Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa mziki wa Wazawa Yanga inatoboa freshi tu

Dickson Job X Kibwana Shomari Kwa mziki wa Wazawa Yanga inatoboa freshi tu

Sat, 8 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa soka nchini wameanza kukaa mkao wa kula kila kona wakisikilizia na kuona nyota wapya wanaotambulishwa na timu wanazoshabikia, lakini wakati zoezi hilo likianza upande wa pili unaonyesha Yanga hadi sasa imefunika kwa kuwa na kikosi imara cha wazawa.

Kikosi hicho cha Yanga kinachoundwa na wachezaji wazawa kinaweza kuhimili ushindani wa mashindano mbalimbali msimu ujao bila kutegemea wale wa kigeni kulinganisha na Simba na Azam kutokana na kuwa majemba wa maana.

Uimara wa kikosi cha wachezaji wazawa wa Yanga unaonekana kutoupa kazi ngumu uongozi wa timu hiyo katika kusaka wachezaji wa ndani kulinganisha na Azam ambayo ina maeneo machache inayohitaji vyuma vya kizawa.

Kwa upande wa Simba ambayo inaonekana ina kibarua kigumu cha kusaka kundi kubwa la wazawa wenye ubora wanaoweza kuifanya timu hiyo iwe na kikosi imara cha wachezaji wa ndani wanaoweza kuipa matokeo mazuri bila kutegemea nyota wa kigeni.

Tathmini iliyofanywa na gazeti hili imebaini kuwa hadi sasa katika siku za mwanzo za dirisha la usajili, Yanga ina nyota 11 wazawa wanaoweza kutumika katika kikosi cha kwanza msimu ujao bila kulipa kazi kubwa benchi la ufundi, huku ikibakiwa na wakali wengine wanne kwenye benchi ambao wanaweza kuingia na kutoleta utofauti mkubwa.

MZIKI ULIVYO

Kwa mujibu wa wachezaji waliopo Jangwani kwa sasa, kikosi hicho cha wazawa cha Yanga kinaundwa na kipa Metacha Mnata, huku mabeki wa pembeni wakiwa ni Dickson Job na Kibwana Shomari huku mabeki wa kati wakiwa ni Bakar Mwamnyeto na Ibrahim Bacca.

Upande wa viungo kuna Jonas Mkude, Mudathir Yahya na Salum Abubakar 'Sure Boy', washambuliaji wakiwa ni Nickson Kibabage na Denis Nkane huku mshambuliaji wa kati akiwa ni Clement Mzize.

Kama haitoshi kwenye kikosi hicho benchini kitabakiwa na Abuutwalib Mshery, Farid Musa, Crispin Ngushi na Zawadi Mauya.

AZAM FC NAKO

Kwa upande wa Azam, yenyewe haijapishana sana na Yanga, japo kuna maendo ya kikosi hicho kinaweza kuipa presha zaidi hasa eneo la langoni, kwani italazimika kumtegemea kinda Zuberi Foba ambaye hana uzoefu wa kutosha.

Hata hivyo kwa maeneo mengine timu hiyo ina majembe ya maana wenye kiwango bora na uzoefu wa kutosha wa ndani.

Hadi sasa, kikosi cha wazawa cha Azam kinaweza kuundwa na Foba, akisaidiwa na mabeki wa pembeni ambao ni; Nathaniel Chilambo na Edward Charles Manyama, wakati Lusajo Mwaikenda na Abdallah Kheri 'Sebo' wakiwa katika nafasi ya beki wa kati.

Kwa upande wa eneo la viungo Azam ya Wazawa ina wakali kama Sospeter Bajana, Feisal Salum 'Fei Toto' na Yahya Zayd, huku washambuliaji kwa eneo la mbele likiundwa na Idd Selemani 'Nado' Abdul Suleiman 'Sopu' na Ayoub Lyanga.

Katika benchi la timu hiyo, wanasaliwa na Pascal Msindo, Cyprian Kachwele na Tepsi Evance ambao kama kocha anataamua kuwaingia uwanjani kuwasaidia wenzao, mambo yakawa bambamu.

