Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa mechi hizi, Yanga wametoboa...

Mayele X Lomalisa Kwa mechi hizi, Yanga wametoboa...

Wed, 4 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi imesimama kwa muda mfupi kupisha fainali za kombe la Mapinduzi lakini vigogo Simba na Yanga wote akili zao pia zipo kwenye ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Timu zote zimecheza mechi 19, huku Yanga ikiwa kinara kwenye msimamo na pointi 50 na Simba ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 44 na nafasi ya tatu Azam ikiwa na pointi 40.

Kwenye mbio za ubingwa bila shaka ni Yanga na Simba kwani kocha msaidizi wa Azam Fc, Kally Ongala alishajitoa baada ya kupoteza dhidi ya Yanga kwa mabao 3-2.

Mechi tisa zijazo ambazo zina pointi 27, ndio zinatoa taswira halisi ya nani atakuwa bingwa msimu huu kwa kuangalia nani atakuwa nyumbani sambamba na timu ambazo itazikutana nazo pamoja na matokeo ya mzunguko wa kwanza.

Simba kwenye mechi zake tisa zijazo itakuwa na mechi tano nyumbani (uwanja wa Mkapa) na mechi nne ugenini.

Simba inatakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inapata matokeo kwenye mechi zote za nyumbani na ugenini ili kujiweka sawa zaidi itaanza kutupa karata yake ya kwanza nyumbani Januari 17, dhidi ya Mbeya City huku mchezo wa kwanza msimu huu ikitoka sare 1-1, ugenini.

Baada ya hapo Simba itaenda kucheza ugenini dhidi ya Dodoma Jiji (Januari 22), kisha itakuwa na mechi mbili ngumu nyumbani dhidi ya Singida Big Stars (Februari 3) na Azam Fc (Februari 21).

Simba kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Singida ilitoka sare 1-1 katika Uwanja wa Liti huku dhidi ya Azam ikipokea kichapo cha 1-0.

Baada ya mechi hizo Simba itaendelea kuwa nyumbani ikiikaribisha Yanga katika Uwanja wa Mkapa (April 9), huku mchezo wa kwanza ukimalizika kwa sare 1-1 na kwa sasa timu zote zipo kwenye mbio za kusaka ubingwa.

Machi 11, Simba itakuwa na kazi ya ziada ugenini kwenye Uwanja wa Manungu dhidi ya Mtibwa Sugar kisha itasafiri hadi mkoani Mbeya kucheza na Ihefu katika Uwanja wa Highland State (April 15), na baada ya hapo itasubiri tarehe ya mchezo wao wa ugenini dhidi ya Namungo.

Upande wa Yanga yenyewe ni kama vile inateleza kwa sababu mechi zake saba kati ya tisa, sita itakuwa ipo nyumbani kisha mechi ya Singida Big Stars, itakuwa ugenini huku mechi mbili za ugenini dhidi ya Simba na KMC ni kama yupo nyumbani tena kutokana na timu hizo kutumia Uwanja wa Mkapa.

Yanga msimu huu amepoteza pointi nne tu kwenye Dimba la Mkapa, akiwa alitoka sare na Simba na kutoka sare dhidi ya Azam, lakini tatu alipoteza mkoani aliopofungwa na Ihefu.

Yanga itaanza kutupa karata yake ikiwa nyumbani Januari 18, dhidi ya Ihefu huku ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa 2-1, mzunguko wa kwanza na kuvunjiwa rekodi ya kutokufungwa mechi 49, iliyochezwa katika Uwanja wa Highland State.

Baada ya mechi hiyo Yanga, itaendelea kuwa nyumbani ikicheza na Ruvu Shooting na Namungo huku mechi za mzunguko wa kwanza ilishinda zote ikiwa ugenini (Ruvu Shooting 1-2 Yanga) (Namungo 0-2 Yanga).

Yanga baada ya mechi hiyo, itakuwa na kibarua kingine dhidi ya KMC huku mchezo wa kwanza waliocheza, Yanga ilishinda 1-0, bao lililofungwa na Feisal Salum Fei Toto dakika za mwishoni.

Mchezo huo kwa asilimia kubwa unaweza kuchezwa nje ya Dar lakini KMC haijawa na matokeo mazuri inapocheza nje dhidi ya Yanga. Baada ya hapo April 9, Yanga itaendelea kuwa ugenini dhidi ya Simba mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa na matokeo ya mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare 1-1.

Yanga itaendelea kubaki Dar kwa michezo miwili dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar, lakini Yanga kwenye mzunguko wa kwanza ilizifunga timu hizo kwa bao 1-0 kila mmoja.

Yanga itakuwa na mchezo wa ugenini dhidi ya Singida na itarudi tena nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji lakini mechi zote bado hazijapangiwa tarehe na kwa dalili ilivyo, Yanga anaweza kwenda ugenini akiwa na asilimia 90 ya ubingwa kama rekodi yake ya Mkapa itaendelea.

WADAU WAFUNGUKA Mshambuliaji wa zamani Yanga, Hery Morris, alisema kutokana na mechi ambazo Yanga imebaki nazo katika Uwanja wa Mkapa, benchi la ufundi na wachezaji wanatakiwa watulie kuhakikisha wanapata matokeo kwani wapo kwenye uwanja wao.

"Njia rahisi zaidi kwa Yanga kwa sababu uwanja ni mzuri, kwa Mkapa Simba na Yanga ndiyo sehemu kubwa wachezaji wao huwa wanatulia kwa hiyo unaona kabisa Yanga ina nafasi kubwa,"alisema Morris.

Upande wa mshambuliaji wa zamani Simba na Mtibwa Sugar, Abdalah Juma, alisema hakuna ugumu wala wepesi wa kucheza nyumbani au ugenini badala yake wachezaji wajitume.

"Simba na Yanga zina nguvu zaidi ugenini kuliko hapo Dar, Simba ambayo ina hizo mechi nyingi nje isiwe na wasiwasi badala yake wachezaji wake wajitume kila kitu kinawezekana,"alisema Juma.

Chanzo: Mwanaspoti