Simba Sc na Yanga Sc kwa jinsi ambavyo zimesajili kwa ajili ya kuanza msimu wa 2023/24, basi fahamu kuwa kuna balaa kubwa litatokea.
Hiyo ni kutokana na kila timu kushusha mashine za maana ambazo kwa namna moja ama nyingine msimu ujao moto utawaka katika kuwania mataji ya ndani ambayo yote yanashikiliwa na Yanga.
TanzaniaWeb.com tumekuletea vikosi vya Yanga na Simba kwa ajili ya msimu ujao ambapo kila timu malengo ni kutwa kila taji ambalo watashindania.
Yanga ambayo hadi jana jioni ilikuwa imetambulisha wachezaji wapya watano, kikosi chao kipya kitaonekana hivi;
DJIGUI DIARRA
Alikuwa na kikosi msimu wa 2022/23, raia huyu wa Mali aliibuka kuwa Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara. Katika eneo hili, hana mpinzani licha ya uwepo wa Metacha Mnata na Aboutwalib Mshery.
YAO ATTOHOULA
Huu ni usajili mpya wa Yanga akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast. Beki huyu wa kulia anatarajiwa kuwa katika kikosi cha kwanza kama mbadala wa Djuma Shaban.
NICKSON KIBABAGE
Ni usajili mpya kutoka Singida Fountain Gate, anakwenda kushindania namba na Joyce Lomalisa katika beki wa kushoto, licha ya kuwa na uwezo wa kucheza winga.
GIFT FRED
Beki wa kati raia wa Uganda, amejiunga na Yanga hivi karibuni akitokea SC Villa ya Uganda. Katika beki wa kati, atania namba na Ibrahim Hamad ‘Bacca’.
BAKARI MWAMNYETO
Nahodha wa Yanga, amerudi katika ubora wake, msimu ujao anatarajiwa kuendelea pale alipoishia msimu uliopita. Dickson Job atakuwa mbadala.
KHALID AUCHO
Kiungo raia wa Uganda, alikuwa na timu tangu msimu uliopita, katika eneo la kiungo namba 6 akiwa fiti, hana mpinzani ingawa mbadala wake ni Zawadi Mauya.
MAXI MPIA
Hili ni ingizo jipya, msimu ujao eneo la winga wa kulia anatarajia kulishikilia, licha ya kuwepo namba kubwa ya wachezaji kama Jesus Moloko na Denis Nkane.
JONAS MKUDE
Mkude ambaye ni mzoefu wa Ligi ya Tanzania, msimu ujao akiwa na jezi ya Yanga anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi akicheza kama namba 8 pembeni ya Khalid Aucho. Hapo ngoma itakuwa ngumu kutokana na uwepo wa Salum Aboubakar ‘Sure Boy’.
FISTON MAYELE
Kitendawili kikubwa bado kipo kwa Mayele akama atabaki ama ataondoka, lakini mshambuliaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na kama atabaki basi ataendelea kucheza namba 9. Mbadala wake Clement Mzize.
STEPHANE AZIZ KI
Katika eneo la namba kumi hana mpinzani kwani baada ya kuondoka Feisal salum, ameimiliki namba hiyo, mara nyingine huwa anasaidiwa na Mudathir Yahya.
KENNEDY MUSONDA
Faida ya Musonda licha ya kuwa ni mshambuliaji wa kati, lakini bado jamaa ana uwezo mkubwa wa kucheza pembeni kama winga wa kulia na winga wa kushoto, hivyo atatumika pembeni kama winga wa kushoto ambapo Farid Mussa naye hucheza.
Baada ya kuona kikosi cha Yanga, upande wa Simba SC mambo yatakuwa hivi;
AISHI MANULA
Ni kipa namba moja, kwa sasa anauguza majeraha, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kurudi kikosi cha kwanza akipona. Mbadala wake Ally Salim.
SHOMARI KAPOMBE
Beki wa kupanda na kushuka, ameletewa damu changa, Davi Kameta ‘Duchu’, watakuwa wakipokezana upande wa kulia.
MOHAMED HUSSEIN
Beki wa kushoto, upande wake hana mpinzani kabisa, hivyo bado atatesa kikosi cha kwanza. Israel Mwenda anaweza pia kucheza upande huu.
HENOCK INONGA
Beki wa kati raia wa DR Congo, ana uwezo wa kupanda kushambulia wapinzani na kushuka kuzuia, ana nafasi kikosi cha kwanza.
CHE MALONE FONDOH
Ingizo jipya ndani ya Simba raia wa Cameroon, anaingia kikosini kutokana na kuondoka kwa Joash Onyango na Mohamed Ouattara. Kennedy Juma atakuwa mbadala wake.
MZAMIRU YASSIN
Kiungo wa kazi ngumu, anafunga anatoa pasi za mabao, ana nafasi kikosi cha kwanza. Nassor Kapama mbadala wake.
FABRICE NGOMA
Ingizo jipya raia wa DR Congo, ana uwezo wa kupanda na kushuka, hivyo anaongeza nguvu kwenye eneo la kiungo mkabaji ambapo kuna vita na Sadio Kanoute.
CLATOUS CHAMA
Kiungo mnyumbuli raia wa Zambia, ana nafasi yake kikosi cha kwanza licha ya msimu ujao kuwa na ushindani mkubwa ambapo huenda wakati mwingine akacheza Saidi Ntibazonkiza.
LUIS MIQUISSONE
Winga ambaye aliwahi kucheza Simba, anatajwa kuwa njiani kurejea kikosini hapo. Nafasi yake kuna watu kama Peter Banda na Pape Sakho.
AUBIN KRAMO
Ni kiungo mshambuliaji kutoka ASEC Mimosas, anapewa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza ndani ya Simba kutokana na uzoefu wake kimataifa. Kibu Denis ni mshindani wake.
JEAN BALEKE
Eneo la ushambuliaji atapewa kazi Jean Baleke licha ya uwepo wa John Bocco na Moses Phiri.