JESHI LA SIMBA

Kitendo cha Simba kupunguza kundi kubwa la wachezaji katika dirisha hili, kinaifanya hadi sasa isiwe na kikosi tishio cha wazawa kutokana na nafasi nyingi uwanjani kutokuwepo kwa wazawa wanaoonekana wanaweza kuleta ushindani mkubwa kwa wageni.

Pia katika kikosi hicho cha Simba cha wazawa kuna maeneo italazimisha kuwatumia wachezaji wasio asilia wa kuzitumikia nafasi hizo, hasa kwa wale wachezaji viraka.

Ili kikosi cha wazawa cha Simba kitimie kwa mujibu wa wachezaji waliopo kwenye timu kwa sasa, wapo wachezaji watalazimika kupangwa katika nafasi ambazo wamekuwa hawazichezi mara kwa mara ili tu waweze kutimia 11 jambo ambalo mara nyingi makocha wamekuwa hawalipendelei.

Kikosi cha wazawa cha Simba kinaweza kuundwa na kipa Aishi Manula, akisaidiwa na mabeki wa pembeni ambao ni; Shomari Kapombe na Mohamed Hussein 'Tshabalala' wakati kwa beki ya kati watasimama Kennedy Juma na Nassor Kapama ambaye anamudui kucheza zaidi ya nafasi moja.

Kwenye eneo la kati Simba itawategemea viungo, Mzamiru Yassin na Jimmyson Mwanuke, huku mawinga wakiwa ni Kibu Denis na Mohamed Mussa, wakati washambuliaji wanaweza kusimama nahodha John Bocco na Habib Kyombo.

Katika benchi Simba inabakia na makipa wawili wazawa ambao ni Ally Salim na Feruzi Teru pamoja na beki wa kulia, Israel Mwenda.

WASIKIE WADAU

Kocha wa soka la wanawake, Edna Lema alisema kuwa kinachoisaidia Yanga ni kundi kubwa la wachezaji wake kucheza mara kwa mara kulinganisha na wachezaji wa timu nyingine ambao nafasi zao kwenye kikosi cha kwanza ilihusisha kundi la wachache.

"Yanga ina wachezaji bora wanaotumika kuliko Simba na Azam. Karibu nusu ya timu wanapata nafasi. Jambo la msingi ni hakuna ulazima wa kutumia nafasi 12 za wachezaji wa kigeni kwa sababu hakuna timu inayoweza kupatia katika kusajili wachezaji hao wote. Zinaweza kusajili wachezaji saba au nane na nyingine tukajaziwa wachezaji wadogo wazawa wanaoweza kukaa kwenye klabu kwa muda mrefu," alisema Lema, nyota wa zamani wa kimataifa aliyegeukia ukocha akizinoa timu za taifa za wanawake za Twiga Stars, Tanzanite na Serengeti Girls sambamba na Yanga Princess.

Nyota wa zamani wa Yanga, Ramadhani Kampira alisema kuwa Yanga imefanikiwa kwa wachezaji wazawa kwa sababu inawapa thamani.

"Kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikiwapa kipaumbele zaidi wachezaji wazawa na huwa hailazi damu pindi inapomuona mchezaji wa nyumbani anayeonyesha kiwango kizuri. Timu nyingine zinapaswa kujifunza katika hilo na kuwapa kipaumbele wachezaji wetu," alisema Kampira, winga aliyetamba miaka ya 1980 akisajiliwa kutoka Sifa United ya Manzese iliyowahi kuwatoa wakali kama Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio' na mdogo wake, Idd Seleman 'Meya' a.k.a Nyigu.

Vikosi vilivyo

YANGA

Metacha, Job, Kibwana, Mwamnyeto, Bacca, Mkude, Nkane, Sure Boy, Mzize, Mudathir na Kibabage.

Akiba: Mshery, Farid, Ngushi na Mauya

AZAM:

Foba, Chilambo, Manyama, Mwaikenda, Sebo, Bajana, Zayd, Fei Toto, Sopu, Lyanga na Nado.

Akiba: Msindo, Kachwele na Tepsi

SIMBA:

Manula, Kapombe, Tshabalala, Kennedy, Kapama, Mzamiru, Kibu, Mwanuke, Bocco, Kyombo na Mussa.

Akiba: Salim, Feruzi na Mwenda.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: