Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa nini ni Try Again na Mangungu?

Mangungu Try Again(1) Kwa nini ni Try Again na Mangungu?

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tangu Simba inyooshwe mabao 5-1 na watani wao, Yanga mambo bado hayajatulia kabisa kwa Wekundu wa Msimbazi.

Simba ilikumbana na kipigo hicho cha aibu cha kwanza katika Ligi Kuu Bara kutoka kwa watani wao hao, tangu mwaka 1968 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, siku ya Novemba 5, huku mabao yote matano yakiwekwa kimiani na nyota wa kigeni.

Mzambia Kennedy Musonda aliitanguliza Yanga kwa bao la kwanza kabla ya Kibu Denis kuisawazishia Simba na timu kwenda mapumziko matokeo yakiwa ni sare ya 1-1 kabla ya kipindi cha pili mambo kuiharibikia Simba kwa kuongezwa mabao kupitia Maxi Nzengeli aliyefunga mawili, huku Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua kila mmoja akifunga bao moja moja na kuhitimisha karamu ya mabao kwa siku hiyo.

Tangu mechi hiyo ilipomalizika kwa mabosi wa Simba kumfuta kazi Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ a.k.a Beto na wasaidizi wake wawili, Corneille Hategekimana na Ouamane Sallemi, kumekuwa na mjadala mzito kuanzia kutoka kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba.

Kila mmmoja amekuwa anajiuliza kitu gani kimeiponza Simba hadi kufikia kupoteza mchezo huo dhidi ya mtani wake wa jadi kwa idadi kubwa kama hiyo ya mabao.

Tusidanganyane, tatizo hapa sio kupoteza mchezo, bali ni kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao, hilo ndilo tatizo linalowaumiza Wanasimba, kiasi cha kufikia hatua ya kuwataka baadhi ya viongozi wao wajiuzulu.

Wanachama wanaamini kipigo hicho kwao ni kama kashfa ambayo inatakiwa iondoke na baadhi ya viongozi ambao wameshindwa kuiongoza timu yao hadi kuiingiza kwenye aibu kubwa kama hiyo.

KWANINI MANGUNGU?

Wanachana na mashabiki wa Simba wanawataka Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu ajiuzulu. Unaweza kujiuliza kwanini Mangungu?

Bosi huyo aliye kwenye kipindi cha pili cha uongozi wake anaponzwa na kauli zake za mara kwa mara kwenye mikutano ya Simba.

Mangungu akiwa kwenye mikutano hiyo amekuwa akiwapa matumaini makubwa wanachama wa Simba kwamba timu yao sio ya kushindana na Yanga tena.

Amekuwa akisema Simba ni timu kubwa ambayo inaweza kushindana na timu kubwa kama vile Al Ahly, Wydad, Mamelodi Sundowns na Zamalek huku akitoa ahadi za kuifunga Yanga wakati wowote atakapokutana nayo.

Hilo ndio kosa lake la kwanza kubwa kwa kuwa wanachama na mashabiki wanazichukulia kauli hizo za kiongozi huyo kishujaa na kwenda kuwatambia wapinzani wao, lakini matokeo yanapokuja kuwa tofauti ndipo kinatokea kinachotokea sasa. Wanamtaka ajiuzulu kwa sababu ameshindwa kutekeleza kile alichowaahidi kwenye mikutano.

Hapa wanachama wanageuka kama watoto walioahidiwa kununuliwa pipi ya kijiti, muda wote wanalia hadi watimiziwe kile walichoahidiwa la sivyo hawatakuelewa hata kidogo.

USHIRIKIANO

Kingine kinachomponza Mangungu, yeye ndiye mwenyekiti wa wanachama wa Simba, lakini amekuwa akijitenga nao kwa muda mrefu. Mara nyingi amekuwa akionekana kwenye matawi ya wanachama hao pindi linapokuja suala la uchaguzi mkuu wa klabu hiyo.

Simba ina mila na tamaduni zake ambazo Mangungu anatakiwa kuzitambua na kuzifuata. Wanachama wa Simba wanataka kushirikishwa katika mambo yanayoihusu klabu katika mambo madogo na makubwa na mtu wa kumzungumza naye ni Mangungu lakini haonekani kwenye matawi na hatoi ushirikiano.

