSA na kumjumuisha mara kadhaa katika kikosi cha wakubwa kupata uzoefu. Himid ni wa mtoto wa kwanza kuzaliwa kati ya watano akiwa na ndugu zake Femina, Rozmana, Feisal na Rahim.

Elimu yake ya msingi alipata katika Shule ya Msingi Kiwandani, Turiani, Morogoro darasa la kwanza na la pili na kuhamia Karume ya Dar es Salaam aliposoma hadi darasa la sita.

Mchezaji huyo alihama na kumalizia elimu ya msingi Shule ya Msingi ya Dk. Omary Ali Juma iliyopo Magomeni, Dar es Salaam kabla ya

kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tabata ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 2011. Staa huyo ni miongoni mwa wachezaji waliowekeza zaidi nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live