Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa mziki huu! Kipigwe tu, ubishi uishe

Baleke X Aziz Ki GOALS Kwa mziki huu! Kipigwe tu, ubishi uishe

Sun, 30 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-2023 ipo ukingoni. Imesaliwa na mechi za raundi zisizozidi nne kabla ya kufikia tamati Mei 28 mwaka huu, huku vita ya ubingwa ikisalia kwa vigogo Simba na Yanga.Yanga ipo katika nafasi kubwa ya kutetea tena taji kwa msimu wa pili mfululizo, kwani ikizichanga vyema karata zake katika michezo minne iliyosaliwa na kuvuna pointi nane tu, italitetea taji.

Timu hiyo ina yenye pointi 68, kama itavuna pointi hizo nane itaifanya ifikishe 76 ambazo haziwezi kufikiwa na watani wao, Simba yenye alama 63 kwa sasa na ikishinda mechi zote nne itafikisha 75 tu!

Lakini wakati ligi hiyo ikiwa mwishoni, kuna baadhi ya mastaa wa kigeni pamoja na wazawa katika mechi za raundi 27 wamekiwasha kiasi kwamba wanaweza kuunda vikosi vya kwanza na akiba na kama wataamua kukipiga uwanjani basi nyasi zitawaka moto.

Ndio, upande wa wageni wanaweza kuunda zaidi ya vikosi vitatu chini ya makocha Nasreddine Nabi na Roberto Oliveira 'Robertinho' na kuliamsha dude dhidi ya wazawa ambao wenyewe wanaweza kuunda idadi ya vikosi kama hivyo chini ya makocha, Fred Felix 'Minziro' na Mecky Maxime.

Hapa chini ni vikosi viwili vya timu za mapro wa kigeni na vile vya wazawa wanaoweza kuliamsha na kuwapa raha mashabiki watakaozishuhudia uwanjani na sababu ya kuwekwa kwenye vikosi vya timu hizo. Endelea nayo...!

CHAMA LA WAGENI

Diarra Djigui (Yanga)

Huu ni msimu wake wa pili kucheza Ligi Kuu Bara na amedhihirisha alistahili kutwaa tuzo ya Kipa Bora kwa msimu uliopita kwa kazi kubwa aliyoifanya akiisaidia Yanga kurejesha taji la Ligi Kuu Bara lililokuwa likishikiliwa kwa misimu minne mfululizo na Simba.

Diarra akishirikiana na makipa wenzake kikosi waliiwezesha Yanga kubeba taji la Ligi Kuu bila kupoteza mechi yoyote, huku nyavu za timu hiyo zikiguswa mara nane tu.

Kwa sasa anastahili kuingia kikosi cha kwanza cha mapro wa kigeni kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya akiwa ndiye kipa kinara wa clean sheet akiwa na 15, huku Yanga ikiongoza msimamo kwa kupoteza mechi mbili tu na nyavu zao kuguswa mara 13 tu, wakati ligi ikiwa inaelekea ukingoni.

Djuma Shaban (Yanga)

Wapo mabeki wengi wa kulia wakigeni wanaoweza kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha mapro wa kigeni, lakini Djuma Shaban anastahili kutokana na kazi kubwa anayoifanya Yanga katika Ligi Kuu.

Ingawa amekuwa akipokezana nafasi na mabeki wakizawa wa timu hiyo, lakini mziki wa beki huyo kutoka DR Congo unajulikana na kuonekana, kwani amekuwa msaada mkubwa katika ukuta wa timu hiyo na kuifanya iwe timu iliyoruhusu mabao machache hadi sasa.

Bruce Kangwa (Azam)

Beki wa kushoto mkongwe mwenye uwezo wa kucheza kama winga wa kushoto anaingia kwenye kikosi hiki kutokana na kuwa na muendelezo mzuri tangu atue Azam misimu minne iliyopita na kuendelea kuibeba timu hiyo inayoshika nafasi ya tatu kwa sasa katika msimamo wa ligi.