Ukiacha hilo kwa kuwa Mangungu anaingia kwenye Bodi ya Simba akiwawakilisha upande wa wanachama amekuwa akishindwa kuwasilisha vizuri kofia yake juu ya yale ambayo wanachama wanayaona hayaendi sawa.

Tuwe wa kweli licha ya Mangungu kushinda baada ya matokeo kutangazwa kundi kubwa la watu waliona kwamba kiongozi huyo hakustahili kushinda kwa hali ya namna ile ya wakati ule na kwa matokeo ya kushtua kama haya dhidi ya Yanga, lazima wanachama watakwenda kumuandama yule ambaye anawawakilisha.

KWANINI TRY AGAIN?

Pamoja na kwamba mfumo wa uongozi umebadilika ndani ya Simba na wanachama hawana nguvu upande wake kwa kuwa Mwenyekiti ya Bodi ya Simba, Salum Abdallah Muhene ‘Try Again’ anachaguliwa na Rais wa Heshima wa Simba, Mwekezaji Mohammed Dewji ‘MO’ lakini kuna sehemu kama kiongozi amezembea na kusababisha aibu kwa klabu ya Simba.

Popote anakapokuwa na vyovyote itakavyokuwa, Try Again hawezi kukwepa kuwajibika kutokana na kipigo hiki cha aibu kutoka kwa Mtani wa Jadi. Try Again amefeli kwenye mambo mengi hadi kuifikisha Simba hapa ilipo na kufungwa na Yanga mabao matano tangu ilipofungwa 5-0 mara ya mwisho Juni Mosi 1968.

USAJILI

Try Again amehusika kwenye usajili wa timu ya Simba kwa asilimia mia moja lakini ameshindwa kujua ni usajili wa aina gani ulitakiwa kufanyika ndani ya kikosi hicho ambacho kilikuwa katika mafanikio makubwa kwa kutinga robo fainali za mashindano ya CAF mara nne katika miaka mitano.

Try Again alipaswa kufahamu kwamba, kikosi cha Simba kilihitaji marekebisho makubwa ili kukabiliana na wapinzani wao katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika kila msimu.

Simba ilitakiwa kufumuliwa kwa kuachana na baadhi ya wachezaji. Inadaiwa Try Again aliukataa ushauri wa Kocha Mhispania, Pablo Franco aliyeandika katika ripoti yake aliyoiwasilisha kwa bodi, akiishauri kuwabakisha wachezaji watatu tu katika kikosi hicho kisha kusajili wachezaji 11 wapya wa kikosi cha kwanza.

Kocha Pablo pia, alipendekeza kuongezwa wachezaji wengine watano wa kikosi cha kwanza ambao wangekuwa na uwezo wa kucheza katika nafasi zaidi ya moja.

Katika usajili wa dirisha kubwa lililopita hakuna mwingine anayeweza kuwajibika kwenye Bodi ya Simba zaidi ya Try Again, Simba iliwaingiza wachezaji wengi wenye viwango vya kawaida, na kuwafanya makocha kurudi kuwategemea wachezaji wale wale ambao walikuwa wanajulikana kwamba wataingia msimu mpya wakiwa na uchovu kutokana na kutumika mara kwa mara msimu ulioisha.

Lakini katika usajili uliopita uliowaingia wachezaji 11 wapya tumeshuhudia wawili tu waliofanikiwa kuingia kikosi cha kwanza ambao ni beki, Che Malone Fondoh na kiungo, Fabrice Ngoma. Mbali na hao wawili wengine waliosajili kwenye dirisha la msimu huu ni pamoja na Willy Onana, Ayoub Lakred, Kramo Aubin, Luis Miquissone, Hussein Abel, Hussein Kazi, David Kameta ‘Duchu’, Khamis Abdallah na Shaaban Idd Chilunda.

Ukimtazama Ngoma kwa makini anavyocheza uwanjani unaona kabisa anatumika kama kiungo mkabaji kimakosa na anatumikia nafasi hiyo baada ya Simba kukosa mtu sahihi wa kucheza eneo hilo.

Hebu fikiri, licha ya kutumika kwa muda mrefu kwa nahodha msaidizi na beki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, bado Simba imeshindwa kusajili beki mwingine wa eneo hilo.