Licha ya kwamba Azam iliyoanza msimu kwa kasi kisha kuzimika katikati na kujiondoa kwenye mbio za ubingwa, lakini kazi kubwa ya nyota huyo wa kimataifa wa Zimbabwe, imeifanya Azam kuwa moja ya timu zenye ukuta mgumu, hasa upande wa pembeni ikiwa ni timu ya nne kwa kuruhusu mabao machache hadi sasa, nyuma ya Yanga, Simba na Singida Big Stars.

Biemes Carmo (Singida Big Stars)

Ingawa ni msimu wake wa kwanza kucheza soka la kulipwa nchini, lakini beki huyo wa kati Mkongoman ameonyesha alivyo imara kwenye kulilinda lango la Singida Big Stars akishirikiana na Pascal Wawa na mabeki wengine wa kati wa timu hiyo.

Carmo panga pangua katika kikosi cha Singida hakosekani na amekuwa nguzo imara iliyopifanya timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza kuwa tishio, ikiwa moja ya timu tatu bora zilizoruhusu mabao machache ikifungwa 20 tu, ikizidiwa na Yanga (13) na Simba (14).

Henock Inonga (Simba)

Beki huyu wa kati mwenye mabao matatu hadi sasa katika Ligi Kuu Bara na moja kwenye michuano ya kimataifa ya CAF anaingia kwenye kikosi hiki kutokana na umahiri wake wa kukaba na kuisaidia timu kupata mabao.

Inonga anayecheza msimu wa pili kwa sasa ndani ya Simba ni mmoja ya mabeki wa kati walio na uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi na kukaba washambuliaji wasumbufu, mbali na uwezo wa kufunga akitumia urefu alionao.

Huwezi kumuacha kwenye kikosi cha kwanza cha mapro wa kigeni kwa kazi kubwa aliyoifanya hadi sasa ndani ya Simba na kuwa mmoja na mabeki bora wa Ligi Kuu Bara.

James Akaminko (Azam FC)

Utasema nini kuhusu kiungo huyo mkata umeme kutoka Ghana? Akaminko ni mmoja wa viungo wakabaji wanaojua kutumia vipaji vyao katika kulifanya soka lionekane ni mchezo mwepesi.

Tangu atue Azam msimu huu kiungo huyo amekuwa mmoja ya nyota walioibeba timu hiyo kw aumahiri wake wa kukaba, kuituliza timu na kuitengenezea nafasi ya mabao kwani hadi sasa licha ya kufunga bao moja, lakini ameasisti mabao matano ya timu hiyo.

Bruno Gomes (Singida Big Stars)

Mabeki wa timu pinzani huwa hawana hamu ya kukutana na kiungo mshambuliaji huyo wa Kibrazili wa Singida Big Stars kutokana na kasi na uwezo mkubwa wa kulitembeza bolu na ufundi wa kupiga mipira ya friikikii.

Ndiye kinara wa mabao wa Singida inayoshika nafasi ya nne kwa sasa katika ligi hiyo, akiwa amefunga tisa, yaliyochangia kwa kiasi kikubwa pointi ilizonazo timu hiyo kwani kila mabao yasiyopungua nane aliyofunga yameipa timu hiyo pointi au ushindi, ikiwa na maana kati ya pointi 51 ilizonazo Singida, karibu nusu imechangiwa na nyota huyo.

Clatous Chama (Simba) Ni mmoja wa roho na nguzo ya Simba kutokana na kipaji kikubwa cha kuuchezea mpira akiwa mahiri kwa kutoa pasi na pia kufunga.

Chama aliyeitumikia timu hiyo kwa misimu minne, anaingia kwenye kikosi hiki cha kwanza cha mapro wa kigeni kutokana na uwezo mkubwa alionao wa kuiendesha timu na kutengeneza mabao yaliyoifanya Simba iwe ndio timu kinara yenye mabao mengi hadi sasa ikifunga 62.

Kiungo mshambuliaji huyo kutoka Zambia ndiye kinara wa kuasisti akiwa na 15, huku akifunga mabao matatu katika Ligi Kuu, mbali na kushika nafasi ya pili ya wafungaji wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na manne, timu hiyo ikiwa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Fiston Mayele (Yanga)

Utasema nini kuhusu kinara huyo wa mabao wa Ligi Kuu Bara kwa sasa? Mayele ndiye mtambo wa mabao wa Yanga kwa misimu miwili mfululizo anayoichezea timu hiyo, huku akiiibeba pia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa imetanguliza mguu hatua ya nusu fainali.

Mayele anajua kufunga. Anafunga mabao magumu, ambayo washambuliaji wengine wa kigeni na hata wazawa hawajawahi kuyafunga. Ana uwezo wa kumiliki mpira, kasi na kufunga kwa kutumia kichwa, miguu wote miwili, mbali na nguvu ya kupambana na mabeki wababe na hadi sasa amefunga mabao 16, yanayolingana na yale aliyofungwa msimu uliopita. Anaanza kikosi hiki cha kwanza kama straika namba moja, kwani vigezo vinambeba hadi sasa wakati ligi ikiwa inaelekea ukingoni.

Jean Baleke (Simba)

Hana muda mrefu tangu ajiunge na Simba katika usajili wa dirisha dogo, lakini moto aliouonyesha kwa sasa unamfanya straika huyo kutoka DR Congo kama ilivyo kwa Fiston Mayele kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha mapro wa kigeni.

Jamaa anajua kufunga. Ni mviziaji mkubwa, lakini ana uwezo wa kupiga chenga na kujipanga kwenye nafasi nzuri za kufunga mbali na kasi inayowatesa mabeki wa timu pinzani.

Hadi sasa, mwamba huyo ameshafunga mabao saba katika Ligi Kuu, mbali na mabao manne yaliyoiwezesha Simba kutinga robo fainali na ikisikilizia mechi ya mwisho dhidi ya Wydad Casablanca ili kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Anastahili kuingia kikosi hiki.

Prince Dube (Azam FC)

Licha ya kwamba hajawa kwenye kiwango bora kilichozoeleka wakati anatua Azam akitokea Zimbabwe, lakini Dube anastahili kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha mapro wa kigeni kutokana na uwezo mkubwa wa kutengeneza mashambulizi na pia kufunga.

Ni mmoja ya washambuliaji nyota wa Azam akiwa amefunga mabao sita hadi sasa na kuasisti mara tatu, huku akiwa mmoja ya mastaa wanaojua kuwapa kashkashi mabeki wa timu pinzani kwa uwezo wake wa kupiga chenga, kumiliki mpira na kasi, mbali na kufunga mabao kwenye engo ngumu.

Majeraha makubwa aliyoyapata msimu uliopita ndiyo yaliyompunguza kasi, lakini badpo mwamba huyo ni tishio na anaungana na wakali wengine kuunda kikosi cha kwanza cha mapro wa kigeni.

MAKOCHA: Nasreddine Nabi (Yanga) akisaidiana na Roberto Oliveira 'Robertinho' (Simba)

KIKOSI CHA AKIBA:

Jonathan Nahimana (Namungo), Nicholas Wadada (Ihefu), Joyce Lomalisa (Yanga), Joash Onyango (Simba), Yannick Bangala (Yanga), Khalid Aucho (Yanga), Kipre Junior (Azam), Saido Ntibazonkiza (Simba), Idris Mbombo (Azam), Stephane Aziz KI (Yanga) na Kennedy Musonda (Yanga)

CHAMA LA WAZAWA

Aishi Manula (Simba) Kipa Bora wa misimu minne mfululizo kati ya mitano iliyopita anaanza kwenye kikosi cha kwanza cha mapro wazawa kutokana na umahiri wake mkubwa wa kuilinda milingoti mitatu.

Manula ndiye kipa namba moja wa Simba na timu ya taifa na amekuwa hodari akiisaidia Simba kuwa timu iliyofungwa mabao machache katika ligi, lakini ikitinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, japo kwa sasa ni majeruhi.

Kwa makipa wazawa waliopo kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa, ni ngumu kumweka nje kwenye kikosi hiki cha mapro wazawa, kwani amewaacha mbali makipa wa timu nyingine hadi sasa akila sahani moja na Diarra wa Yanga kwa kuwa clean sheet nyingi akiwa na 12.

Shomary Kapombe (Simba)

Ni mmoja ya mabeki wa wakongwe wa pembeni wenye kasi na uwezo mkubwa wa kukaba na kuanzisha mashambulizi.