Haya yote yanaonyesha wazi changamoto nyingi za usajili uliopita jinsi ulivyoikwamisha Simba. Tayari kocha ameondoka je, nani awajibishwe kwenye matumizi yasiyoridhisha ya Sh3 bilioni za usajili alizotoa mwekezaji?

SHIDA NI NINI?

Pamoja na kudumu ndani ya Simba kwa takribani miaka 20, lakini inaonekana bado Try Again ana safari ndefu kidogo ya kuiongoza Simba. Wanachama wa Simba wanaumia zaidi wanapokumbuka kauli zake jinsi alivyokuwa akijinasibu kwenye usajili wa klabu hiyo kwa kuamini kuwa wamepata wachezaji bora kumbe bado kulikuwa na nyakati ngumu ambazo Simba inatakiwa kupitia.

Try Again alipokuwa akihudhuria mafunzo ya FIFA ilitegemewa na alionekana kama vile angekuja kuwa kiongozi wa mfano hapa nchini katika soka letu, lakini leo hii Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said anaonekana kuwa bora zaidi yake katika uongozi.

Hii yote inatokana na mafanikio anayoyapata Hersi pale Yanga, huku Simba ikiendelea kupiga ‘maktaimu’.

Hersi ameweza kuwaweka mbali baadhi ya vigogo wenye majina makubwa wa Yanga (ambao watu wengi walidhani Yanga isingeweza kusonga mbele bila ya wao).

Alichokifanya, Rais huyo wa Yanga hakuwatupa watu hao, bali aliwatengenezea nafasi katika klabu na yeye kuwa na mfumo wake wa uongozi ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Jangwani na Twiga Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Pia, Hersi ameweza kuchukua uamuzi mgumu katika kukijenga na kukiboresha kikosi cha Yanga hatua kwa hatua bila ya kuogopa jina la mchezaji.

Isingekuwa rahisi kwa timu kama Simba kuweza kuwaacha wachezaji wenye majina makubwa kama Said Ntibazokinza ‘Saido’, Mukoko Tonombe, Yannick Bangala na Djuma Shaban kama wangekuwa katika kikosi hicho cha Wekundu, lakini Hersi ameweza kuuma jongoo kwa meno.

Angalia jinsi alivyoweza kuziba kivuli cha Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kuwafanya mashabiki na Yanga kuanza kumsahau na kuona hakuna shida yoyote katika kikosi chao.

USHAURI

Pamoja na kwamba Hersi anaonekana kama mtu anayechukua uamuzi mgumu peke yake, lakini ndiye aina ya kiongozi anayetakiwa katika Simba ya sasa. Ni kama ilivyokuwa kwa marehemu Zacharia Hans Poppe ambaye alikuwa akijivika mabomu ili kuipigania timu kwa nguvu zake.

Bahati mbaya sana Try Again anazidiwa akili na Hersi kwenye kufanya usajili. Pia, Bodi ya Simba chini ya Try Again imewakataa wachezaji wengi sana ambao wangeweza kuwa msaada kwa klabu na kwenda kusajili wachezaji wa bei rahisi ambao hawana msaada kwa klabu.

IJIFUNZE KWA YANGA

Miaka minne iliyopita kauli hii ilikuwa kinyume chake, lakini kwa sasa inatakiwa kusimama kama ilivyo. Simba inatakiwa kujifunza kwa Yanga. Iachane na kusajili wachezaji wa bei rahisi. Ikubali kuwekeza na kununua wachezaji wenye uwezo wa kushindana na kuipa matokeo ndani ya uwanja.

KWANINI MO YUKO KIMYA?

Msimu wa 2017-18 Simba ilitolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) katika hatua ya 64 Bora na timu ya Daraja la Pili, Green Warriors ya Mwenge mjini Dar es Salaam, kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1, tena ikiwa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara.

Mara baada ya kutolewa, MO Dewji aliandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba kama angekuwa na nguvu angemuondoa Kocha Joseph Omog. Na siku inayofuata Omog aliondolewa.

Wengi wanafahamu maumivu ya kufungwa na mtani wa jadi tena mabao mengi kuliko kufungwa na Green Warriors, Je, Mo amechukua uamuzi gani katika kipindi hiki akiwa na nguvu ya kufanya uamuzi kwenye Bodi ya Simba?

Chanzo: Mwanaspoti