Kapombe anayeichezea Simba kwa msimu wa tano mfululizo sasa tangu aliposajiliwa kutoka Azam ni beki mwenye uwezo mkubwa akiitumikia pia timu ya taifa, Taifa Stars

Mbali na kukaba na kutengeneza mashambulizi, lakini ni mahiri kwa kuasisti akiwa na sita kwenye ligi, ukiacha asisti nyingine tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika akiiwezesha timu kunusu nusu fainali ya micuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu barani Afrika.

Mohammed Hussein 'Tshabalala' (Simba)

Mabeki wa kushoto wazawa wapo wa kutosha, lakini ni ngumu kumuacha nje, Tshabalala katika kikosi cha kwanza cha mapro wazawa kwa kazi kubwa anayopifanya Msimbazi kwa misimu zaidi ya mitano mfululizo ndani ya timu hiyo.

Tshabalala kama ilivyo kwa Kapombe amekuwa nguzo ya kutengeneza mashambulizi ya Simba, huku akikaba kiufundi na kuwanyima raha mawinga wakorofi wa timu pinzani na ni mmoja ya mabeki waliotengeneza ukuta mgumu kwa Simba kwa misimu yote aliyopo Msimbazi.

Mbali na kukaba na kushambulia, pia anafunga na kuasisti akiwa mmoja wa mabeki walioasisti mara nyingi kwenye ligi hiyo akimfukukia Kapombe.

Dickson Job (Yanga)

Mmoja ya mabeki wa kati wenye uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja uwanjani, akitumika pia kama beki wa kulia ndani ya Yanga na kutoa matokeo bora kwa timu hiyo.

Ni kweli wapo mabeki wengi wa kati wazoefu na mahiri wazawa, lakini ni ngumu kumuacha nje Job kwenye kikosi cha kwanza cha mapro wa kizawa kwa uwezo wake mkubwa wa kukaba, kutengeneza mashambulizi na hasa kuruka juu, licha ya kimo chake cha ufupi.

Ushirikiano wako na nahodha wake, Bakar Mwamnyeto ndani ya Yanga imeifanya timu hiyo kuwa na ukuta mgumu kupitika na ndio maana sio ajabu hadi sasa kuwa timi iliyoruhusu mabao machache (13) katika mechi 26 ilizokwishacheza msimu huu.

Bakar Mwamnyeto (Yanga)

Hakuanza msimu vizuri kutokana na matatizo ya kifamilia aliyokuwa nayo ikiwamo kupata misiba ya wapendwa wake, kiasi cha kumtoa kikosi cha kwanza cha Yanga kabla ya kukaa sawa na kurejea na moto mkali kwa sasa.

Nahodha huyo wa Yanga amekuwa mmoja ya nguzo imara ya ngome ya timu hiyo, akishirikiana na nyota wenzake kuifanya isipitike kirahisi kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na hata zile za kimataifa ikiwa imetinga robo fainali na ikitanguliza mguu mmoja kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.

Uwezo wake wa kukaba kwa akili na kutengeneza mashambulizi akisaidia pia kuasisti na kufunga kunamfanya aingie katika kikosi cha kwanza cha mapro wa kizawa.

Yusuf Kagoma (Singida Big Stars)

Kiungo fundi wa kukaba mwenye uwezo wa kushambulia aliyeanza msimu akiwa na Geita Gold kabla ya dirisha dogo kuhamia Singida anaingia kwenye kikosi hiki kwa umahiri wake.

Kagoma ana uwezo mkubwa kwa kukaba na kutengeneza mashambulizi mbali na kuituliza timu pale inapozidiwa na wapinzani, akiwa pia na uwezo wa kufunga mabao, japo hadi sasa ana bao moja, lakini ni mmoja ya nguzo imara ya Singida inayowania kumaliza Tatu Bora sambamba na Azam FC.

Ayoub Lyanga (Azam)

Hatajwi sana katikam kikosi cha Azam, lakini ni mmoja ya wachezaji walioibeba kwa kiwango kikubwa timu hiyo kwa kuhusika na mabao mengi ndani ya msimu huu, japo alianza akiwa majeruhi na kushindwa kuitumikia kwa ufanisi.

Lyanga amefunga mabao manne tu kwa sasa, lakini ameasisti mabao saba, huku akisaidiana na mastaa wengine wa timu hiyo kuifanya Azam iwe tishio, japo imeshaondoka kwenye mbio za ubingwa.

Ni mchezaji mwenye kasi, mwenye chenga na mjanja kuwatoka mabeki na kupiga krosi zenye macho ambazo zimekuwa zikiipa timu mabao, kwanini asiingine kwnye kikosi cha kwanza cha mapro wa kizawa?

Mzamiru Yasin (Simba)

Kiungo asiyechoka uwanjani, wenyewe wanapenda kumuita kiungo punda. Mzamiru japo haimbwi sana Msimbazi, lakini ni mmoja ya wachezaji mahiri na wenye mchango mkubwa ndani ya timu hiyo kwa msimu huu akifunga na kuasisti na akitengeneza ukuta mgumu wa timu hjiyo akishirikiana na nyota wengine akiwamo Sadio Kanoute na mabeki wa kati.

Anaingia kwenye kikosi hiki kwa uwezo wake wa kukaba, kuituliza timu na kutengeneza mashambulizi, huku akiwa msaada wa eneo la ushambuliaji na wale wanaolinda lango, akifunga mabao mawili na kuasisti mara tano.

Reliants Lusajo (Namungo)

Katika nafasi ya mshambuliaji namba moja wa kikosi cha kwanza, kuna majina mengi makubwa, akiwamo John Bocco, Clement Mzize na Anwary Jabir, lakini ki ukweli ni ngumu kumuacha nahodha huyo wa Namungo.

Lusajo amekuwa na muendelezo mzuri kwa washambuliaji wazawa kwa kufunga karibu kila msimu mabao yasiyopungua 10, japo kwa sasa ametupia nane wakati ligi ikielekea ukingoni.

Mbali na kufunga na kusumbua mabeki, lakini Lusajo anafaida nyingine ya kuasisti na kuchangia sehemu kubwa ya upatikanaji wa mabao, japo kasi yake imepungua kwa majeraha anayopata mara kwa mara.

Jeremiah Juma (Tanzania Prisons)

Mshambuliaji huyo aliyerejesha makali yake baada ya kuanza kwa kusuasua msimu huu sasa amerudi kwenye moto wake akitupia na kuisaidia timu yake kupata matokeo mazuri kwenye Ligi.

JJ anajua kufunga na ni mmoja ya washambuliaji wajanja ambao akikutana na beki zembezembe anajua kuwatia adabu na uwezo wake wa kupiga chenga, kujipanga na kumiliki mpira mbali na kufunga unamfanya aingie kwenye skwadi hili la kwanza la mapro wazawa. Hadi sasa ana mabao tisa.

Sixtus Sabilo (Mbeya City)

Mbeya City bado inapambana kujiokoa isishuke daraja, lakini hii haiwezi kumzuia Sixtus Sabilo kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha chama la mapro wazawa kutokana na kasi kubwa aliyoifanya hadi sasa katika Ligi Kuu.

Ni mmoja ya wachezaji wenye kuhusika na mabao mengi, akifunga tisa na kuasisti sita, huku akiwa na uwezo wa kukimbiza mabeki wa timu pinzani na kutengeneza mashambulizi makali.

Rekodi za misimu sita aliyopo kwenye Ligi Kuu Bara akipitia timu mbalimbali zimezidi kumuongezea nafasi ya kuanza kikosi hiki kutokana na ukweli jamaa anatumika nafasi mbalimbali uwanjani.

MAKOCHA: Fred Felix 'Minziro' wa Geita Gold akisaidiana na Mecky Maxime wa Kagera Sugar.

KIKOSI CHA AKIBA:

Metacha Mnata (Yanga), Shomary Kibwana (Yanga), Yahya Mbegu(Ihefu), Ibrahim Bacca(Yanga), Lenny Kissu(Ihefu), Sospeter Bajana (Azam), Idd Seleman 'Nado' (Azam), Rafael Daud (Ihefu), Elias Maguri (Geita Gold), Matteo Anthony (KMC) na Abdul Seleiman 'Sopu' (Azam).

Chanzo: Mwanaspoti